WANACHAMA MFUMO WA HIARI WAJIUNGA NSSF

0
699


Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

Wananchi wa kada mbalimbali wamejitokeza na kujinga na mfumo wa hiari wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), kupitia kampeni ya zamu yako ambao huwawezesha kujiwekea akiba ya maisha yao ya baadaye pindi wanapofikia umri wa kustaafu.

Kampeni hii ya sasa ya zamu yako ni maalumu kwa Watanzania wote walipo kwenye sekta isiyo rasmi wa hapa nchini ambao wamejiajiri wenyewe katika shughuli mbalimbali za kujiongezea kipato.

Akizungumzia kampeni hiyo, Ofisa Matekelezo wa NSSF, Abbas Cothema, alisema wananchi wengi wanaendelea kujitokeza kwa wingi baada ya kuelewa kuhusiana na mifuko ya hifadhi ya jamii.

Alisema hatua hiyo inaonesha mafanikio makubwa kupitia kampeni ya zamu yako.

“Kwa kweli uelewa kwa sasa kwa wananchi ni wa hali ya juu kwani wengi wameamua kujiandikisha na mpango huu wa hiari bila kushurutishwa na mtu yeyote haya ni mafanikio makubwa sana kwa NSSF,” alisema Cothema.

Alisema kwa sasa wanaendelea na kampeni hii katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam, baada ya kupata maombi mengi kwa wadau wanaofanya shughuli mbalimbali za kijamii na hivyo wanahamasisha na kuandikisha wananchi mbalimbali.

Kwa mujibu wa Cothema, hadi sasa wamefanikiwa kupata wanachama wengi katika zaidi ya mikoa 15 ambapo wengi wao wamejiunga kupitia mpango wa hiari.

“Tunashukuru kwa sasa wananchi wanaendelea kuelewa kuhusiana na umuhimu wa kujiandikisha kwa hiari jambo ambalo linapelekea baadhi ya vikundi vinavyojumuisha wajasiriamali vimeendelea kuleta maombi ya wanachama wao kupewa elimu ya kujiwekea akiba na baadaye waweze kujiunga kwenye mpango huu wa hiari,” alisema.

Kwa mujibu wa utaratibu wa NSSF, kiwango cha chini cha kujiandikisha kwenye mpango huo wa hiari ni kuanzia Sh 20,000 na kuendelea ambapo mwanachama anayejiunga anafaidika na mafao sita yanayotolewa na NSSF yakiwemo mafao ya pesheni ya uzeeni  na matibabu bure kwa mwanachama na mwenza, watoto wasiozidi umri wa  miaka 18.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here