24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Waliotumbuliwa na JPM sasa wafika 17

Nora Damian –Dar es Salaam

NOVEMBA mwaka juzi, Rais Dk. John Magufuli alisema ataendelea kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri pale patakapokuwa na uhitaji wa kufanya hivyo.

Alisema amekuwa akilazimika kumtuma Waziri Mkuu na wakati mwingine kumpigia simu hata saa 8 usiku akimtaka awakumbushe mawaziri wake kazi za uwaziri ni utumwa, hivyo lazima wawe watumwa wa watu masikini.

“Kazi hii ni ngumu na ni utumwa, mimi sitashangaa, hata nikibaki na mmoja wala sitajali. Kubadilisha ni ‘very simple’, wabunge wako 300 nafanya ‘rotation’ tu ili kusudi nipate matokeo,” alisema Rais Magufuli.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, anafanya idadi ya mawaziri na naibu mawaziri walioondolewa katika nafasi zao kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kufikia 17.

Katika idadi hiyo, mawaziri 15 waliondolewa kwa kutumbuliwa na wawili walijiuzulu.

WALIOJIUZULU

Waliojiuzulu ni aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene na aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani.

Septemba 7, mwaka juzi, Simbachawene aliandika barua ya kujiuzulu baada ya kutajwa katika ripoti ya uchunguzi wa biashara ya madini ya Tanzanite na almasi iliyoonyesha namna Serikali ilivyopoteza matrilioni ya fedha kutokana na sababu mbalimbali.

Hatua hiyo ilikuja muda mfupi baada ya Rais Magufuli kuwataka viongozi wote ambao wametajwa katika ripoti hiyo wakae pembeni kupisha uchunguzi ambao utakuwa huru na wa haki.

Ngonyani naye alijiuzulu baada ya kutuhumiwa kutotekeleza majukumu yake kikamilifu, alipokuwa akifanya kazi Shirika la Madini la Taifa (Stamico) lenye dhamana ya kusimamia madini.

WALIOTUMBULIWA

Mei 20, 2016, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, aliondolewa katika nafasi yake kwa tuhuma za kuingia bungeni akiwa amelewa.

Mei 23, 2017, Nape Nnauye (Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo) alitumbuliwa siku moja baada ya kupokea ripoti kutoka kwa kamati aliyokuwa ameiunda kuchunguza sakata la kuvamiwa kwa ofisi za Clouds Media Group.

Mei 24, 2017, Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Profesa Sospeter Muhongo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini kufuatia sakata la mchanga wa madini (makinikia) wa Kampuni ya Acacia.

Januari 19, 2018, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu aliyekuwa akishughulikia walemavu, Dk. Abdallah Possi na kumteua kuwa balozi.

Pia Oktoba 7, 2018, wakati alipofanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kwa kuongeza idadi ya wizara, alitengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe huku nafasi yake ikichukuliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangala.

Katika mabadiliko hayo, Mhandisi Ramol Makani naye aliachwa na nafasi yake ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii ilichukuliwa na Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga.

Mwingine ni Anastazia Wambura aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Juliana Shonza.

Aidha Julai 2018, Rais Magufuli alifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri na kumtupa nje aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, huku nafasi yake ikichukuliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola.

Rais Magufuli alisema Mwigulu alishindwa kushughulikia azimio la Bunge kuhusu suala la kufunga mashine za kielektroniki za utambuzi wa alama za vidole (Afis) katika vituo 108 vya polisi, mradi uliofanywa na Kampuni ya Lugumi kwa gharama ya Sh bilioni 37. 

Septemba 2018, Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Dk. Susan Kolimba aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kumteua Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Damas Ndumbaro kuchukua nafasi hiyo.

Wengine ni Charles Mwijage (Wizara ya Viwanda) na Dk.  Charles Tizeba (Wizara ya Kilimo) ambao waliondolewa Novemba 2018, kwa kushindwa kushughulikia bei ya korosho, kahawa, pareto na ufufuaji wa Kiwanda cha Chai Mponde kilichopo mkoani Tanga na kile cha Buko mkoani Lindi.

Rais Magufuli alieleza hadharani kuwa hakuona taarifa yoyote ya Waziri wa Viwanda au Kilimo kukemea sekta binafsi.

Alisema kiwanda cha chai kilikaa bila kufanya kazi kwa miaka minane hadi alipomtuma Waziri Mkuu kwenda kutatua tatizo na kwamba Kiwanda cha Mponde na cha Lindi havikurudishwa na wizara na hata mchakato wake mawaziri husika hawakuujua.

Mwingine aliyeondolewa ni Gerson Lwenge aliyekuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji.  

Pia aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda, naye aliondolewa kisha nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa.

Kakunda aliondolewa kufuatia malalamiko yaliyoelekezwa katika wizara yake na wafanyabiashara waliokutana na Rais Ikulu, Dar es Salaam mwaka jana.

Aidha Julai 21 mwaka jana, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba na kumrejesha tena Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene kuchukua nafasi hiyo.

Wakati akimwapisha Simbachawene, Rais Magufuli alitaja sababu za kumng’oa Makamba kuwa ni pamoja na kutotekelezwa kwa wakati kwa katazo la mifuko ya plastiki na kutotumika vizuri kwa fedha zinazotolewa na wafadhili kwa miradi ya mazingira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles