27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Waliosoma Azania wakabidhi madawati

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM

WANAFUNZI waliosoma Shule ya Sekondari Azania mwaka 1989 -1992 wameichangia madawati 100 yenye thamani ya Sh milioni 15.

Pia wamewataka wanafunzi wanaoendelea kusoma kutoipotezea sifa ya ufaulu shule hiyo kama ambavyo ilivyokua awali.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Mwenyekiti wa Azania Alumni mwaka 1989 -1992,  Daudi Machoya alisema waliamua kufanya hivyo kutokana na mchango wa shule hiyo katika maisha yao katika elimu.

Machoya alisema hiyo ni mradi mmoja na nyingine zinafuata katika kuhakikisha wanaonyesha mchango wao wa maendeleo katika shule hiyo.

Alisema wakiwa katika umoja wao wa kutumia mtandao wa simu   walijadiliana  kwa nini shule hiyo kwa sasa haifanyi vizuri.

“Baada ya kujadili tulimtuma mwakilishi wetu ambaye ni mtangazaji  wa Clouds, Harris Kapiga kuangalia changamoto zilizopo na kuzungumza na walimu pia.

“Kapiga alirudi na kutuelezea upungufu wa madawati pamoja na ukarabati wa jengo la shule hiyo ambayo serikali tayari imeshaanza kuikarabati,” alisema Machoya.

Alisema baada ya hapo wakaangalia kila mwananfunzi mmoja aweze kuchangia mpaka walipofanikiwa kupata madawati hayo 100.

Alisema wapo na wenzao katika umoja huo Marekani, Finland, Sweden na China ambao kwa pamoja walijumuika na kuona umuhimu wa kurudisha fadhila hizo.

Lakini pia alisema wameshtushwa na matokeo mabaya  ambayo wanaendelea kuyapata kwa sasa katika mitihani ya taifa.

“Zamani ilikua na historia, tulikuwa  tunapata daraja la kwanza  90-100 lakini sasa idadi imeshuka na sifuri kuongezeka… kunahitajika jitihada za makusudi  katika hili,” alisema Machoya.

Katibu wa umoja huo, Abdi Abuu maarufu kwa jina la ‘Mpole’ alisema kikundi chao kilianza mwaka 2014   lengo likiwa ni mikakati endelevu wa kuisaidia shule hiyo.

Akipokea msaada huo, Kaimu Mkuu wa shule, Casian Mbunda aliwashukuru na kuwataka wadau wengine kujitokeza kusaidia kwa sababu  bado wana mahitaji ya miundombinu.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa shule hiyo, Shangwe Mtei aliushukuru umoja huo kwa kuwaboreshea miundombinu na kuahidi watafanya vizuri katika masomo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles