27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WALIOPEWA VIWANJA CDA WAPEWA MWEZI MMOJA

Na RAMADHAN HASSAN

-DODOMA

MANISPAA ya Dodoma imetoa siku 30 kwa wale wenye barua za kupewa viwanja walipie na wasipofanya hivyo vitagaiwa kwa watu wengine.

Pia imetoa siku 90 kwa wale ambao  hawajaendeleza viwanja vyao kufanya hivyo, vinginevyo watanyang’anywa na kugaiwa watu wengine.

Hayo yalielezwa jana mjini hapa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema kwa wale waliopewa barua wanatakiwa kutambua kwamba bado hawajawa wamiliki ila wanatakiwa kulipia ndipo wapate uhalali kwa mujibu wa sheria.

“Viwanja vya ofa vipo 18,000. Hawa ni wamiliki halali wa viwanja, lakini kuna wale wenye barua za viwanja wao wapo 22,000. Hawa hawajakamilisha umiliki wa viwanja kwa hiyo sio wamiliki halali,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema kuna watu wamepewa barua za kulipia viwanja, lakini wamekuwa wakizunguka nazo kutafuta wateja kuwauzia na kwamba ofisi yake haitavitambua.

“Kuna mtu alipewa kiwanja na CDA barua ya toleo, mwingine ana viwanja zaidi ya 40 mtu mmoja, nasema kwa sababu najua ukimwangalia hajalipa hata kiwanja kimoja isipokuwa anatembea na hizo barua anatafuta wateja kwa ajili ya kuuza viwanja hivyo, hawa wakiuza wanafanya kosa.

“Kwani wewe sio mmiliki, hivyo natoa ‘notice’ ya siku 30 kwa wananchi wote wa Dodoma pamoja na Watanzania wote waliopewa barua za kupewa viwanja walipie viwanja vyao ndani ya siku 30 kuanzia tarehe 28, mwezi huu (jana) baada ya hapo tutachukua viwanja hivyo na kuwapa wananchi wengine,” alisema.

Alisema hawanyang’anyi viwanja hivyo bali wanatwaa kwa mujibu wa sheria, lengo likiwa ni kila mmoja aweze kumiliki kiwanja mkoani Dodoma.

“Baadhi yao walikuwa wanatumwa kuuza viwanja hivyo na watumishi ambao hawakuwa waaminifu wa CDA, tumebaini hilo, mtu kwa sababu alikuwa mkuu sehemu fulani unakuta ana viwanja 40 anatafuta madalali wanapewa barua hizo, tunataka Watanzania wapate viwanja wajenge Dodoma,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema wapo wanaomilki viwanja zaidi ya miaka mitano zaidi ya kimoja, lakini wamekuwa hawaviendelezi, hivyo manispaa itavichukua na kuwapatia wananchi ili waweze kuviendeleza.

Mkurugenzi huyo alitoa rai kwa Watanzania wanaotaka kujenga Dodoma wasinunue viwanja ovyo kwani kuna utapeli unaendelea.

Kunambi alisema baada ya kufanya tathmini, viwanja vilivyopimwa na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ni takribani 65,000 viliandaliwa ambapo kati ya hivyo 6,000 vilikuwa havijakamilika, huku 25,000 vilikuwa vimeandaliwa hati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles