30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WALIOPANDISHA BEI SARUJI KUSAKWA KILA KONA

Na GABRIEL MUSHI-DAR ES SALAAM


WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, ametangaza kuanza kuchukua hatua za kuwafutia leseni mawakala wote wanaouza saruji kwa bei ya juu licha ya kutokuwapo kwa upungufu wa bidhaa hiyo kwa sasa.

Hatua hiyo imekuja baada ya kutengemaa kwa mitambo ya uzalishaji malighafi ya saruji katika viwanda kadhaa nchini, ambayo ilisababisha uhaba wa saruji sokoni kwa zaidi ya siku 20.

Mwijage alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam wakati alipotembelea kiwanda cha Tanzania Portland Cement (Twiga) kilichopo Wazo na Camel Cement Company kilichopo Mbagala.

Akizungumza na uongozi wa kiwanda kinachozalisha saruji ya Twiga, Mwijage alisema lazima baadhi ya mawakala watolewe kafara ili kudhibiti hali hiyo.

Pia aliuagiza uongozi wa kiwanda hicho kuwaelekeza mawakala wanaosambaza saruji wanayozalisha kushusha bei ya bidhaa hiyo kutoka Sh 18,000 katika baadhi ya maeneo hadi kufikia Sh 13,500 au bei ambayo wamekubaliana na wazalishaji hao.

“Mimi nimefanya kazi hapa miaka 18, nafahamu mchezo wote wa vijana wako wanaoufanya, ndiyo maana nakuagiza uniletee orodha ya mawakala wote wanaosambaza saruji ili niwabaini na kuwafutia leseni.

“Kwa sababu sasa Dangote anazalisha tani 4,500 kutoka tani 2,000 kwa siku, Twiga anazalisha tani 6,000 kutoka tani 3,500 kwa siku, Tembo tani 1,100, Nyati tani 2,000 hivyo hakuna uhaba wa saruji sasa. Tayari hali imetengemaa ila kwanini bei iendelee kubaki juu.

“Kiujumla kwa siku tunazalisha tani 16,000 na sasa tunatumia tani milioni 5.8 kutoka tani milioni 4.8 kwa mwaka na viwanda vyote vilivyosimikwa sasa vina uwezo wa kuzalisha tani milioni 10.5 kwa mwaka,” alisema.

Aidha, alisema ili kuendelea kuhimili soko la ndani na la nje, tayari kuna viwanda vitatu ambavyo ni cha Mamba,  Nyati namba 2 na kiwanda cha wachina cha Engian ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha malighafi inayotumika kuzalisha saruji zaidi ya tani milioni saba kwa mwaka.

“Suala hili la saruji kupanda, naomba watu wanivumilie, dawa ya kupanda naijua, saruji imejaa sokoni, bei inashuka yenyewe, ila wale wanaopandisha inaitwa ‘profiteering’ siku ya kiama inshallah basi hukumu ni yao kama wanataka kuishi duniani shauri yao hukumu ni yao.

“Bahati mbaya Camel anaishia Dar es Salaam ila wale kina Twiga, Simba na Dangote wapeleke mikoa ya pembezoni yaani Simiyu, Kagera, Geita na Katavi, saruji ipelekwe kule na ninawapa deadline baada ya muda fulani nitakwenda kusimamia hayo malori yashushe,” alisema.

Meneja Undelezaji Biashara wa Kampuni ya Saruji ya Twiga (TPCC), Mhandisi Danford Semwenda  alisema ni kazi ngumu kuwadhibiti mawakala wa uuzaji wa saruji hiyo hivyo wanaomba ushirikiano kutoka serikali ili kudhibiti hali hiyo.

“Sisi hatujapandisha bei, na wala mawakala wetu hatuna uhakika kama wamepandisha bei ila ili kudhibiti hali hii inabidi tushirikiane,” alisema.

Naye Meneja Mkuu Msaidizi wa Kiwanda cha Camel, Ghalib Hassan , alisema upatikanaji wa malighafi ya kuzalisha saruji ‘clinker’ umeendelea kuwa changamoto kwao.

Alisema kutokuwapo kwa umeme wa uhakika nao umekuwa kikwazo kwa kiwanda hicho kufikia malengo ya kuzalisha tani 600 kwa siku na hivyo kuzalisha tani 400.

“Clinker tulikuwa tunanunua dola 35 lakini sasa inaelekea dola 70 hivyo kuongeza gharama za uzalishaji. Hata hivyo tunaendelea kupanua kiwanda chetu na hadi kufikia Disemba mwaka huu tutaweza kuzalisha tani 2,400 kwa siku ili tukidhi na kuanza kuuza nje ya Dar es Salaam,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles