25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Walionyooshewa kidole na JPM wafunguka

Na EVANS MAGEGE

BODI ya Pamba Tanzania (TCB) imefunguka kuhusu agizo la Rais Dk. John Magufuli kwa kuelezea mikakati yake ya usimamizi wa zao la pamba nchini.

Leo zinatimia siku 13 tangu inyooshewe  kidole na Magufuli kwa kutakiwa ijiandae baada ya kile kilichotokea kwa Bodi ya Korosho (CBT).

Novemba 12, mwaka huu wakati Magufuli akiwaapisha mawaziri wawili na manaibu wanne baada ya kufanya mabadiliko madogo ya Baraza lake la Mawaziri, alisema baada ya CBT, TCB pamoja na bodi nyingine za mazao zijiandae huku akieleza bayana kwamba Serikali itakuwa inapitia utendaji kazi kwa kila bodi.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa njia ya simu katikati ya wiki hii, Mkurugenzi wa TCB, Marco Mtunga, alisema kauli hiyo ya Magufuli ni amri, hivyo wao kama bodi wameichukua kwa uzito mkubwa wa kuhakikisha tija ya zao la pamba inaongezeka kwa mkulima.

Alisema kwa tafsiri ya kawaida juu ya kauli hiyo, inamaanisha msimamo wa Serikali wa kuhakikisha wakulima wake wanapata bei nzuri kwa mazao yao.

“Kauli ya Rais ni amri hivyo tumeichukulia kama maelekezo ya Serikali, na kawaida huwezi kuijadili amri kwamba ukubali au ukatae, bali kikubwa kwetu sisi kama watendaji tumejipanga kutekeleza yale ambayo Serikali inataka,” alisema.

Alipoulizwa ni tatizo gani ambalo wao kama bodi wanaona linawasumbua katika kuliendeleza zao la pamba, alijibu kwa kifupi kwamba ni kilimo duni.

Pia alifafanua jibu lake kwa kusema kilimo duni kimesababisha wakulima kuambulia  tija ndogo kuliko nguvu wanayoitumia.

“Tija imekuwa bado ni ndogo, unakuta mkulima anazalisha kilo 200 au 300, lakini nguvu aliyoitumia ni kilo 1,000, hali hii inatokana na kilimo duni,” alisema.

 TCB WAMEJIPANGAJE?

Akizungumzia mipango yao ya muda mfupi na mrefu, alisema bodi hiyo inakusudia kutoka nafasi ya 10 ya uzalishaji wa pamba barani Afrika na kufika nafasi ya kwanza ifikapo mwaka 2022.

Alisema kwa msimu wa kilimo cha mwaka 2018/2019, wametenga Sh bilioni 42 kwa ajili ya uzalishaji wa zao hilo.

Alitoa ufafanuzi wa matumizi ya fedha hizo kwa kusema wametenga Sh bilioni 15.6 kwa ajili ya kununua tani elfu 22 za mbegu.

Katika mbegu hizo, alisema tayari bodi imeishagawa tani elfu 14, huku malengo ni kugawa tani elfu 18.

Pia alisema wananunua tani elfu nne za mbegu kwa ajili ya ziada kama ikitokea uhitaji mkubwa ndani ya msimu huu.

Alikwenda mbali zaidi kwa kusema bodi hiyo imetumia Sh bilioni 25 kwa ajili ya kununua chupa milioni sita za sumu ya kuua wadudu wanaoshambulia zao hilo.

Pia imetumia Sh bilioni 1.6 kwa ajili ya kununulia mabomba ya kunyunyizia dawa.

Alisema mbegu zote, vifaa pamoja viuatilifu watavisambaza katika mikoa 17 na wilaya 56 zinazolima pamba.

BEI YA MSIMU WA 2018

Akizungumzia malalamiko ya wakulima dhidi ya bei elekezi ya msimu wa mwaka huu kuwa ilikuwa ndogo, alisema Tanzania ilikuwa na bei nzuri ya kununua pamba kwa mkulima kuliko nchi zote jirani zinazolima zao hilo.

Alisema wakulima waliuza pamba kwa bei ya asilimia 80 ya bei ya soko la dunia,  kiwango kilichokuwa juu zaidi ya nchi kama Zambia, ambayo ni moja ya mzalishaji mkubwa wa zao hilo kwa nchi zinazopakana na Tanzania.

MALENGO YA SASA HADI 2022

Akizungumzia malengo ya muda mrefu ya bodi hiyo, alisema kulingana na ukubwa wa eneo la nchi, wamedhamiria kwamba ifikapo mwaka 2022, nchi iwe na uwezo wa kuvuna pamba kilo bilioni moja (tani milioni moja).

Alisema kiwango hicho kitaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kwa uzalishaji wa zao la pamba.

Alisema kwa wastani katika msimu wa mwaka huu nchi iliyoongoza kwa uzalishaji wa pamba barani Afrika ni Mali, ambayo ilizalisha kilo milioni 700.

“Ndiyo nasema tukifika kiwango cha uzalishaji wa kilo bilioni moja tutakuwa tumetimiza azma yetu ya kuwa wazalishaji wa kwanza barani Afrika, kwa msimu huu sisi tumeshika nafasi ya kumi kwa kuzalisha tani laki mbili na elfu 22,” alisema.

Pia alisema japokuwa ni mapema kutabiri, lakini kwa msimu ujao, kama wakulima watakuwa wamepata elimu ya kutosha ya kutunza mashamba, uvunaji wa pamba utaongezeka na kufikia tani laki tatu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles