33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Walioko kwenye utalii sasa kufanya mitihani

Faraja Masinde -Dar es salaam

SERIKALI imesema kuwa imeanzisha utaratibu wa kuwa na ithibati kwa wote walioko kwenye fani ya utalii ambapo kuanzia sasa watafanya mtihani maalumu, lengo likiwa ni kupata watu wenye viwango stahiki.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangala wakati wa kongamano la wadau wa sekta ya utalii linalokutanisha wataalamu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.

Dk. Kigwangala alisema kuwa mbali na kupata watu wenye viwango, lakini pia wanataka kuimarisha eneo la usalama na ubora ili kuwatambua wote walioko kwenye fani hiyo.

“Tumemua kwanza kuboresha kozi ambazo zinatolewa kwenye vyuo vya Serikali, lakini pia kuboresha mtaala ambao unatumika kwenye vyuo binafsi na kuanza kutoa kozi za uanagenzi, ambazo zinafundishwa kwa watu ambao walikosa mafunzo kwenye Chuo cha Taifa cha Utalii na kuyapata wakiwa kazini.

“Lakini pia tumeanzisha utaratibu wa kufanya ithibati kwa maana kwamba wewe soma kokote kule, lakini ukitaka kuajiriwa Tanzania kwenye ofisi ambazo zimesajiliwa na Serikali, utafanya mtihani maalumu ili kuwa na ubora unaohitajika,” alisema Dk. Kigwangala.

Alisema kuwa mkakati huo ulianzishwa miaka miwili iliyopita na kuwapa watu nafasi ya kusoma na kuanzia mwakani wataanza kuwakagua kwa lengo la kuhakikisha kuwa walioko kwenye sekta hiyo wanajulikana.

“Hivyo kila baada ya muda watakuwa wanarejea kupata mafunzo ili kuwaimarisha zaidi kama ilivyo kwenye sekta nyingine na kuwapa vyeti. Hii pia itasaidia katika kuongeza usalama kwa wageni wanaokuja.

“Hivyo hata mtu akihama au kuacha kazi tutakuwa na taarifa zake, hii itasaidia sana kuboresha huduma zinazotolewa kwenye utalii,” alisema Dk. Kigwangala.

Alisema ni muhimu katika kubadilisha ufahamu, uzoefu katika sekta hiyo kwani kuna wasomi ambao wanafanya tafiti mbalimbali zinazohusiana na utalii, lakini ni lazima waunganishwe katika mkakati huo.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dk. Shogo Sedoyeka, alisema kuwa waliona kuna haja kubwa ya kufanya mkutano huo kutokana na kuwapo kwa wahitimu ambao wamekuwa hawakidhi mahitaji ya soko hatua ambayo iliwalazimu kukaa na wadau.

“Hivyo tumekaa na wadau ili kuhakikisha kuwa tunapunguza changamoto hizi ili wahitimu wetu waweze kukidhi mahitaji hasa ya soko, ikiwamo namna ya kukuza ujuzi, uzoefu na namna ya kutambua tabia za wageni kwa kuwa wamekuwa na tabia mbalimbali.

“Pia katika chuo chetu kila mwaka wanafunzi 150 hadi 200 wanahitimu, lakini ni asilimia chache tu ndio wanaopata ajira hatua ambayo inaonyesha kwamba huenda hawakubaliki na soko au bado wanaendelea kusaka nafasi za ajira ikilinganishwa kwamba wahitimu ni wengi,” alisema Dk. Sedoyeka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles