25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

WALIOFUKIWA MGODINI WATOA ISHARA KUWA HAI

Na EMMANUEL IBRAHIMU -GEITA

MATUMAINI ya kuwapata hai wachimbaji 13, akiwamo Raia wa China, Meng Juping waliofukiwa Januari 25, mwaka huu katika Mgodi wa Dhahabu wa RZ Union, yameanza kujitokeza baada ya waokoaji kuanza kuwatumia wachimbaji wadogo wadogo ili kuepusha madhara zaidi, ikiwamo eneo hilo kutitia tena kwa uzito.

Dalili za wachimbaji hai kupatikana wakiwa hai zilijitokeza jana saa moja usiku baada ya kuanza kugonga bomba lililoingizwa na waokoaji wakati wakiendelea kuchimba, hivyo kutoa ishara ya mahali walipofukiwa. 

Awali akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Victoria, Yahaya Samamba, alisema baada ya kufikia mita 20, Kamati ya Uokoaji kwa kushirikiana Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Geita, ilibadilisha mfumo wa uokoaji na kuanza kutumia wachimbaji wadogo wadogo badala ya mashine za kisasa.

Alisema kwa sasa wanatumia wachimbaji wadogo wadogo wanaoingia ndani ya shimo la mita zaidi ya 25 na kuchimba kwa kutumia sururu, jembe na tindo, huku mchanga ukipandishwa kwa winchi kutoka juu na kila wanapochoka wamekuwa wakibadilishwa na wengine kuingia kuendela na ufukuaji.

“Mitambo hii imekomea eneo la mita 20, tumeona tutumie wachimbaji wadogo ili twende sambamba na uokoaji ulio salama zaidi, kwa hiyo usiku wa jana (juzi) kuanzia saa tano usiku tuliondoa magreda kwa sababu tumefika eneo laini, hivyo linaweza kusabisha maafa kwa sababu ya uzito,” alisema.

Samamba alisema wachimbaji wadogo wameanza kazi hiyo ya kufukua kama wanavyochimba dhahabu, wakifuata njia ya awali na kwa sasa mashine itafanya kazi nyingine pale itakapoonekana inafaa au eneo jingine watakaloamua kuanza uchimbaji kutafuta njia.

RAMANI ZAWAKWAMISHA

Katika hatua nyingine, Mhandisi wa Kampuni ya Mgodi wa Busolwa, Ibrahim Nayompa, alisema wamechelewa kuwaokoa waliofukiwa kutokana na ramani za awali zilizotolewa na wamiliki wa mgodi huo kutokubainisha kwa usahihi eneo walilokuwa wachimbaji hao wakati wakiangukiwa.

Alisema uokoaji umekuwa mgumu kutokana na kubahatisha eneo husika na sasa wanafanya kwa kubahatisha na hawana uhakika hali inayowalazimu wachimbaji waliofanya kazi katika mgodi huo kuwasaidia kwa kuwachorea picha za ramani mpya ili kuwapa mwanga eneo gani wanapaswa kuwatafuta.

“Mimi ninachokiona tunachelewa kuwaokoa kwa sababu wamiliki wa mgodi huu wameshindwa kutupatia ramani ya uhakika, sasa tunabahatisha tu, jana ulikuwa shuhuda namna mashine ilivyoshindwa kulenga na kutoboa kwenye eneo la shimo walipo ndugu zetu,” alisema.

Nayompa alisema hata hivyo wanaendelea na utafutaji kwa kutumia wachimbaji na matumaini yao watafanikiwa kuwafikia wakiwa salama licha ya changamoto hizo.

KALEMANI ATEMBELEA WAOKOAJI

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, alitembelea mgodi huo na kutoa pole kwa niaba ya Serikali kwa uongozi wa mkoa na wananchi na kuwataka waokoaji kuendelea na kazi hiyo kwa umakini, huku wakiangalia pia usalama wao.

Dk. Kalemani aliutaka uongozi wa mkoa na kamati ya uokoaji kujikita zaidi katika shughuli ya uokoaji na waachane na mambo mengine yanayoweza yakasababisha kazi iwe ngumu.

“Hata hivyo, mnapaswa kuangalia eneo hili na mwelekeo wake na toboeni njia upande mwingine kuelekea huku walikoangukiwa hao wachimbaji huku mkienda taratibu na mkiwafikia basi hata namna ya kuwapa chakula wakiwa hai iendelee,” alisema.

Baada ya kuwasili eneo hilo, alipokea taarifa ya maafa hayo iliyosomwa na Samamba na jinsi uokoaji unavyoendelea na hatua ambazo wamefikia.

Kwa upande wake, Mbunge wa Busanda, Lolensia Bukwimba (CCM), alisema alitembelea eneo hilo na kuwatia nguvu waokoaji na kuwaomba kuendelea na jitihada za kuwaokoa waliofukiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles