31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Walioandamana kumpongeza JPM wakutana na cha moto


ELIYA MBONEA-ARUSHA

WACHIMBAJI wadogo wa migodi ya madini ya Tanzanite iliyopo Mirerani, Simanjiro walioandamana kumpongeza Rais Dk. John Magufuli wamekutana na wasichokitarajia baada ya kutakiwa kuacha kusambaza umbea na taarifa za uongo zinazoisababishia Serikali hasara.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, alipokuwa akipokea maandamano ya amani ya wachimbaji hao waliokuwa wakimpongeza Magufuli kwa kupunguza baadhi ya kodi zilizokuwa kero kwao.

Akizungumza na wananchi, wachimbaji, wana apolo, mabroka, viongozi wa Chama cha Wachimbaji Madini Manyara (Marema), Mnyeti, aliwataka wachimbaji hao kuacha kulazimisha njaa zao kuwa njaa za taifa.

“Mirerani tuacheni uongo na umbea, hapa duniani ukitafuta watu waongo utawapata hapa. Mtu akifukuzwa kazi mgodini anaamua kwenda kumchongea kwa viongozi wa Serikali.

“Wapo baadhi wanadiriki kusema uongo eti tajiri fulani anatorosha madini nje ya nchi, tukifuatilia kupitia vyombo unakuta hakuna kitu kama hicho badala yake unaambulia mchanga tu.

“Umbea wenu umetufanya tushindwe kufanyia kazi taarifa mnazotupa badala yake tunaingia hasara kubwa, ukimbana aliyeleta taarifa atakuomba umsaidie kupata kazi kwenye mgodi aliokuja kuusemea eti ili awe anakuletea taarifa zaidi,” alisema Mnyeti.

Pia aliwataka wamiliki wa migodi na wafanyakazi wao kuingia makubaliano ili wakipatwa na magonjwa ikiwamo kifua kikuu kutibiwa kwa utaratibu.

“Nyinyi wachimbaji mmekuwa mkijichongea wenyewe mbele ya Serikali kutokana na kuwatelekeza watumishi wenu pindi wanapopatwa na ugonjwa wa TB.

“Hapa kuna matajiri wana kiburi cha kutelekeza wafanyakazi wao, natangaza mfanyakazi wako akija ofisini kwangu kulalamika ametelekezwa baada ya kuugua TB, nitaanza na wewe kukuweka ndani wakati tukishughulikia kesi yao.

“Na nyinyi wachimbaji nawaagiza msikubali kuingia kazini bila kuwa na mkataba na mwajiri wako ili ukiugua akuhudumie,” alisema Mnyeti.

Pia aliwataka wachimbaji hao kulipa kodi bila kusukumwa kwa sababu Serikali iliyopo si ya ujanja ujanja.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Marema, Justine Nyari, alisema maandamano hayo yalilenga kumpongeza Magufuli kwa kuondoa baadhi ya kero za madini kwao.

“Kwa hatua hii ya Rais Magufuli kwetu tunaahidi kushirikiana na Serikali kwa kulipa kodi zinazostahili,” alisema Nyari.

Naye mmoja wa Wakurugenzi wa Kampuni ya Tanzanite One, Faisal Juma, alisema dhamana aliyoitoa kwao wataichunga kwa kulipa kodi stahiki.

“Tumejipanga kulipa kodi zilizosalia ili kulisaidia taifa letu kwa kizazi cha sasa na kijacho viishi maisha ya raha,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Chama cha Wafanyabiashara na Wauzaji wa Madini (Tamida), Hussein Gonga, alisema Magufuli alisikia changamoto zao na kuzifanyia kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles