WALIMU WASOMEWA SHTAKA LA KUUA MWANAFUNZI KWA KUKUSUDIA

0
460

 

Na Renatha Kipaka, Bukoba


Walimu wawili Respicius Patrick Mtazangira na Herieth Gerald, ambao ni watuhumiwa wa mauaji ya mwanafunzi Sperius Eradius (13), aliyekuwa akisoma Shule ya Msingi Kibeta iliyopo Manispaa ya Bukoba, wamefikishwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Bukoba na kusomewa shtaka la mauaji.

Washtakiwa hao walisomewa shtaka lao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi John Kapogoro.

Katika kesi hiyo ya mauaji namba 18 ya mwaka 2018, watuhumiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi yao.

Mara baada ya kusomewa shtaka linalowakabili, Hakimu Kapogoro aliamuru warudishwe mahabusu kwani halina dhamana.

Akitoa ufafanuzi wa kesi hiyo, Kaimu Wakili wa Serikali Mfawidhi, Athuman Matuma, alisema ushahidi umekamilika na ofisi yake inaendelea na utaratibu wa kufungua jalada la kesi hiyo Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba.

Alidai kulingana na ushahidi uliokusanywa na kukamilika, mauaji ya Sperius yalikuwa ni ya kukusudia kutokana na silaha alizoshambuliwa nazo.

“Ushahidi wetu unaonyesha kuwa Mwalimu Respicius Mtazangira alikuwa anamshambulia mwanafunzi Sperius Eradius kwa vipande vya kuni vilivyokuwa vimekusanywa na wanafunzi wa darasa la saba kwa ajili ya kupikia chakula chao,” alidai Matuma.

Alidai kuwa pamoja na Sperius kupiga kelele kuwa anauawa akiomba msaada kwa wanafunzi wenzake, mwalimu Mtazangira aliendelea kumpiga.

Pamoja na ushahidi huo, Matuma alidai kuwa baadhi ya walimu walimwendea mwalimu Mtazangira kumwomba aache kumpiga mwanafunzi huyo, lakini aliendelea kumpiga jambo ambalo linaonyesha alikusudia kumuua.

Kesi hiyo imehairishwa hadi Septemba 17 kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kimahakama ili iweze kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa.

Sperius alifariki dunia Agosti 27, mwaka huu, muda mfupi baada ya kudaiwa kupigwa shuleni na mwalimu Mtazangira aliyekuwa mwalimu wa nidhamu katika shule hiyo kwa kutuhumiwa kuiba mkoba wa mwalimu Herieth Gerald.

Marehemu alizikwa Agosti 31, mwaka huu nyumbani kwa baba yake mzazi Kata ya Mubunda, Kijiji cha Kitoko wilayani Muleba.

 

 

 

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here