26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Walimu waibuka na madai mapya

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako.

NA NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM

CHAMA cha Walimu  Tanzania CWT) kimesema madai ya walimu yasiyokuwa ya mishahara ambayo hadi sasa bado hayajalipwa ni zaidi ya Sh bilioni 10.

Wiki iliyopita, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, wakati akizungumza katika kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa na Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC1), alieleza kuwa katika madai yasiyokuwa ya mishahara hakuna mtumishi ambaye hajalipwa.

Alisema madeni ya walimu yamegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni madai yanayotokana na mishahara na yasiyokuwa ya mishahara ambayo yamekuwa yakilipwa na Serikali kupitia wizara yake huku madai ya mishahara yakishughulikiwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluoch alisema walimu waliolipwa madai yasiyokuwa ya mishahara ni wachache na kwamba mengine bado yanaendelea kukusanywa.

“Hatuwezi kwenda namna hii, matamko kama haya, mawaziri wawe wanajiridhisha kwanza. Kama walimu waliosimamia mtihani wa kidato cha nne mwaka jana hadi leo hawajalipwa na waziri anajua yote haya,” alisema Oluoch.

Alisema walimu waliosimamia mtihani huo mwaka jana wanadai zaidi ya Sh bilioni nne.

Chama hicho kimepanga kukutana na timu iliyoundwa kushughulikia madeni ya walimu   kufanya tathmini kujua madeni yaliyolipwa na yale ambayo bado walimu wanadai.

Alisema mara ya mwisho walikutana Aprili 19, mwaka huu, ambako Serikali iliomba kupewa muda wa miezi minne na walipanga kukutana tena mwezi uliopita lakini hadi sasa hawajakutana.

“Tunasubiri ni lini tutakutana nao   watupe majibu kuhusu madeni ya walimu. Mwezi huu tuna kikao cha baraza na mojawapo kati ya taarifa tunayotakiwa kuiwasilisha ni hii ya madeni…kazi yetu ni kupeleka kwenye vikao vya chama ndivyo vitakavyotupa mwongozo,” alisema.

Wakati huohuo, CWT  kimesema wiki iliyopita kiliwasilisha  Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) madeni ya walimu 988 wa Mkoa wa Songwe ambayo ni karibu Sh bilioni moja.

Wilaya za mkoa huo na madeni ya walimu katika mabano ni Ileje (Sh milioni 400), Mbozi ( Sh milioni 400) na Momba (Sh milioni 140).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles