24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

WALIMU WAASWA KUWAHAMASISHA WANAFUNZI KUSOMA SAYANSI

Na SAMWEL MWANGA

WALIMU katika Wilaya ya Maswa   wametakiwa kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi hususan kipindi hiki ambacho taifa linaelekea kwenye uchumi wa viwanda   kuweza kupata wataalamu wa kutosha.

Pia waratibu elimu kata na walimu wakuu wametakiwa kusimamia kwa ukamilifu masuala yote ya taaluma katika shule za maeneo yao   kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Ofisa Elimu Msingi Wilaya ya Maswa, Simon Bujimu alikuwa akitangaza matokeo ya mtihani wa ujirani mwema wa darasa la saba wa wilaya za Maswa na   Kwimba.

Alisema  umefika wakati wa walimu wa   shule za msingi wilayani humo kuwa wabunifu na kuwahamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi.

Bujimu alisema masomo hayo  ni chachu ya maendeleo ya nchi hasa katika kuelekea Tanzania ya uchumi wa viwanda.

“Wakati umefika kwa walimu wa shule za msingi kuongeza ubunifu   tuweze kuwahamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi.

“Masomo haya ni chachu ya maendeleo   nchini hasa tunapoelekea katika Tanzania ya uchumi wa viwanda,”alisema.

Alisema   serikali inatambua  walimu ni injini ya elimu  kwa sababu bila wao elimu haiwezi kusonga mbele hivyo wanapaswa watumie nafasi zao    kuhakikisha  serikali inapata wataalamu waliobobea katika masomo ya sayansi kwa kuwajengea misingi bora.

“Hatuwezi kupata wataalamu wa kutosha viwandani kama hatutahamasisha masomo ya sayansi  shuleni…. itakuwa na utegemezi mkubwa kuwa na wataalamu kutoka nje ya nchi jambo ambalo si zuri,”alisema.

Alisema   shule 10 zilizofanya vizuri katika ufaulu wa jumla wilayani humo  zitapongezwa na nyingine 10    zilizofanya vibaya zitasaidiwa kuona ni wapi zimeshindwa ili nazo ziweze kufanya vizuri.

Bujimu alizitaja shule 10 zilizofanya vizuri katika wilaya hiyo kwa ufaulu wa jumla kuwa ni  shule za msingi Mwatumbe, Mwanhengele, Mwaliga, Mwandu, Mwabomba, Mwanganda, Shishiyu, Kadoto, Igwata na Mlimani.

Shule nyingine 10 zilizofanya vibaya kwa ufaulu wa jumla ni   Ngongwa, Nguliguli, Mwamitumai, Malita, Kiloleli, Bushitala, Mpindo, Ikungulyankoma, Mwamanenge B na Iwelimo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Maswa, Dk. Fredrick Sagamiko alisema mitihani hiyo ya ujirani mwema ni mpango wa Mkoa wa Simiyu wa kujipima kitaaluma kwa wanafunzi wanaotegemea kufanya mitihani yao ya mwisho na wao wanatekeleza kwa vitendo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles