30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

WAKULIMA WAELEZA UBORA WA MBEGU MPYA YA PAMBA

Na MWANDISHI WETU -MWANZA

WAKULIMA wa Mkoa wa Simiyu wamesema mbegu mpya ya pamba ya UKM 08 ambayo haina manyoya ni bora na kwamba inaongeza uzalishaji wao.

Kutokana na hilo, wameitaka Serikali kuisimamia kikamilifu kuhakikisha wakulima wote wanatumia.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, baadhi ya wakulima waliopanda mbegu hiyo katika msimu wa mwaka 2016/17, walisema mbegu hiyo ina ubora wa hali ya juu ikilinganishwa na mbegu ya manyoya ya UK91 ambayo imekuwa ikitumika kwa miaka 26.

Mbegu ya UK91 huzalisha wastani wa kilo 300 kwa ekari ikilinganishwa na mbegu mpya ya UKM08 iliyotolewa manyoya ambayo inazalisha mpaka kilo 1,200 kwa ekari.

Akielezea mafanikio aliyoyapata Christopher Nkhanda ambaye ni mkulima kutoka Meatu mkoani Simiyu, alisema mbegu ya UKM 08 ni bora na yenye mavuno mengi.

“Katika ekari 27 nilizolima niliweza kupata tani 17 za pamba ambazo ni wastani wa kilo 600 kwa ekari pamoja na kwamba hali ya hewa ilikuwa mbaya kutokana na ukame.

“Hapo awali mavuno yalikuwa hayazidi kilo 300 hata katika msimu ambao hali ya hewa ni nzuri na kuna mvua ya kutosha.

“Mwanzo niliziogopa sana mbegu hizi kutokana na kusikia maneno ya watu kuwa hazioti, hata wakati naanza kuzilima kwa majaribio mwaka juzi watu walinicheka lakini niliona zina mafanikio makubwa ndipo nilipoamua kuzilima kwa wingi na kufanikiwa kupata mavuno mara mbili ya yale ya siku zote,” alisema.

Alisema katika kutumia mbegu hizo amejifunza kuwa kutokana na ubora wake, haupaswi kupanda nyingi kama walivyokuwa wamezoea mbegu ya zamani aina ya UK 91.

Naye Matondo Kitinya ambaye naye ni mkulima, alisema alinunua kilo sita kwa ajili ya ekari moja kwa Sh 15,000 na kuzipanda kwa majaribio.

Alisema aliweza kuvuna kiasi cha kilo 700 na kupata kipato cha Sh 900,000 kutokana na mavuno hayo.

“Ekari moja niliyolima kwa msimu uliopita nilitumia kiasi cha Sh 180,000 kulima, kupanda, palizi hadi kuvuna na kufanikiwa kuvuna kiasi cha kilo 700 tofauti na kilo 200 ambazo nilikuwa nikipata awali wakati nikitumia mbegu ya UK 91,” alieleza.

Alisema mbegu ya zamani walikuwa wakipanda kiasi cha kilo 15 hadi 20 kwa ekari moja tofauti na hizo ambazo wanapanda kilo sita tu lakini zikiota ndani ya siku tatu japo alisema ili upate mafanikio yake ni lazima uzipande kwa kuzingatia vipimo na mstari kwa kuwa hazihitaji kubanana na mche mmoja hutoa vitumba 80 au zaidi.

Akizungumzia mbegu hizo, Meneja wa Kanda wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Jones Bwahana, alisema imekuwa na mafanikio makubwa kwa wakulima walioitumia na kwamba mkakati wa bodi ni kuhakikisha mpaka kufikia 2019 mbegu hiyo ya UKM08 inalimwa katika eneo lote la uzalishaji wa pamba hapa nchini.

Alisema tani zaidi ya 4,000 za mbegu ya UKM08 zilizotolewa manyoya zitasambazwa katika msimu huu wa 2017/18.

Alisema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika tangu mwaka 2010, ilitoa jukumu la uzalishaji mbegu bora aina ya UKM 08 kwa Kampuni ya Quton (T) Ltd ambazo zimekuwa zikithibitishwa na Taasisi ya Kupima Ubora wa Mbegu (TOSCI) kabla ya kusambazwa kwa wakulima.

Mkuu wa Kampuni ya Quton (T) Ltd, Pradyumansinh Chauhan, alisema mbegu hiyo imethibitika kuweza kuhimili magonjwa kutokana na kuandaliwa katika mfumo ambao unaua vijidudu vyote vinavyosababisha magonjwa.

Alisema kwa sasa wanazalisha tani 4,000 za mbegu wakati uwezo wao ni tani 10,000 kwa msimu na mbegu hizo kwa sasa zimeanza kulimwa katika maeneo ya wilaya ya Meatu, Bariadi mkoani Simiyu, Bunda Mkoa wa Mara na Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles