Kulwa Mzee, Dar es Salaam
Wakazi watatu wa jijini Dar es Salaam, waliokutwa na tausi watatu wenye thamani ya Sh 3,444,150 wanaodaiwa kuwa wa Ikulu, wamekiri makosa na kulipa fidia ambapo ndege hao wamerudi serikalini.
Uamuzi huo umefikiwa leo Jumatano Oktoba 30, saa tano asubuhi ikiwa ni siku tano tangu washtakiwa hao waende gerezani ambapo wamekiri baada ya kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salum Ally.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon aliwataja washtakiwa kuwa ni David Graha, Mohamed Hatibu na Mohamed Ally ambao wamefikia makubaliano, Oktoba 28 mwaka huu na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).
Amedai washtakiwa walikubaliana kuondolewa mashtaka yote na kubakia na shtaka moja la kujihusisha na biashara ya nyara za Serikali bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Inadaiwa kwa nyakati tofauti walikutwa na tausi watatu wenye thamani ya Sh 3,444,150. Katika makubaliano wamelipa fidia kwa hasara waliyosababisha ya Sh 6,890,000 na tausi wabakie kuwa mali ya Serikali huku adhabu nyingine kwa mujibu wa sheria zitatolewa na mahakama ndipo washtakiwa waachiwe huru.
Washtakiwa hao inadaiwa walitenda makosa hayo kati ya Julai mosi mwaka 2015 hadi Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam.