24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wakatoliki waandamana kupinga ufisadi DRC

Kinshasa, CONGO

WAKRISTO wa dhehebu Kikatoliki nchini  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wamefanya maandamano katika maeneo mbalimbali nchini humo kupinga ufisadi.

Maandamano hayo yaliitishwa na Kamati ya Katoliki ya Walei, ambao waliwataka raia wa DRC kwa ujumla kuingia mitaani kupinga ufisadi na ukosefu wa haki za kisheria.

Walei hao waliitisha maandamano hayo ya amani kutokana na kupotea kwa Dola za Marekani milioni 15 katika Benki ya Taifa ya DR Congo na kuwekwa katika benki ya biashara kabla ya kutoweka kabisa.

Pia walei wanaaminiwa kuwa ndio waliomshinikiza aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila kuacha azma yake ya kugombea muhula wa tatu madarakani.

Hii ni mara ya kwanza kwa Kamati ya Walei kuitisha maandamano chini ya utawala wa Rais Felix Tshisekedi.

Licha ya kilio cha umma ambao uliwataka wahusika wachukuliwe hatua, lakini si Rais Tshisekedi wala mahakama waliotoa maelezo ya kutosha kuhusu sakata hilo.

Awali Gavana wa Kinshasa, Gentiny Ngobila, na Kamati ya Uratibu ya Walei (CLC) walikubaliana kusitisha maandamano hayo mjini Kinshasa ili kuzuia, yasifanyike Oktoba 19 ambayo ni siku ilipofanyika Operesheni Kin Bopeto.

Hata hivyo, maandamano hayo yaliendelea katika maeneo mengine ya nchi kama ilivyopangwa.

Akizungumza na BBC, mmoja wa viongozi wa Wakatoliki hao, Isidore Ndaywele Nziem, alisema kuwa wanakerwa na ufisadi uliokithiri, ukiukaji wa sheria kwa kutowaadhibu wahalifu na kudorora kwa mfumo mzima wa sheria nchini DRC.

Si mara ya kwanza kwa Kanisa Katoliki kuitisha maandamano katika DRC kupinga kile ambacho linaona kuwa hakifai kwa jamii ya Wakongo.

Mwanzoni mwa mwaka jana, maaskofu wa kanisa hilo waliitisha maandamano dhidi ya Kabila, kumshinikiza aondoke madarakani na kutangaza kuwa hatawania urais Desemba mwaka jana. Maandamano hayo yalifanyika katika miji mbalimbali.

Mwishoni mwa mwaka juzi, kanisa hilo pia liliitisha maandamano yaliyosababisha vifo vya waandamanaji saba baada ya makabiliano kati yao na polisi.

Polisi wa kupambana na ghasia walikabiliana na waumini wa kanisa hilo waliokuwa wamemaliza ibada ya kuwaombea waumini waliouawa na kusababisha baadhi yao kujeruhiwa kwa hofu kuwa wangeandamana jijini Kinshasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles