WAKATALUNYA HAWANA MSIMAMO SANJARI  WA KUJITENGA

0
2

HAMKANI za siasa za Kimataifa na mikanganyiko yake huhitaji kutazamwa kwa jicho la Mwewe katika mwendelezo, hitimisho au kufifia katika kufuatiliwa licha ya vuguvugu kuendelea kama kinachotokea sasa katika Jimbo la Catalunya nchini Uhispania, ambapo mvutano baina ya jimbo hilo na mamlaka kuu ni mwendelezo wa mwiba unaochoma mguu ambao sasa unasababisha tende.

Mwezi mmoja  na nusu na ushei uliopita niliandika kwenye safu hii kuhusu jimbo hilo kutokana na shambulio la kigaidi lililofanywa La Ramblas na Cambrils Kusini-Magharibi mwa Barcelona, magaidi waliitumia Catalunya kushambulia mataifa mengi kwa vifo na majeruhi ya watalii kutoka Ireland, Uingereza, Ufaransa, Australia, Pakistan, Venezuela, Algeria, Peru, Ujerumani, Uholanzi, Ugiriki, Hong Kong, Taiwan, Ecuador, Marekani, Argentina, Romania, Cuba, Australia na Ufilipino kwani walifahamu fika hamkani ya mvutano baina yake na Serikali kuu ya Taifa hilo inawapa nafasi.

Catalunya iliyoko Kaskazini Mashariki kwenye Peninsula ya Iberia yenye mamlaka binafsi inayosimamia majimbo manne ya Barcelona, Girona, Lleida na Tarrago ambapo mji wake mkuu (Barcelona) ni wa pili kwa idadi ya watu nchini humo na wa saba kwa msongamano katika maeneo ya mijini yaliyomo ndani ya EU.

Katiba ya mwaka 1978 ya Hispania inatoa kiwango cha mamlaka ya uamuzi kwa maeneo 17 yanayojumuishwa kwenye Taifa hilo ambalo kimsingi si shirikisho, yanayoongozwa kwa mujibu wa sheria za asili za maeneo kwa mujibu wa muktadha sadifu wa wakazi japokuwa mifumo ya mabunge ya maeneo hayo unalingana.

Uasi wa Catalunya kutaka kuwa Taifa lenye mamlaka kamili ulizizima ilipoamua kupitisha Katiba tanzu inayotambua mamlaka zaidi ya yaliyoainishwa kwenye Katiba kuu, mvutano ukakolea na sasa moto wa figisu ya mkanganyiko umetiwa mafuta zaidi kutokana na matokeo ya kura ya maoni iliyofanyika Oktoba Mosi, asilimia 90 miongoni mwa asilimia 43 ya wapiga kura walioshiriki sawa na watu milioni 2.3 wanataka jimbo hilo lijitenge na kuwa nchi kamili.

Lakini kisichofahamika wazi kuhusu mzozo unaofukuta ni kwamba ndani ya jimbo lenyewe Wakatalunya wamegawanyika kwa mitazamo miongoni mwao, kuna wanaotaka mamlaka tanzu iongezwe wigo lakini si kujitenga wakihofia kutetereka kiuchumi lakini wengine wanataka kujitenga bila kujali athari hizo ili wapate nafasi ya kujiendesha kama Taifa kamili na kuwa na uamuzi usiobinywa na Serikali kuu. Wengi miongoni mwa Wakatalunya wenye umri mkubwa hawataki kujitenga wakidai kuwa pamoja na mengi yasiyoendeshwa sawa na Serikali kuu lakini bado wanaishi kidemokrasia kulinganisha na nyakati zilizopita.

Lakini asilimia kubwa ya vijana wanataka uhuru kamili wakipingana na wazee na kusababisha kuibuka kwa chuki miongoni mwao kutokana na asili kwa waliozaliwa Catalunya na walioanza kuishi hapo miaka mingi iliyopita wakitokea maeneo mengine ya Hispania. Ubaguzi unayatafuna makundi yote mawili yaliyokosa ithibati sadifu ya wanachotaka lakini Serikali kuu ya Hispania haikwepi lawama katika mkanganyiko unaofukuta, kutokana na kutoshughulikia kikamilifu changamoto nyingi za kihistoria ikijiaminisha kuwa Hispania ni Taifa moja lenye mfumo mzuri wa mgawanyo wa madaraka hivyo maoni tofauti ni batili.

Kinachosababisha vyama vyenye mrengo wa kujitenga jimboni Catalunya ni kudorora kwa uchumi unaoyumba tangu miaka saba iliyopita, jimbo hilo likiilaumu Serikali kuu kutoshughulikia suala hilo na kupigia debe hisia za kujitenga ambazo sasa zinaungwa mkono zaidi kuliko zilipoanza. Mkanganyiko huu umechagizwa na namna unavyoshughulikiwa badala ya Serikali kuu ya Waziri Mkuu Mariano Rajoy kuzungumza na     Serikali ya Catalunya chini ya Rais Carles Puigdemont, iliamua kutumia mabavu kuzima inachokiita uasi ikitishia kurudisha vurumai zilizorindima wakati wa utawala wa Dikteta Jenerali Fransisco Franco na kusababisha mzozo mzima kufukuta mashiko ya kihistoria inayoligawanya zaidi Taifa hilo.

Catalunya ikifanikiwa kujitenga hakuna shaka kuwa majimbo mengine yaliyosalia nayo yanaweza pia kuibuka na matakwa hayo lakini kinachoipa kiburi Catalunya ni taswira ya kitaifa hata ndani ya mamlaka tanzu ikiwa na Bunge, bendera yake, Rais, jeshi lake la polisi, sheria za utangazaji na balozi ndogo katika baadhi ya nchi duniani zinazosimamia ukuzaji wa biashara na uwekezaji kwenye jimbo hilo. Kulinganisha na majimbo mengine yenye mamlaka tanzu Catalunya yenye asilimia 16 ya watu wote wa Hispania pato lake la ujumla la ndani la asilimia 19 ni zaidi ya robo ya tija inayopatikana kwa kuuza ghafi za Hispania nzima nchi za nje.

Kati ya watalii milioni 75 wanaoitembelea Hispania milioni 18 huitembelea Catalunya na Bandari ya Barcelona ni miongoni mwa bandari kuu 20 zinazopitisha shehena nyingi ya Jumuiya ya Ulaya (EU). Theluthi moja ya Wakatalunya wote wanaofanya kazi wana weledi wa kitaaluma wa kazi wanazofanya, ingawa miongoni mwa vinyongo ni kwamba wanalipa kodi zaidi lakini mgawanyo wa kasma ya kodi ya ujumla kwa jimbo hilo hauwiani na mchango wao. Lakini ili kuwa Taifa kamili inabidi Catalunya ijisimamie kwa ulinzi wa mipaka, forodha, uhusiano wa kimataifa, benki kuu, mawasiliano ya anga na kodi ya ndani mambo ambayo bado yanasimamiwa na Serikali kuu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here