23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wahitimu Mkwawa waipongeza Serikali

FRANCIS  GODWIN, IRINGA

WAHITIMU wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa mkoani Iringa, wameipongeza Serikali  kwa  kuwadhamini masomo yao kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).

Akitoa pongezi kwa niaba ya  wenzake kupitia hotuba ya wahitimu  hao, Philemon Frugence ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Elimu katika Sayansi mwaka 2018/19, alisema pasipo udhamini wa mikopo ya Serikali, ingekuwa ni vigumu kwa  wengi wao kumaliza masomo yao.

Akisoma hotuba hiyo mbele ya Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais mstaafu Jakaya  Kikwete juzi wakati wa mahafali ya  11 ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu  Mkwawa Iringa, Frugence alisema  wengi wa wanafunzi waliohitimu ni watoto wanaotoka familia duni kiuchumi, hivyo udhamini huo  umewapatia haki watoto wote   kupata elimu ya juu.

Alisema pamoja na Serikali kutoa   mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, bado zipo changamoto mbalimbali ambazo wanaomba iendelee kuzitatua katika chuo hicho.

“Mkuu wa chuo safari yetu hapa  chuoni haikuwa fupi na tambarare  kama wengi walivyodhani, bali  ilikuwa ni ndefu yenye milima na mabonde.

“Miongoni mwa sababu   zilizosababisha safari yetu kuwa ndefu ni pamoja na upungufu wa vyumba vya hosteli. Changamoto ya malazi kwa wanafunzi itarudia kila mwaka katika hotuba za wanafunzi kutokana na umuhimu wake mkubwa,” alisema Frugence.

Alisema kukosekana kwa malazi ndani ya chuo kumewafanya wengi  wao kuendelea kuishi nje ya chuo na maisha ya nje ya chuo yamegubikwa na hofu ya kiusalama, hasa wakati wa usiku wanapotakiwa kwenda  kujisomea ndani ya chuo.

 “Tumekuwa tukihofu kuvamiwa na kuibiwa mali zetu, kelele za watu  tunaoishi nao mitaani ni nyingi,   kama walevi na muziki ambao ni vigumu kuuzuia kutokana na kuwa maeneo yasiyo rafiki ya kujisomea kwa utulivu huko mitaani, kwani wanaishi maeneo ya biashara za  wananchi,” alisema Frugence.

Alisema changamoto nyingine ni bei kubwa ya pango na unyanyasaji  unaofanywa na wamiliki wa nyumba  walizopanga wanafunzi mitaani nje ya  chuo.

Frugence alisema Serikali ili kusaidia   wanafunzi kuondokana na changamoto hizo, ni vema kujenga hosteli za kutosha ndani ya chuo ili waweze kuishi katika mazingira salama kielimu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa chuo hicho na Makamu Mkuu wa  UDSM, Profesa Wiliam Anangisye  alisema bodi ya usimamizi  inachukulia mahafali hayo kama matokeo ya jukumu lake la msingi la  usimamizi wa  chuo hicho.

Alisema  bodi imeendelea  kutekeleza majukumu yake ya kusimamia shughuli zote za chuo,  ambazo ni kutunga na kusimamia utekelezaji wa sera na mikakati  mbalimbali  ya  chuo kwa  miaka  mitano (2016/17 -2019/20) na sera mbalimbali zinazotungwa.

Kuhusu changamoto ya ukosefu wa malazi, alisema imeendelea kuwa kero kwa wanafunzi.

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu  cha Dar es Salaam, Jaji mstaafu Damian Lubuva aliipongeza Serikali kwa kudhamini idadi kubwa ya wahitimu kupitia HESLB.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles