Imechapishwa: Tue, Oct 3rd, 2017

WAHITIMU 177 WATUNUKIWA VYETI, GAVANA AWAASA KUZINGATIA MAADILI  

Na Joseph Lino


MAADILI inahusisha kanuni za maadili ambazo huwezesha mtu kuchagua kati ya haki na mabaya.

Kila taaluma huwa na maadili ambayo yanamuongoza mwanataaluma kufanya kazi kwa weledi na uadilifu. Miongoni mwa sekta zinazokabiliwa na changamoto katika utendaji wa  kazi ni sekta ya benki na taasisi za fedha nchini. Ukosefu wa maadili katika sekta hiyo umekuwa ukirudisha nyuma maendeleo ya huduma ya fedha nchini.

Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu, anasema maadili katika sekta ya benki na taasisi za fedha ni nguzo muhimu katika kuboresha sekta hiyo.

Ndulu anaelezea namna sekta ya kibenki imekuwa na changamoto za maadili kwa wafanyakazi wake.

“Benki zetu zimekuwa na changamoto za kimaadili katika utendaji, kuhudumia wateja na kutunza rasilimali zilizopo katika mabenki.

“Wateja wa mabenki hawawezi kuwa na imani na benki kama hakuna maadili yanayotumika vizuri, kama hawatoi huduma kwa ustadi na uadilifu au kutumia njia zinazomridhisha muweka fedha au mkopaji,” anasema Ndulu.

Gavana wa Benki Kuu aliwaeleza wahitimu wa mafunzo ya kibenki kutoka Taasisi  ya Mabenki Tanzania (TIOB) wiki iliyopita, kuwa kufanya kazi kwenye taasisi za fedha ni lazima mfanyakazi ajue viwango gani na maadili yakufuata.

“Mtihani wa mafunzo ya kibenki yanamhakikishia kila mwajiri wa benki kuwa huyu anayemwajiri si tu anajua kuhudumia, lakini pia amejifunza maadili ya kufanya kazi kwenye sekta hiyo,” anasema.

Ndulu anafafanua kama wao wasimamizi wa mabenki na taasisi za fedha wanahakikisha kila mfanyakazi hasa anapitia katika mafunzo hayo hasa wale wanaotaka kupanda vyeo.

Sekta ya kibenki imetoa ajira zaidi 15,000 nchini, ambapo wafanyakazi waliopita katika mafunzo hayo ni wachache mno ikilinganishwa na idadi ya wafanyakazi waliopo sasa.

Mkurugenzi Mtendaji wa TIOB, Patrick Mususa, anasema wafanyakazi 674 kati  ya 15,000 ndio waliopitia katika mafunzo ya kibenki kutoka benki 59 tangu ianzishwe  taasisi hiyo mwaka 1993.

Mususa anasema kuwa cheti cha taaluma ya kibenki ni nguzo muhimu katika kutekeleza wajibu na majukumu ya kazi zao, pia alitoa wito kwa mabenki kuona umuhimu wa vyeti vya mafunzo hayo kupatikana kwa wafanyakazi wote wa benki.

“Nguzo za vyeti hivi ni kutoa mafunzo ambayo ni nguzo ya kuendeleza, kujielimisha kila siku na kuboresha taaaluma ambayo ni nguzo ya uadilifu,” anasema Mususa.

Wiki iliyopita wahitimu 177 walitunukiwa vyeti vya mafunzo ya kibenki  ambapo wahitimu 17 walitunukiwa cheti cha Banking Certificate (Astashahada ya Benki) na 141 walikuwa wa ngazi ya juu ya taaluma (Certified Professional Bankers), huku 19 walipewa vyeti vya kubobea katika masomo maalumu (Banking Specialists).

Wahitimu hao wengi ni wafanyakazi katika taasisi za fedha nchini na wengine ni wale wanaojiandaa kuingia katika soko la ajira katika sekta hiyo.

TIOB ilianzishwa mwaka 1993 baada ya kuonekana umuhimu wa kuwa na chombo cha kitaifa cha kusimamia Taaluma ya kibenki hasa baada ya kufungua milango kwa taasisi za fedha za kimataifa kuwekeza Tanzania.

Lengo la kuanzisha taasisi hiyo ilikuwa kusimamia na kuendeleza taaluma ya kibenki ili taasisi za fedha nchini ziweze kupata wataalamu wenye elimu na ujuzi wa kuwawezesha kutoa huduma bora za kifedha kwa jamii kwa ujumla.

TIOB ilianzishwa ikiwa na wanachama waanzilishi 11 tu ambao ni taasisi za fedha zilizokuwepo nchini mwaka 1993, kwa sasa kuna jumla ya taasisi wanachama 59 na wanachama binafsi 7,000.

 

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

WAHITIMU 177 WATUNUKIWA VYETI, GAVANA AWAASA KUZINGATIA MAADILI