31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

WAGONJWA WA AKILI WAONGEZEKA MIREMBE

Na Ramadhani Hassan – Dodoma

IDADI ya wagonjwa wanaotibiwa kutokana na matumizi ya dawa za kulevya wameongezeka katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili ya Mirembe, iliyopo mkoani Dodoma.

Hospitali hiyo ipo ndani ya Taasisi ya Isanga ambayo imekuwa ikipokea watuhumiwa wa makosa ya jinai, wanaotenda makosa kutokana na kuwa na magonjwa ya akili.

Pia, hospitalini hapo kuna kituo maalumu cha kushughulikia wenye matatizo ya matumizi ya dawa za kulevya zikiwamo bangi, heroin na cocaine.

Chanzo chetu cha habari kilichopo hospitalini hapo, kiliiambia MTANZANIA jana kuwa tangu operesheni ya kupambana na dawa hizo ianzishwe jijini Dar es Salaam, idadi ya wagonjwa wanaopelekwa hospitalini hapo imeongezeka.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, kabla ya operesheni hiyo kuanza, walikuwa wakipokea wagonjwa watatu hadi wanne kila siku.

“Awali tulikuwa tukipokea idadi hiyo ya wagonjwa, lakini kwa sasa wameongezeka hadi kufikia 10 kwa siku.

“Wanaoletwa hapa wengi wao ni watumiaji wa dawa aina ya heroin ingawa watumiaji wa cocaine nao wapo japokuwa idadi yao ni wachache.

“Hadi sasa wagonjwa wa ndani ambao tumewalaza wapo kama 60 na wale wagonjwa wa nje ni kama watatu au wanne ambao tumewaruhusu,” kilisema chanzo hicho cha habari.

Wakati chanzo hicho kikisema hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Erasmus Mndeme, ambaye pia ni mtaalamu wa magonjwa ya akili, alisema hana taarifa za wagonjwa wa akili waliosababishwa na dawa za kulevya kuongezeka hospitalini hapo.

“Sina taarifa za kuongezeka kwa wagonjwa hao kwa sababu ripoti ya kama wameongezeka au wamepungua huwa tunaipokea kila mwisho wa mwezi.

“Kwa hiyo, naomba uvumilie hadi mwisho wa mwezi ndipo nitakapokupa takwimu sahihi,” alisema Dk. Mndeme.

Wakati hali ikiwa hivyo, katika Mtaa wa Hazina mkoani hapa ambako panadaiwa kuwa ndiko inakofanyika biashara hiyo, mmoja wa vijana wanaotumia dawa hizo ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema wauzaji wamebadilisha mbinu za uuzaji kwa kuwawauzia watumiaji wanaowafahamu.

“Sasa hivi pusha anakuangalia usoni, je anakufahamu au hakufahamu na asipokufahamu hakuuzii kwa sababu wanaogopa kukamatwa.

“Lakini jambo linalotuumiza ni kwamba bei imepanda maradufu. Hii bei inatuumiza kwa sababu mimi kupata stimu ni mpaka nitumie kete nne, yaani tunaumia sana,” alisema kijana huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles