31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wagonjwa ajali za moto wasaidiwa matibabu

Na HARRIETH MANDARI-GEITA


MGODI wa Dhahabu wa Geita (GGM) unatarajia kutumia Sh milioni 40 kwa ajili ya kuwagharamia upasuaji wagonjwa 40 walioathirika na ajali za moto.

Akizungumza mjini hapa juzi kabla ya kuwasafirisha kwenda Hospitali ya Sekou Toure ya Mwanza, wagonjwa hao wakiwamo watoto, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa GGM, Brad Cato, alisema kwa miaka 17 sasa wakishirikiana na wataalamu wa afya kutoka Australia wa Shirika la Rafiki Surgical Mission wamekua wakitoa tiba hiyo bila malipo.

“Kwa muda mrefu sasa tunayo furaha kuwa sehemu ya wadau tunaosaidia kupambana na changamoto zinazokumba sekta mbalimbali mkoani humu,” alisema.

Brad alisema katika kipindi chote hicho GGM imeshasaidia wagonjwa zaidi ya 1,642 wakiwamo watoto na watu wazima na katika awamu ya mwisho ya matibabu, wagonjwa 21 walifanyiwa upasuaji na kupona kabisa baada ya kusafirishwa Mei, mwaka huu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, Josephat Maganga, alisema Serikali inashirikiana na GGM kupitia mfuko maalumu wa huduma za kijamii (CSR) katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa nia ya kutatua changamoto zinazokumba jamii.

“Kupitia fedha za CSR, changamoto mbalimbali zimeweza kutatuliwa zikiwemo ujenzi wa zahanati, barabara na pia tiba za wagonjwa,” alisema.

Pia alisema tiba ya upasuaji ina gharama kubwa ambayo ni zaidi ya Sh milioni moja hivyo msaada huo umeokoa maisha ya wananchi wengi ambao kama wasingetibiwa wangeteseka na maumivu.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa GGM, Dk. Kiva Mvungi, alisema kwa miaka iliyopita GGM imekuwa ikisaidia watoto na watu wazima wenye midomo sungura lakini kutokana na idadi yao kupungua kila mwaka ndipo walipoanzisha huduma ya kuwasaidia walioathirika na makovu ya kuungua na moto.

“Kampuni yetu kwa kushirikiana na Serikali tumekuwa tukisaidia wagonjwa kila mwaka na awamu hii ni wale walioathirika na kuunguzwa na moto kutokana na idadi ya waathirika wa midomo sungura kupungua,” alisema.

Pia alisema tatizo la mdomo sungura hutokea pale mama mjamzito anapokosa madini na virutubisho mbalimbali mwilini ikiwamo ukosefu wa madini ya folic acid.

Mmoja wa wanufaika wa tiba hiyo, Margareth Damian, alisema amekuwa akiishi maisha ya kunyanyapaliwa katika jamii anayoishi huku wakimbatiza majina mengi ya kumbeza.

Alisema alipata makovu hayo mwaka 2014 baada ya kulipukiwa na jiko la mafuta ya taa akiwa Shule ya Sekondari Bariadi.

“Nimekuwa nikiishi maisha ya huzuni kwa sababu pale ninapoishi nimeshabatizwa majina mengi yakiwemo sura mbili, nashukuru sana kwa msaada huu nina imani majina hayo yatakoma,” alisema huku akitokwa na machozi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles