30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

WAGONJWA 110 WA UKIMWI  WATOWEKA MUHIMBILI

 

 

NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM


Watu 110 wanaoishi na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) waliokuwa wameanza kutumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo (ARVs) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wametoweka.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalum, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Maambukizi MNH, Amina Mgunya alisema asilimia tano kati yao ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 16 hadi 24.

Alisema tangu 2004 hadi sasa wagonjwa 10,047 wamehudumiwa katika kliniki hiyo.

Alisema kati yao wanawake ni  6,282 na wanaume ni 3,765 na kwamba wagonjwa 346 wamefariki dunia na 4,971 wamehama (wamehakikishwa) kituo.

“Muhimbili ni hospitali kubwa inayopokea wagonjwa wa rufaa kutoka katika maeneo mbalimbali nchini, mtu anapopewa rufaa kuja huku na kulazwa, tukimpima  na kukutwa ana maambukizi, tunamuanzishia dawa papo hapo, hii ni kulingana na mwongozo wa sasa wa serikali.

“Huwa tunawapa kadi maalum (blue card) ambayo huwa na namba maalum ya usajili wake, kadi hiyo huhitumia kupata huduma ikiwamo dawa za ARVs kliniki.

“Ikiwa ataruhusiwa kurejea nyumbani, ataendelea kupata huduma kwenye hospitali yoyote kwa kutumia kadi hiyo hata kama ni nje ya mkoa.

“Lakini ili kuwaondolea adha ya kuja Muhimbili mara kwa mara wagonjwa 4,971 wamehamishwa vituo vya karibu na maeneo yao,” alisema.

Dk. Amina alisema wamebaini sababu nyingi zinazochangia hali hiyo kutokea ikiwamo kujinyanyapaa wenyewe.

“Kuna ambao wamedai kuwa wameokoka hivyo wanaendelea na maombezi kwamba wanaamini Mwenyezi Mungu atawaponya.

“Kuna wengine wameacha kutokana na imani potofu, wamekimbilia kwa waganga wa kienyeji wakiamini huko wakitibiwa watapona,” alisema.

Alisema wapo pia ambao wameacha kuhudhuria kliniki hiyo hospitalini hapo kwa kuhofia wenza wao.

“Wanahofia kwamba itakuwaje siku watakapogundua kuwa wanahudhuria kliniki hiyo na wanatumia dawa hizo. Kuna hofu ya kunyanyapaliwa, huwa wanapatiwa kadi maalum ya kuchukua dawa hizo, hapa hospitalini huwa wanachukua dawa katika dirisha moja na wagonjwa wengine,”  alisema.

Habari hii imeandaliwa na Veronica Romwald, Salma Omary (TUDARCO) na Halima Ally (TUDARCO)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles