31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

WAGOMBEA UBUNGE KINONDONI WANAVYOLILIA KAMPENI ZA KISTAARABU

Na, SHADRACK SAGATI


KIPENGA kimepigwa! Kampeni katika Uchaguzi Mdogo katika Jimbo la Kinondoni zimeanza mara tu baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanya uteuzi wa wagombea kutoka vyama 12.

Huu utakuwa ni mtifuano wa siku 27 za kampeni ambazo wagombea hao kwa kushirikiana na wafuasi na viongozi wa vyama vyao vya  siasa watajinadi kwa wapiga kura wa jimbo hilo ili mmojawapo aweze kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Kinondoni jimbo lenye kata 10 za Hananasif, Kigogo, Kijitonyama, Kinondoni, Magomeni, Makumbusho, Mwananyamala, Mzimuni, Ndugumbi na Tandale lina idadi ya wapiga kura 264,117 ambao watapigia kura katika vituo 611.

Wakati walipokuwa wanarejesha fomu, wagombea  wote waliishukuru NEC kuwateua kugombea ubunge kwenye uchaguzi huo mdogo na wote waliahidi kufanya kampeni za kistaarabu kwa mujibu wa sheria.

Johnson Mwangosi wa chama cha SAU alisema “Nimefurahi kuteuliwa kugombea ubunge wa kinondoni, ni mara ya pili kugombea ubunge katika jimbo na nayajua machungu yake. Kwa kambi ya upinzani naomba tusiwe na masihara, lazima tushikamane ili tuweze kupambana na CCM.”

Wakili wa Kujitegemea, Mohamed Majaliwa anayegombea kwa tiketi ya NRA, alisema chama chake kina maana ya ujenzi wa kijamii, aliwahakikishia wakazi wa Kinondoni watarajie siasa ya kisayansi, siasa inayolenga kwenye maendeleo kuanzia mtu binafsi, jimboni hadi Taifa.

Aliwataka wapiga kura wa Jimbo la Kinondoni wasihadaike na udogo wa chama chake. Alisema chama chake ni kikongwe kama vilivyo vyama vikubwa, ila kilirudishwa nyuma kutokana na misukukosuko ya kisiasa, lakini sasa chama kimerudi na wategemee huduma nzuri na aliwaahidi kuwaletea maendeleo wananchi wa Jimbo hilo la Kinondoni.

Ali Omari Abdallah wa TADEA, alisema amesukumwa kugombea ubunge katika jimbo hilo kwa kuwa kuna mahitaji mengi yanayohitaji fikra mpya katika kuijenga Kinondoni. Anaomba uchaguzi uwe salama na wa heri na usiwe wa upendeleo wala uonevu kwa chama chochote.

David Majejele wa Chama cha Kijamii (CCK) aliomba kuwa mwakilishi wa Jimbo la Kinondoni ili kuwa mtetezi wao wa haki mbalimbali zinazohitajika kwa wananchi. Alitoa mwito kwas wananchi wampatie kura za ndio ili aweze kuwa mwakilishi wao

Aliomba vyama vingine washikamane kumaliza ngwe ya uchaguzi huo kwa amani, wafanye kampeni za ustaarabu, amani na upendo na wananchi wataamua ni yupi wanamhitaji awe mwakilishi wao.

“Hii ni mara ya pili kugombea ubunge katika jimbo hili, safari hii naomba wanipatie mimi niwe mwakilishi wao,”alisema Majejele na kuongeza kuwa anaamini  uchaguzi huo utamalizika kwa amani na salama.

“Ombi langu kwa wenzangu kampeni zetu ziwe za amani na ustaarabu na siku ya kupiga kura tukapige kura kwa amani,”alisema.

Mwajuma Milambo mgombea wa (UMD) yeye aliomba wagombea wote wafanye kampeni vizuri za kistaarabu ili wana Kinondoni ikifika siku ya kupiga kura watumie haki ya msingi.

Nawaomba wananchi wa Jimbo la Kinondoni wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura ili wamchague kiongozi wanayemtaka, kwani wasipojitokeza wao hatima ya Kinondoni iko mikononi mwao ya kuamua nani awe mwakilishi wao,”alisema mgombea huyo.

Mwajuma pia alikishukuru chama chake kwa kumteua kuwa mgombea wa UMD na aliishukuru Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kumteua kuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kinondoni.

Mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Salum Mwalimu ambaye chama chake kilisusia uchaguzi katika jmbo la Songea Mjini, Singida Kaskazini na Longido alisema wameamua kusimamisha mgombea katika jimbo hilo kwa kuwa wameona wananchi ndio wanaojua hatima ya jimbo lao.

“Nawashukuru wanachama wenzangu kunisindikiza, huu ni mwanzo muhimu wa kuanza safari ya kugombea ubunge katika Jimbo la Kinondoni.  Fomu imepokelewa vizuri na haina makosa ni imani yangu kwamba hawajaona kosa na mimi ni mgombea ambaye sina doa.

“Naahidi kuwa naenda kufanya kampeni zitakazoleta umoja bila kujali tofauti za vipato, imani na itikadi za vyama. Naenda kuwaunganisha watu wa Kinondoni ili tuweze kupigania haki, demokrasia na maslahi ya Kinondoni,”alisema Mwalimu.

Mgombea wa TLP, Godfrey Malisa  yeye pia alishukuru kupata fursa hiyo ya Kinondoni na akawaomba wakazi wa jimbo hilo  wajitokeze kwa wingi kwenda kwenye kampeni zake wakamsikilize namna anavyonadi sera zenye faida kwa jimbo hilo.

“Nawaomba wasisue uchaguzi huu, wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura kwani hatima ya maendeleo ya jimbo hili iko mikononi mwao,”alisema Malisa.

John Mboya mgombea wa Chama cha Demokrasia Makini  yeye alisema “Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuteuliwa kugombea ubunge, naomba Mungu nikashindane niweze kushinda.”

Maulid Mtulia wa CCM alikishukuru chama chake kumwamini kwa kumteua na pia anawashukuru wana CCM wenzake kupokea vizuri uamuzi wa Kamati Kuu kwa kumteua yeye.

Alisema wataanza kampeni za kistaarabu kama ilivyo kawaida ya chama chake na akaomba vyama vingine vitakapopata fursa ya kusimamisha wagombea wafanye kampeni ya kistaarabu.

“Kwa kuwa Kinondoni ndio Dar es Salaam na Dar es Salaam ndio Tanzania, bila shaka Kinondoni ndio Tanzania, lazima tuwafundishe maeneo mengine kampeni za kistaarabu zinatakavyofanywa na tutafanya kampeni za kistaarabu hadi mwisho wa kampeni,”alisema Mtulia.

Rajab Juma  anagombea ubunge kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) yeye aliporejesha fomu alianza kuilaumu Chadema kusimamisha mgombea ubunge katika jimbo hilo kwa madai kuwa hatua hiyo itapunguza nguvu ya upinzani.

“Hili ni jimbo ni la CUF, lakini Chadema imempitisha mgombea hatua hii ni  kupoteza nguvu za upinzani, tulipata jimbo hili kwa ushirikiano wa vyama sio  ushirikiano wa mtu mmoja mmoja, chama tulichoshirikiana kipo, iweje walete mgombea? Alihoji Juma.

Msimamizi wa Uchaguzi katika Jimbo la Kinondoni, Aron Kaigamjuli alisema shughuli za uchaguzi imeanza. ilianzia kwa wagombea kuchukua fomu na vyama 12 vilishiriki na vyama hivyo ndivyo ambavyo vimerejesha fomu.

“Sisi Kinondoni tumejiandaa kuhakikisha uchaguzi unakwenda vizuri na kutakuwa na usalama wa kutosha, tutaendelea kuvihusisha vyama wakati wa kampeni kuhakikisha kusiwepo vurugu wakati huo na mgombea atakayechaguliwa na wananchi tutamtangaza kuwa mbunge,”alisema.

Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Kinondoni utakwenda sambana na Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Siha na unafanyika baada ya waliokuwa wabunge wa majimbo hayo kujiuzulu nyadhifa zao na kujiunga na chama cha kingine cha siasa.

Mwandishi wa Makala haya ni Afisa Habari Mwandamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na anapatikana kwa namba 0788 014 648

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles