26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyakazi wa saluni, wateja wao hatarini zaidi kwa corona

AVELINE KITOMARY 

SERIKALI  kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imetoa wito kwa wafanyakazi wa saluni kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19) kutokana na kundi hilo kuwa katika hatari kubwa ya maambukizi. 

Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Kitengo cha Maji na Usafi wa Mazingira, Wizara ya Afya, Anyitike Mwakitalima, wakati akitoa elimu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga na virusi hivyo.

Mwakitilima alisema licha ya kundi hilo kuwa katika hatari, pia lina uwezo wa kuwaambukiza watu wengine wakiwamo wateja wao.

“Kwa wale ambao wanasafisha nywele, kucha, wanafanya ‘massage’, wanaosuka nywele, mchukue tahadhari kwa sababu mpo katika hatari kubwa sana ya kuambukizwa, lakini vile vile kuambukiza watu wengine maambukizi ya virusi vya corona,” alisema Mwakitalima.

Alisema Serikali inaendelea kuwakumbusha wafanyakazi wote katika maeneo ya saluni kuhakikisha wanaepuka msongamano pindi wanapokuwa katika majukumu yao, huku akisisitiza ni muhimu kwa kinyozi kuvaa barakoa pindi anaponyoa.

“Tunawakumbusha, tena kwa upendo kabisa, tunawakumbusha muepuke msongamano, ndani awepo mtu anayenyoa na anayenyolewa, na yule ambaye ananyoa ahakikishe muda wote amevaa barakoa, tunawaambia hivi kwa sababu tunawapenda,” alisema Mwakitalima.

Kwa upande wake, Sfaff sergeant (S/Sgt) Valentine Ngowi, aliwataka madereva wote wa vyombo vya moto, hususan bodaboda na bajaj kuhakikisha wanavitakasa vyombo vyao vya usafiri kwa sabuni mara kwa mara ili kuua maambukizi ya virusi vya corona endapo vitakuwepo.

“Kwa madereva hasa  wa bodaboda na bajaj wahakikishe wanajikinga kwa kutakasa vyombo vyao kwa maji na sabuni mara kwa mara ili kujiweka salama zaidi dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona,” alileza Ngowi.

Naye balozi wa kampeni ya Mikono safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) amesisitiza kuwa ili kupambana na corona, watu wasichoke kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka ili kuepuka kupata maambukizi.

Uhamasishaji huu unaofanywa kupitia kampeni hii ya “Mikono safi, Tanzania salama” inayoratibiwa na Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Project CLEAR kwa kushirikiana na Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) kutoka Mjomba Theatre Gallery unaendelea katika Jiji la Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles