31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyabiashara waipongeza TRA kwa kutoa elimu ya kodi

MWANDISHI WETU- MBEYA

Wafanyabiashara katika mpaka wa Kasumulu unaotenganisha nchi za Tanzania na Malawi uliopo Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya wameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kutoa elimu ya Kodi ambayo inawaongezea uelewa wa masuala ya Kodi na ari ya kuilipa kwa hiari.

Hayo yameyasemwa na wafanyabiashara wa mpaka wa Kasumulu mara baada ya kutembelewa katika b8ashara zao na kupewa elimu ya ulipaji kodi na maofisa wa TRA wanaofanya kampeni maalumu ya elimu ya Kodi  ya mkoa kwa mkoa inayoendelea mkoani Mbeya.

Mmoja wa wafanyabiashara hao Ramadhani Msangi amesema amefurahi kutembelewa na kupewa elimu ya Kodi na kwamba imemuwezesha kupata taarifa sahihi za ulipaji kodi ambazo alizokuwa nazo hapo awali hazikuwa taarifa sahihi.

“Kwa kweli mimi leo nimepata taarifa sahihi za ulipaji kodi kwa awamu nne kwa mwaka kwani hapo awali taarifa zilizokuwa nazo ni kwamba natakiwa kulipa Kodi yote kwa mara moja, Nawapongeza sana TRA kuja huku kwetu kutuletea elimu na taarifa sahihi za ulipaji kodi, elimu hii iwe endelevui,” amesema Msangi

Naye Rose Nelson ambaye ni mmiliki wa duka la bidhaa za jumla mpakani Kasumulu  ameishukuru TRA kwa kuanzisha kampeni ya elimu kwa Mlipakodi na kuongeza kuwa itawasaidia wafanyabiashara wa mipakani ambao wamekuwa na uelewa mdogo wa masuala ya ulipaji kodi na kwamba ingekuwa rahisi kwa wao kupotoshwa kwa kupewa taarifa zisizo sahihi na watu wa mtaani.

“Kwa kweli ujio wa TRA hapa mpakani ni jambo jema sana na hii elimu ya Kodi wanayotupatia sisi wafanyabiashara inatupa uelewa ambao sasa hatutakuwa na visingizio vya kutokulipa Kodi ya serikali,” amesema Rose.

Anaongeza kuwa TRA inatakiwa kupeleka Elimu hiyo ya Kodi  nchi nzima ili kila mfanyabiashara na wananchi waelewe umuhimu wa kulipa Kodi kwa maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake mfanyabiashara Justone Luvanda amewashauri wafanyabiashara wenzake kuwaona maofisa wa TRA kama marafiki kutokana na kuwa wanakusanya mapato ambayo yanaisaidia serikali kutekeleza majukumu yake kwa wananchi kama kujenga barabara, kununua dawa za hospitali na vifaa tiba.

“Mimi nitoe tu wito kwa wafanyabiashara wenzangu hapa mpakani na sehemu nyingine kuwa tuwape ushirikiano maofisa wa TRA kwa kuwa wanakusanya mapato ya serikali ambayo yanatuwezesha kupata huduma za kijamii na kuboresha miundo mbinu mbalimbali inayochochea maendeleo”, amesema Luvanda.

TRA inaendesha kampeni maalumu ya kutoa elimu kwa Mlipakodi mkoa kwa mkoa na sasa ipo mkoani Mbeya na Wilaya zake kuhakikisha elimu ya Kodi inawafikia wafanyabiashara na wananchi wote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles