27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wadhamini wa Lissu wataka akamatwe

Na KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

WADHAMINI wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, wamedai kwa nguvu zao wameshindwa kumfikisha mahakamani, hivyo wamewasilisha maombi wakitaka akamatwe.

Wadhamini hao, Robert Katula na Ibrahim Ahmed, waliwasilisha maombi yao jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

“Sisi tumeshindwa kwa nguvu zetu kumleta mahakamani Lissu, tumeleta maombi ili mahakama itoe amri ya kukamatwa,” alidai Katula.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai kesi ilikuja kwa kutajwa amri za mahakama kwa Lissu kama zinavyojieleza, na kwamba wadhamini wanaweza kuelezea.

“Tumepewa nakala ya maombi ya wadhamini wakitaka mahakama itoe amri ya kumkamata Lissu, tunatambua maombi yamepangwa kesho (leo) tutawasilisha hoja zetu,” alidai Wankyo.

Hakimu Simba alisema kesi hiyo ya uchochezi itatajwa leo kuangalia masuala ya kisheria kuhusiana na maombi hayo.

Awali wadhamini hao walimwomba Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe awasaidie kumrudisha mshtakiwa huyo nchini ili afike mahakamani.

Tangu Desemba mwaka jana mahakama hiyo imekuwa ikiwataka wadhamini wamfikishe mshtakiwa huyo mahakamani ili kesi iendelee.

Mbali na Lissu, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Lissu, Mkina, Jabir na Mehbooh wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 katika Jiji la Dar es Salaam, washtakiwa watatu; Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 katika Jiji la Dar es Salaam, walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13, 2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Alidai mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Mbali na mashtaka hayo washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016, Dar es Salaam, bila ya kuwa na mamlaka yoyote, waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles