26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

WADAU JITOKEZENI KUIUNGA MKONO CHABATA


Na JENNIFER ULLEMBO-DAR ES SALAAM

BAISKELI ni moja ya michezo inayopendwa duniani kwa asilimia kubwa, kwani mbali na kuwapa watu fedha kwa kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali, pia umekuwa ukiwasaidia kuimarisha na kutunza afya.
Chama cha Baiskeli Tanzania (Chabata), kilianza mikakati ya kuandaa mashindano ya Taifa miezi mitano iliyopita.
Viongozi wa chama hicho, walikuwa wakitegemea kupata wadhamini na wadau watakaoongeza nguvu, ili kufanikisha mashindano hayo.
Licha ya Tanzania kutofanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya mchezo huo, bado waendesha baiskeli na viongozi wa Chabata, wameendelea kujipa moyo wa kuhakikisha mchezo huo unasonga mbele na kwa kusaka fedha za kufanikisha mashindano hayo.
Lakini hivi sasa upepo umeonesha kubadilika, chama hicho hakina fedha za kufanikisha mashindano na wadhamini hawajajitokeza.
Awali walijitokeza wadhamini wachache, ambao mwisho waliamua kujitoa, huku wengine wakitoa kigezo cha ugumu wa hali ya kiuchumi kwa sasa.
Michezo kama baiskeli na mingineyo midogo ikishindwa kupewa uzito mkubwa kama ilivyo kwa soka, jambo linalofuata ni vyama vyake kushindwa kupiga hatua.
Inaonyesha wazi nguvu za ziada zinahitajika kuiwezesha Chabata kufanikisha malengo iliyojiwekea kwa mwaka huu.
Umoja na nguvu baina ya viongozi wa chama hicho pekee, haiwezi kuwa njia ya kuusaidia mchezo wa baiskeli na kufanikisha mashindano hayo.
Bado wadau na wapenzi wa michezo nchini, wameendelea kuweka uzito kusaidia mchezo huu kusonga mbele.
Nchi yetu imebarikiwa kuwa na vipaji, lakini kama watakosa misingi na msimamo imara wa kuendeleza kile walichonacho, daima tutaendelea kuwa wasindikizaji katika mashindano kwa kushuhudia mataifa mengine yakibeba medali na kuweka rekodi bora zaidi.
Hivi sasa uongozi wa chama hicho, umeonyesha wazi kupoteza matumaini ya kufanikisha mashindano hayo kwa mwaka huu. Ingawa Mwenyekiti wake, George Mhagama, ameendelea kujipa moyo wa kuhakikisha wanayafanikisha kwa njia yoyote.
Wadau wa michezo ungeni mkono jitihada hizi za Chabata kwa ajili ya kuitangaza nchi kupita mchezo huu, ambao katika mataifa mengine umekuwa ukipewa kipaumbele na thamani kubwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles