WABUNGE CCM WACHARUKA MPANGO WA SERIKALI

0
39

Na ESTHER MBUSSI-DODOMA


WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameukosoa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2018/19, huku wakimshambulia Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kuwa ni kiongozi asiyekuwa na ushirikiano na kamati za Bunge.

Wamesema kuwa Dk. Mpango hasikilizi hata ushauri wa mambo mbalimbali unaotolewa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti.

Wakichangia mjadala wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2018/19, baadhi ya wabunge hao, walidai Dk. Mpango amekuwa akitoa takwimu zinazokinzana na pia hasikilizi ushauri wao na kushauri kamati hiyo ivunjwe kwa sababu haina utekelezaji.

Aliyekuwa wa kwanza kuchangia mpango huo, alikuwa Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa,  ambaye alisema kuwa waziri huyo ana kiburi ambacho hakilisaidii Bunge wala Serikali.

“Bahati nzuri wabunge wa CCM wanakuheshimu sana, lakini una kakiburi fulani hivi ambako kwanza hakaisaidii Bunge, pili huisaidii Serikali kwa sababu mimi naweza nikaja na hoja ya msingi ya kuisaidia Serikali, na nimeshakuja kwako mara nyingi kukwambia hapa kuna mwanya tunaweza tukapata fedha, lakini namna ya kukupata utafikiri unataka kumpata nani sijui.

“Sina uhakika hata simu za wabunge kama huwa unapokea, sisi ni wabunge wenzako, wote humu ndani tunataka tukusaidie kwa sababu wewe ndio umekamata mfuko wa fedha, sasa huwezi kwenda kutafuta fedha peke yako, sisi ndio wasaidizi wa kukusaidia.

“Mipango ambayo tunakushauri, basi angalau ungekuwa unapokea kama si asilimia 75, basi asilimia 50, basi hata 25. Nikuombe Dk. Mpango wa mpango, jitahidi kusikiliza ushauri wa Kamati ya Bajeti kwa sababu mnafikia pahala mnakaa kwenye bajeti mnaishauri Serikali, lakini hakuna kinachochukuliwa kama kamati hii haipo, maana yote tunayoshauri yakichukuliwa labda ni mawili au matatu.

“Wenzako wote wanasikia, isipokuwa Dk. Mpango wa mpango husikii na ukiona Seneta anazungumza ameshasikia mengi huko nje, Dk. Mpango wewe si msikivu,” alisema Ndassa.

 

BASHE

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, alisema hakuna jambo muhimu duniani katika kupanga mipango kama takwimu na kwamba uchumi wowote duniani una kioo.

Alisema kioo cha uchumi wowote unaokua au kusinyaa moja ni taasisi za fedha, biashara na soko la hisa.

“Mzunguko wa fedha umepungua kutoka shilingi bilioni 222 hadi 12, waziri anasema wamepunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima, huwezi kuondoa umasikini nchi hii bila kuwekeza kwenye kilimo.

“Hatuwezi kuondoka kwenye umasikini kama hatuwekezi kwenye kilimo, huwezi kuleta mapinduzi ya viwanda bila kuwekeza kwenye kilimo, mkulima wa nchi hii ndiyo kageuka ‘punching box’, tunadhibiti mfumuko wa bei ya chakula kwa kumtia umasikini mkulima, aina gani ya uchumi hii.

“Wabunge wenzangu, tumepewa dhamana na wananchi, tusiharibu nafasi ya Rais kuchaguliwa mwaka 2020 kwa sababu ya Waziri Mpango. Waziri wa Fedha asipowajibika hatutatoka hapa,” alisema Bashe.

 

SERUKAMBA

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba, alisema Waziri Mpango kutoa takwimu zinazokinzana katika Deni la Taifa. Kwamba mwaka huu alisema deni la Taifa limekuwa Dola za Marekani bilioni 18, mwaka uliopita ilikuwa 19, sawa na ongezeko la asilimia 9.76.

“Mwaka unaofuata tunaambiwa ni 18, lakini kuna ongezeko hili wanalinganisha na Dola bilioni 16 kipindi cha 2015. Kwenye mpango huu wa mwanzo wanasema Oktoba ilikuwa 19, wa pili Oktoba ilikuwa bilioni 16 na kwenye mpango huu mpya wanasema limefika Dola bilioni 26 ukilinganisha na Dola 22 za mwaka 2016 Juni, lakini kwenye ripoti ya Juni tunaambiwa dola 19.

“Kwa hiyo moja ya tatizo tulilonalo hapa ni takwimu hizi zinazoletwa na Wizara ya Fedha, takwimu ni za kwao. Haiwezekani tukawa na tofauti ya dola bilioni tatu.

“Ukiangalia mipango yote mitatu ni ‘copy and paste’, yaani ni kile kile hapa tunapanga, lakini ni kwa sababu ni Katiba, lakini wanachokwenda kufanya wao wanajua Bunge lako halijui,” alisema Serukamba.

Alisema deni la taifa sasa hivi linakua kwa Sh trilioni nne kwa mwaka kulingana na takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Aidha, alisema Serikali katika mpango huu imekuwa haina imani katika sekta binafsi, na alimtaka waziri aliambie Bunge ni kwanini katika kitabu chake hakuna mahali amezungumzia sekta binafsi.

“Kama tumerudi kwenye ujamaa tuambiane wote tujue, lakini haiwezekani tunaimba ujamaa halafu tunataka matokeo ya kibepari, haiwezekani, hakuna katikati.

“Mpango hauongelei kukuza tija, angalia kwenye kilimo hakuna anayeongelea kukuza tija, maana nilitarajia wangesema mwaka huu tumezalisha tani fulani za mahindi, mwaka ujao tutavuna, pamba hakuna, kahawa, tumbaku hakuna korosho

“Sasa tunapanga nini? Ni kweli tunapanga, lakini mwisho wa siku yale yale, huku kwenye mipango yote wanasema wataweka fedha Benki ya Rasilimali (TIB), kwa ajili ya miradi ya maendeleo, toka wameanza kusema hawajaweka hata senti tano TIB.

“Sasa mimi naomba mambo ambayo mnaona hamuwezi kufanya msiyaandike, labda mniambie Bunge lako halisomi nyaraka hizi. Sisi hatuongelei uzalishaji, tunaongelea kubana, kubana tu, mmegeuza ni uchumi wa kubana tu hadi wameleta sheria hapa ya kubana, hakuna anayeongelea kupanua.

“Tunamdanganya nani hapa, mimi namwonea huruma sana Rais, anahangaika wenzake hawambwambii ukweli, mtanisamehe… leo Rais anakwenda kuwaambia viwanda ndiyo vizalishe sukari, lakini tumesema hapa siku zote hakuna aliyetuelewa katika hili Bunge, lakini Rais amesema viwanda vitazalisha sasa.

“Lakini wabunge nenda kwenye kumbukumbu tumesema waongezeeni maeneo walime, Ilovo waliomba maeneo wakanyimwa, leo wameenda Zambia, ni namba mbili kwa sukari Afrika,” alisema Serukamba.

 

SUGU

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Chadema),  alisema Serikali inapozungumzia mpango wa kubana matumizi, haimaanishi kwa sababu katika mpango huu viongozi kadhaa wameongezeka.

“Ukiangalia mawaziri na makatibu wakuu wameongezeka na viongozi wa kawaida wana ulinzi wa kupita kiasi.

“Naibu Spika ana wasaidizi wawili ambapo akisafiri wanalipiwa ndege ‘business class’, zile ni fedha. Mimi nakumbuka wakati ule ukiwa Naibu Spika, ulikuwa na gari moja na katibu wako tu, lakini leo hii naibu ana walinzi wawili na msafara wa magari mengi.

“Tunazungumzia mipango, lakini mipango bila utaratibu haiwezi kuwa mipango, watu wanalalamika sana, tukizungumzia Uwanja wa Ndege wa Chato, hakuna mwenye tatizo napo, tatizo ni namna ilivyokuja na utaratibu wake,” alisema Mbilinyi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here