31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Vyama 8 vyajitoa uchaguzi Z’bar

Mohammed_masudNA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

VYAMA nane vya siasa vimejitoa rasmi kushiriki uchaguzi wa marudio utakaofanyika Machi 20, mwaka huu visiwani Zanzibar.

Pia vyama hivyo, vimemshangaa Rais Dk. John Magufuli kudai hahusiki na uchaguzi wa Zanzibar  wakati amepeleka majeshi kulinda amani visiwani humo.

Tamko hilo lilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa umoja wa vyama hivyo, Mohamed Masoud Rashid ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi na Maendeleo (Chauma).

“Kama anaona Zanzibar haimhusu, ni vyema akaondoe majeshi yake na sisi tuendelea kudai haki yetu ya kikatiba,”alisema Rashid.

Alisema tamko la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha la Oktoba 28, mwaka jana  halina uhalali wowote, hivyo ni dhahiri kuwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana haujafutwa.

“Kutoakana na kauli zetu, sisi vyama shiriki wa uchaguzi uliopita tunatamka rasmi kuwa ZEC haina mamlaka ya kufuta uchaguzi na wala haina mamlaka ya kuandaa marudio ya uchaguzi mwingine,”alisema Rashid.

Alisema kitendo cha Jecha kujinyakulia mamlaka ya kikatiba na kisheria, ni uvunjaji mkubwa wa Katiba na sheria.

“ Baada ya kufuatilia kwa makini barua ya ZEC, tumebaini haina umakini wa kufuata Katiba na sheria katika uandishi na utekelezaji wa hoja…kibaya zaidi tume imethubutu kupuuza na kuvunja Sheria ya Uchaguzi wa Zanzibar namba 11 ya 1984 ,”alisema Rashid.

“Hakuna kikao chochote cha Tume ambacho kilikaa kwa ajili ya kufikia uamuzi wa kufuta uchaguzi ili kukidhi kiwango cha mikutano ya Tume na kutoa uamuzi ambao ungeungwa mkono na wajumbe walio chini ya Katiba ya Zanzibar,” alisema.

Alisema hawana imani kama uchaguzi wa marudio utakuwa huru na wa haki na badala yake wanategemea hali inaweza kuvurugika.

“Ni wajibu wa tume kuzingatia matakwa ya sheria na Katiba zinazosimamia uchaguzi na haiwezekani kuepuka misingi na matakwa ya wananchi katika kuchagua viongozi wanaowataka na Tume haina mamlaka yoyote,”alisema Rashid.

Vyama  ambavyo vimejitoa kushiriki uchaguzi huo, ni Chama cha Chauma, Democratic Party (DP), Demokrasia Makini , Sauti ya Umma (SAU), Jahazi Asilia, National Reconstruction Alliance (NRA), UPDP na UMD.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles