31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Vurugu zavunja mkutano CUF

Mwenyekiti wa zamani wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, akiongozwa na maofisa wa polisi kuingia kwenye ukumbi uliofanyika Mkutano Mkuu Maalumu Dar es Salaam jana.
Mwenyekiti wa zamani wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, akiongozwa na maofisa wa polisi kuingia kwenye ukumbi uliofanyika Mkutano Mkuu Maalumu Dar es Salaam jana.

Patricia Kimelemeta na Jonas Mushi,

NI vurugu. Ndivyo unavyoweza kusema hasa baada ya Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama cha Wananchi (CUF), kuvunjika.

Hatua hiyo imekuja baada ya wafuasi wa Lipumba, kupinga uamuzi uliouita wa kura za kutengenezwa za kuridhia kuondoka kwa Mwenyekiti wao aliyejiuzulu katika nafasi yake Agosti mwaka jana.

Pamoja na hali hiyo Julai mwaka huu, aliutangazia umma kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu na kutaka kurudi katika nafasi yake ya uenyekiti hali iliyolazimu askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kuingilia kati na kuwatawanya wafuasi hao.

Uamuzi huo ambao ulitarajiwa kufikia tamati jana umegeuka kaa la moto ambapo uliibuka mvutano mkali kati ya wafuasi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi(CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na kundi linalomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad katika Mkutano Mkuu Maalumu wa kujaza nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.

Katika mkutano huo ambao ulitawaliwa na sura mbili za Utanganyika na Zanzibar, wajumbe wa pande hizo mbili walirushiana vijembe ndani ya ukumbi, huku kila kundi likivutia upande wake wakati wa kuamua hatima ya kuondolewa au kurudi ndani ya uongozi kwa Prof. Lipumba.

Mkutano huo uliofanyika jana katika Hoteli ya  Blue Pearl Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam ulianza saa tano asubuhi, ambapo ndani na nje ya ukumbi wafuasi wa Profesa Lipumba walikuwa wakihaha kuzungumza na wajumbe, huku wengine wakiimba nyimbo mbalimbaliza chama hicho.

Ndani ya ukumbi

Dalili za vurugu zilianza kuonekana baada ya wajumbe kumchagua mwenyekiti wa mkutano huo, Julius Mtatiro, ambapo baada ya kueleza namna atakavyoendesha kikao hicho, baadhi ya wajumbe walianza kumrushia vijembe na kudai kuwa ameteuliwa kwa mkakati maalumu na viongozi wa juu wa chama hicho.

Pamoja na hali hiyo wakati akisoma ajenda za mkutano huo, wajumbe walihoji hatua ya kutokuwapo Profesa Lipumba, ambaye angeeleza sababu zake mbele ya Mkutano Mkuu kuliko maelezo yaliyotolewa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.

Kutokana na hali hiyo wajumbe hao waliibuka huku mjumbe wa mkutano huo,  Maftah Nachuma ambaye pia ni Mbunge wa Mtwara Mjini alisema Ibara ya 77 (7) ya katiba ya chama inaelekeza kuwa maamuzi halali ya Mkutano Mkuu ni yale yatakayoungwa mkono na 2/3 ya wajumbe wa Zanzibar na 2/3 ya wajumbe wa Tanzania bara.

Alisema kwa msingi wa ibara hiyo, kura zinatakiwa kupigwa kwa kuwatenga wajumbe suala ambalo lilipingwa na baadhi ya wajumbe wengine.

Hata hivyo mjumbe mwingine Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, alisema kuwa anashangazwa na suala la Profesa Lipumba, kutaka lisijadiliwe huku mwenyewe akiwemo.

“Mheshimiwa Katibu Mkuu ninachotaka kusema hapa kama kweli tunakiri hapa kuwa Lipumba amekifanyia kazi chama chetu, kwanini hata kwenye huu mkutano hakualikwa. Aitwe hapa na aeleze sababu za kujiuzulu kwake kuliko hicho unachokisema wewe (Maalim Seif).

“Hapa kuna kubaguana kwa wazi kabisa ndiyo maana hata wakati wa Uchaguzi Mkuu uligawa pikipiki, magari kwa CUF wenzetu wa Zanzibar sisi huku bara hata baiskeli tulikosa.

“Lakini hata kwenye hayo makabidhiano hata Profesa Lipumba hakuwepo,” alisema mjumbe huyo ambaye alijitambulisha kuwa ni Mwenyekiti wa CUF mkoani Mtwara.

Ilipotimu saa Saa 8:45 mchana Profesa Lipumba aliwasili katika eneo hilo la mkutano, huku akipokewa na wafuasi wake waliokuwa nje ya jengo hilo kwa nyimbo na vigelegele.

Hata hivyo hadi kufikia saa 9:15 alasiri hakukuwa na mwafaka wowote, ambapo mwenyekiti wa Muda, Julius Mtatiro, aliahirisha mkutano kwa mapumziko ya saa moja.

Chanzo chetu kingine kilieleza kwamba, baada ya Profesa Lipumba kuingia ndani ya ukumbi, mvutano mwingine uliibuka wa namna ya upigaji kura ambapo baadhi ya wajumbe walisema kura zinatakiwa kutenganishwa bara na Zanzibar.

Juma Duni ajitoa

Awali akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Uchaguzi na Mipango, Shaweji Mketo alielezea ajenda ya mkutano huo kuwa ni kutoa taarifa ya kujiuzulu kwa Lipumba na kufanya uchaguzi wa nafasi zilizo wazi.

Pia alitoa taarifa ya uamuzi wa kikao cha Baraza Kuu la Uongozi  Taifa kilichokaa juzi na kupendekeza majina ya wagombea wa nafasi zilizo wazi.

“Jana (juzi) tulikaa kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa ambapo tuliandaa agenda za Mkutano Mkuu Maalum pamoja na kupendekeza majina matatu ya wagombea wa nafasi zilizo wazi,” alisema Mketo na kuongeza.

“Wakati tukiwa kwenye kikao tulipokea barua kutoka kwa wagombea wawili wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti bara akiwemo Juma Duni Haji ambaye alisema ameamua kufanya hivyo ili kukidhi matakwa ya kikatiba na kuepusha mvutano,” alisema.

Mketo alisema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, kiongozi atakayejiuzulu nafasi yake atapaswa kugombea nafasi hiyo baada ya miaka miwili tangu ajiuzulu.

Alisema pamoja na sharti hilo chama kiliona Duni ni mtu muhimu ndani ya chama hivyo waliamua kuacha agombee nafasi hiyo.

Mgombea mwingine aliyejitoa katika nafasi hiyo ni Dk. Juma Amir Muchi, ambaye naye aliandika barua na kusema amejitoa kwa hiari yake.

Alisema wagombea waliopitishwa na Baraza Kuu la Uongozi kwa nafasi ya makamu mwenyekiti ni Mussa Haji Kombo  na Salim Bimani.

Katika nafasi ya mwenyekiti, walijitokeza wagombea tisa huku akitaja majina ya watu waliopendekezwa na Baraza Kuu kuwa ni Juma Nkumbi, Twaha Taslima na Riziki Shahali  Ngwali.

Kura zapigwa

Baada ya mvutano wa muda mrefu iliamuriwa kupigwa kwa kura na wajumbe wa Mkutano Mkuu na kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti wa mkutano huo, Julius Mtatiro, wajumbe 476 waliamua Profesa Lipumba aondoke, huku 14 wakitaka aendelee kubaki katika nafasi ya uenyekiti.

Baada ya kukamilika kwa zoezi la kupiga kura, wafuasi wa Profesa Lipumba, walipinga zoezi la upigaji kura kwa madai kuwa katiba ya chama hicho haikuzingatiwa na kura hizo zimefanyika katika mazingira ya vurugu, kwani wanachama walikataa kupiga kura na wengine walikua wanalia.

Kutokana na hali hiyo, wafuasi wa Profesa Lipumba walitoka nje na kuanzisha vurugu huku wakidai kuwa hakuna kiongozi yeyote atakayekanyaga kwenye ofisi kuu za chama hicho zilizopo Buguruni.

“Wabaki na chama chao na sisi tubaki na majengo yetu ya Buruguni, hakuna mtu atakayekanyaga pale, hapo ndiyo tutajuana, bora tugawane mbao wa Zanzibari wabaki na chama chao na sisi tubaki na majengo yetu.

“Haiwezekani Maalim Seif atoke Zanzibar aje Dar es salaam kuvuruga chama kama yeye alishindwa ni huko huko, si huku kwetu, hatukubali mpaka kieleweke,” walisikika baadhi ya wafuasi hao wa Lipumba waliokuwa wakizungumza kwa jazba.

Wafuasi ukumbini

Ilipotimu saa 11 jioni hali ilianza kubadilikana huku wafuasi wa Lipumba waliokua nje walilazimika kuingia ndani ya ukumbi.

Baada ya kungia walianza kupambana kutaka mbele ya meza kuu kwa lengo la kuwapiga viongozi akiwemo Maalim Seif na kuanza kurusha viti hali ilizua taharuki.

Timu ya MTANZANIA iliyokuwa ndani ya ukumbi huo iliwashuhudia wajumbe hao wakimshikiza kuondolewa kwa viongozi hao “Ondokeni nendeni kwenye Zanzibar hii bara hamuwezi kutuendesha mnavyotaka ninyi hapa ni Lipumba tu,” walisikika wafuasi hao.

Ilipotimu saa 1:45 usiku Mtatiro alilazimika kuahirisha mkutano huo hadi utakapotangazwa tena.

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa viongozi wa juu wa chama hicho wamegawanyika, kutokana na kila mmoja kuunga mkono kundi analoamini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles