30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Vituko vya mwakilishi wa Rais Kikwete

mgsNa Peter Fabian, Mwanza
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, ambaye ni mwakilishi wa Rais Jakaya Kikwete mkoani hapa, amebuni aina mpya ya ulinzi wake binafsi pamoja na msafara wa magari unaoambatana naye anapokuwa katika ziara zake za kikazi.
Aina hiyo ya ulinzi na msafara wake wa magari unaofanana kwa kiwango kikubwa na ule wanaopewa viongozi wakuu wa kitaifa, akiwemo Rais na Waziri Mkuu, ni wa kwanza kushuhudiwa na wakazi wa mkoani hapa na umedaiwa kugharimu kiasi kikubwa cha fedha.
MTANZANIA Jumamosi limeushuhudia msafara huo unaowajumuisha pia askari wa usalama barabarani ambao kazi yao ni kujipanga barabarani na kuwazuia watumiaji wengine wa barabara wenye magari ili kusitisha kwanza safari zao mpaka hapo Mulongo na msafara wake wanapopita.

Katika msafara wake, Mulongo huambatana na Mkuu wa Polisi wa wilaya husika, maofisa usalama wa wilaya na mkoa, magari kadhaa ya watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza pamoja na maofisa wa wilaya anazozitembelea.
Sambamba na msafara huo wa magari, Mulongo pia analindwa na makundi matatu ya wanausalama ambao ni askari polisi wa kawaida, askari kanzu na maofisa usalama wa taifa.
Ingawa amekuwa akitumia aina hii ya ulinzi na usafiri hata katika safari zake za kawaida asubuhi anapotoka katika hoteli ya kitalii anayoishi kwenda ofisini wake, katika ziara yake ya kujitambulisha kwa wakazi wa Mkoa wa Mwanza aliyoianzia Wilaya ya Ilemela, ulinzi wake ulionekana kuimarishwa zaidi, huku idadi ya magari kwenye msafara wake nayo ikiongezeka.
Watu wa makundi mbalimbali waliozungumza na MTANZANIA Jumamosi kuhusu aina huyo mpya ya msafara na ulinzi wa Mulongo, wameeleza kushangazwa na jinsi mkuu huyo wa mkoa anavyojikweza na mwenendo wake wa kiuongozi waliodai kuwa una chembechembe za vitisho.
Wakizungumza kwa sharti la majina yao kutoandikwa gazetini kwa kile walichodai kuwa ni kuhofia kushughulikiwa na Mulongo, walisema wana mashaka na mwenendo wa kiongozi huyo na kubashiri kuwa unaweza kuwa na athari mbaya kwa serikali na hata Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika baadhi ya maeneo ambayo Mulongo alifika kujitambulisha na kuzungumza na wananchi alionya kuwa serikali itawachukulia hatua wale ambao wamekuwa wakijitokeza kwenda kulinda kura za wagombea wao nyakati za uchaguzi.
“Nimekuja kwenu kujitambulisha kama Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, hilo ndilo lengo la ziara yangu hii ambayo ni ya kwanza tangu nifike mkoani hapa.
“Nataka mtambue kuwa jukumu lenu la kwanza ni kukomesha uhalifu, niwasihi toeni taarifa za uhalifu polisi. Lakini naambiwa na ninyi mna tabia ya kubeba mawe na silaha za jadi kwa madai ya kwenda kulinda kura katika maeneo ya vituo vya kupigia kura, sasa nawatahadharisha kuwa watakaobainika na kukamatwa watajuta na waliowatuma tutawashughulikia,” alionya Mulongo.

Kabla ya kutoa onyo hilo, wakazi wa Wilaya ya Nyamagana waliohudhuria mkutano wa kujitambulisha ulioitishwa na Mulongo, walitumia fursa hiyo kutoa kero zao kwa kumueleza kuwa wakazi wa maeneo ya Bugando na Igogo wamekuwa wakivamiwa na kuporwa mali zao na vijana wa genge la kihalifu la Panya Road.
“Kuna wimbi la vijana wanaowavizia watu nyakati za usiku na kuwanyang’anya simu za mkononi na wanawake wamekuwa wakikabwa na kuchukuliwa mikoba na vito vya thamani, tunaomba msaada wa askari polisi kufanya doria maeneo mbalimbali hapa Igogo ili kuondoa kero hii,” alisema mmoja wa wakazi wa maeneo hayo.
Baadaye Mulongo na msafara wake walielekea Kata ya Butimba na kuzungumza na wananchi katika eneo la Stendi Kuu ya Mabasi ambako alielezwa kuwa eneo hilo halina miundombinu ya uhakika ya maji taka na vyoo vinahitaji ukarabati.
Mmoja wa maofisa wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mhandisi Ezekiel Kunyaranyara, ambaye alitakiwa na Mulongo kutolea maelezo suala hilo, alisema taratibu za manunuzi ndizo zinazochelewesha ukarabati huo, lakini tayari mkandarasi yupo eneo la stendi akiendelea na kazi.
Majibu hayo yalionekana kumkera Mulongo, ambaye alimkaripia Kunyaranyara kwa kumtaka asikilize maagizo yake kwa sababu akiagiza kitu lazima kitekelezwe haraka.
Alisema amehamishiwa mkoani Mwanza kwa ajili ya kufanya kazi kwa maelekezo maalumu, kwa hivyo watendaji wasiotimiza wajibu wao wajue watapoteza kazi.
Katika ziara yake hiyo, Mulongo alitembelea Kata za Nyamagana, Igogo, Butimba, Buhongwa, Mirongo, Pamba na Igoma kwa upande wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza (Nyamagana) na Ilemela alitembelea Kata za Sangabuye, Bugogwa, Kirumba, Pasiansi na Busweru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles