27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

VITISHO VYA TRUMP NI KINYUME NA MAADILI YA MAREKANI


Na MICHAEL KNIGGE (DW)

MAJIBU ya utawala wa Trump juu ya azimio la UN kuhusu hadhi ya mji wa Jerusalem yanaonyesha rais huyo yuko tayari kucheza mchezo wa wafuasi wake hata kwenye jukwaa la kimataifa, anasema Michael Knigge katika maoni yake.

Kwanza kabisa tunapaswa kuweka mambo mawili wazi. Ni haki ya Rais Donald Trump, kuitambua kivyake Jerusalem kama mji mkuu wa Israel, hata kama hili linakwenda kinyume na sera ya muda mrefu ya Marekani ya kutoegemea upande na hata kama hili linakiuka onyo lililotolewa na washirika wa Marekani kutoka mataifa ya Ulaya na ya Kiarabu kutofanya hivyo.

Vivyo hivyo ni haki pia kwa wanachama wa Umoja wa Mataifa kuelezea kutoridhishwa kwao na uamuzi wa Trump kwa kupigia kura azimio ambalo bila kuitaja Marekani na rais wake moja kwa moja,  lilikosoa hatua yake na kusisitiza kuwa hadhi ya mwisho ya Jerusalem itaamuliwa kupitia majadiliano kulingana na maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu jambo hilo.

Katika muktadha huo, ni muhimu kubainisha kwamba azimio hilo halifungamanishi, hii ikimaanisha kuwa halina nguvu ya kisheria na hivyo ni la kiishara kwa sehemu kubwa.

Ingawa azimio hilo halina madhara yoyote ya kivitendo, utawala wa Trump ulivurunda katika kulishughulikia. Imeonyesha dhahiri namna utawala huo ulivyoonyesha kuvurunda katika jambo hili dogo la sera ya kigeni.

Hili halikupaswa kuja kama jambo la kushangaza hata kwa mtu ambaye amekuwa akifuatilia kwa pembeni, mgogoro wa Mashariki ya Kati kwa kipindi cha miongo miwili iliyopita, kwamba hatua kama ya Trump kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel ingepelekea mataifa ya Kiarabu na mengine kupinga uamuzi huo katika Umoja wa Mataifa.

Ukifahamu hili na bila uwezo wa kuzuia kile ambacho ni onyesho la kiishara la upinzani kwa hatua ambayo ni ya utata, utawala wa Trump ulipaswa tu kutoa taarifa ya kukosoa kura hiyo ikiambatana na kiapo kwamba Washington inasimamia uamuzi wake.

Lakini kama ilivyotarajiwa, utawala wa Trump ulichagua kutofanya hivyo. Badala yake uliingia mzima mzima katika makabiliano.

Wakati tabia ya rais huyo alieko madarakani kumshambulia kila anayethubutu kumpinga, kumkosoa au kumfanyia mzaha kupitia twitter imepungua kwa kiasi fulani, kumwona balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, akitumia mtandao huo kutoa vitisho kwa mataifa yanayopanga kuunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa kwamba Marekani itakuwa inaandika majina, ni jambo lililopotoka.

Lina sauti ya mtawala wa kibabe anayewalazimisha walio chini yake kusalimu amri na si ya mwakilishi wa nchi ambayo kijadi inajichukulia kuwa nguzo ya demokrasia.

Kinachosumbua zaidi, ambacho ni vigumu kuhukumu siku hizi, ni kitisho kwamba Marekani ingekata msaada kwa mataifa yanayounga mkono azimio hilo na barua ya onyo iliyotumwa na Haley kwa wanachama wa Umoja wa Mataifa kabla ya kura hiyo.

La mwanzo si tu lingeyaumiza mataifa yaliyoathirika, lakini pia Marekani yenyewe, kwa vile msaada huo unaipa Marekani nguvu ya ushawishi katika mataifa hayo.

La mwisho lilifikia kilele katika sentensi inayosema; “Rais atakuwa anafuatilia kura hii kwa uangalifu na ameomba niripoti kwake juu ya waliopiga kura dhidi yetu,” jambo linalosikika kama mwalimu wa shule ya msingi anayewatishia wanafunzi watukutu kwamba mkuu wa shule anawafuatilia.

Hili linasikika kama kichekesho, lakini si kichekesho. Kwanza, kwa sababu linaonyesha kwamba hisia za utawala wa Trump na mkakati wake wa diplomasia ya kimataifa vinaweza kujumlishwa kama “njia yangu au njia kuu,” ambayo ni nakala ya mkakati wa ndani uliompelekea Trump kuchaguliwa.

Pili, inaonyesha ushamba wa utawala wa Trump kuamini kwamba kuyatishia mataifa huru unaweza kuwa mkakati wa busara, ukweli unaoshadidiwa na matokeo ya kura hiyo.

Na tatu, inaonyesha utayarifu kwa upande wa utawala wa Trump kudhoofisha hata kilichobakia katika nia njema ya Washington na washirika wengi muhimu wa kimataifa kwa ajili ya kuwaridhisha wafuasi wake wa ndani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles