24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Vita ya ujangili yaundiwa mkakati mpya

KAMILI MMBANDO

VITA ya ujangili ni moja kati ya vita kubwa ambazo Serikali imeamua kupambana nazo kulifanya taifa kujitegemea kiuchumi.

Ujangili ni uwindaji haramu wa wanyamapori unaofanywa katika hifadhi na watu wanaofanya kazi hiyo huitwa majangili ambao huvuruga sekta ya utalii ambayo ina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi yetu.  

Majangili walio wengi hupendelea zaidi kuwaua tembo na faru na huchukua pembe zao na kuziuza kwa gharama kubwa wakitafuta utajiri wa haraka usiokuwa halali kwa gharama ya rasilimali zetu.

Mwaka jana pekee sekta hiyo ilichangia asilimia 17 ya pato la taifa jambo ambalo linatulazimu kama taifa kuimarisha vivutio hivyo vya asili kwa kuhakikisha ujangili unakomeshwa kabisa na kuona wanyama kwenye mbuga zetu wakiendelea kuzaliana na kuongezeka ili kuvutia utalii.

Licha ya umuhimu huo, miaka ya hivi karibuni idadi ya tembo katika hifadhi zetu ilipungua zaidi hususani katika Pori la Akiba la Selous na Ruaha kutokana na kuwapo ujangili mkubwa kwenye maeneo hayo.

Ikumbukwe kwamba ujangili ulishamiri zaidi mwaka 2005 na 2017 na kusababisha zaidi ya tembo 30,000 barani Afrika kutoweka. 

Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2007-2014, idadi ya tembo barani Afrika ilipungua kutokana na kuongezeka kwa ujangili ulioangamiza zaidi ya tembo 140,000. 

Aidha barani Afrika idadi ya tembo inazidi kupungua  kutokana na kuharibiwa kwa mazingira yao ya asili huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni ujangili.  

Inakadiriwa kuwa jumla ya tembo walio katika ukanda wa Savana katika nchi 18 zilizojumuishwa ni 352,271 (sawa na asilimia 93) ya tembo wote katika nchi hizo. 

Nchi zilizohusika kwenye utafiti huo ni  Botswana ambayo ilichangia maeneo ya tafiti kwa asilimia 37, Zimbabwe asilimia 23 na Tanzania asilimia 12 huku Angola, Tanzania na Msumbiji zikiongoza kwa vifo vya tembo. 

Kutokana na Tanzania kuwa ni moja ya nchi inayoongoza kwa kuwa na vifo vingi vya tembo, Serikali iliamua kuweka jitihada za makusudi kupunguza vitendo vya ujangili nchini.

Moja ya jitihada hizo ni pamoja na kuanzisha kikosi kazi cha taifa cha kupambana na kuendesha operesheni maalum za mapambano dhidi ya ujangili. 

Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Serikali la Pams Foundation walibuni mbinu za kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zinakwamisha vita dhidi ya ujangili.

Moja ya jitihada hizo ni kuondoa vikwazo vilivyokuwa vikisababishwa na mifumo kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa watuhumiwa kushindwa kutumikia adhabu zao na kujikuta wakishinda kesi mahakamani na kuwa huru.

Katika kujadili changamoto hizo iliandaliwa warsha maalum ya kukijengea uwezo kikosi kazi hicho kinachojumuisha vyombo vya ulinzi na usalama, maafisa forodha,Takukuru na mamlaka za hifadhi za Taifa. 

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolph Mkenda alifungua warsha hiyo mkoani Dodoma Januari 21-25 na kusema jitihada zilizofanywa na Serikali kupambana na ujangili zimeonyesha kuzaa matunda. 

Anasema kiwango cha mauaji ya tembo katika hifadhi za taifa kimepungua hadi kufikia 23 kwa mwaka 2018, ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka ya 2016-2017. 

Anasema mwaka 2016-2017 mauaji ya tembo yalikuwa194, lakini juhudi za vyombo vya ulinzi na usalama zimesababisha kupungua kwa ujangili hadi kufikia idadi hiyo hususani katika Pori la Akiba la Selous na Ruaha.

Katika kipindi hicho meno 211 na vipande 413 vya meno ya tembo vilikamatwa, silaha 355 na risasi zaidi ya 20,000 kutokana na ushirikiano wa vyombo hivyo. 

Aidha Katibu Mkuu huyo anagusia kesi za wahalifu ambapo anawataka maofisa kuwa na vielelezo na ushahidi wa kutosha utakao wasaidia kuendesha kesi mahakamani na kutolewa hukumu stahiki ili kuepuka changamoto ya kukamata wahalifu, kuwafungulia mashtaka kisha wakaachiwa huru.

“Jambo la kesi linahitaji umakini mkubwa kwakuwa hakuna kitu kibaya kama kumkamata mhalifu anashtakiwa halafu baada ya siku chache unakutana naye mtaani anatembea kifua mbele na kuanza kukubeza,”anasema. 

“Jitihada za kikosi kazi cha kuzuia uharifu na ujangili katika hifadhi zetu haziwezi kuzaa matunda kama hazitaungwa mkono na Jeshi la polisi licha kwamba wawekezaji wamekiri kuongezeka kwa idadi ya wanyama katika mbuga ya Selous na Ruaha lakini jitihada zaidi zinahitajika kukabiliana  na vitendo vya ujangili,” anasema Profesa Mkenda kwenye hotuba yake. 

“Hata hivyo naomba msilegeze kamba kutokana na mafanikio haya, wahalifu hawachoki wanabadili mbinu kila kukicha, hivyo muendelee na uzi ule ule kuhakikisha ujangili unabaki historia katika nchi yetu,” anasisitiza. 

Mkurugenzi Msaidizi na Mwenyekiti wa kikosi kazi Taifa cha kuzuia na kupambana na ujangili, Robert Mande anasema lengo la warsha hiyo ni kutengeneza mtandao na kuondoa vikwazo vinavyokuwa vikiikabili sekta hiyo.

“Tuligundua majangili wana umoja na wana mbinu nyingi, hivyo ni lazima na sisi tutengeneze mtandao na kuondoa vikwazo vilivyopo ili kufikia malengo tuliyojiwekea na kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu ujangili.”anasema.

Aidha mkurugenzi huyo anasema silaha zilizokuwa zikitumika katika ujangili ni silaha za kivita kama vile AK47, SMG, UZI GUN, Rifle, SAR, Short Gun na Gobole. 

Mkurungezi wa Taasisi ya Pams Foundation, Elisifa Ngowi iliyodhamini warsha hiyo alipongeza hatua ya kuunganisha nguvu ya pamoja kwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama na kudai kuwa itasaidia kuondoa mauaji kufikia ziro ifikapo 2024.

Naye InspektaGenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro ambaye alifunga warsha hiyo alikitaka kikosi kazi hicho kilichoundwa kutumia taarifa za kiintelijensia kuwabaini wahalifu kwa kutambua wapi ulikoanzia na kuushughulikia. 

Pia alikitaka kikosi kazi hicho kuweka pembeni tofauti zao na kuaminiana kuondoa uhalifu huo kwa kuwa magaidi kote duniani hiyo ndiyo silaha yao kubwa katika kufanya vitendo vya ujangili. 

Sirro anasisitiza kuwa raslimali zote ni mali ya taifa si mali ya mtu wala taasisi, hivyo kikosi kazi hicho kinapaswa kushirikiana kwa kuweka mbele maslahi na uzalendo kwa nchi yao ili kufanikisha oparesheni hiyo. 

“Ujangili ni moja ya makosa makubwa ya kimtandao duniani ambayo yanachukua nafasi ya nne nyuma ya biashara haramu ya dawa za kulevya, usafirishaji silaha haramu na usafirishaji haramu wa binadamu. 

“Ujangili na biashara haramu ya mazao ya wanyama na misitu si tu imekua na kufikia hatua ya kutisha, bali inashirikisha makundi makubwa ya uhalifu duniani yanayomiliki silaha mbalimbali za kivita ambazo hutumika pia katika biashara ya silaha na usafirishaji haramu wa dawa za kulevya, ugaidi na uharamia,”anasema IGP Sirro na kuendelea:

“Biashara haramu ya nyara ni chanzo kimojawapo cha kujipatia rasilimali fedha kwa ajili ya kufadhili harakati za vikundi vinavyosababisha vitendo vya kigaidi na waasi duniani kote. 

Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo, Juma Julius anasema semina hiyo ni nyenzo muhimu itakayosaidia kujenga mtandao utakaofanikisha kupeana taarifa za ujangili kutoka katika maeneo yote ya nchi.

Julius ambaye ni Ofisa forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tunduma anasema kupitia semina hiyo wamejifunza mbinu za kuwabaini watakatishaji fedha, utoroshwaji wa magogo na masuala ya kiintelejensia. 

“Kupitia semina hii tumepata uzoefu kutoka kwa wahusika waliobobea katika kukamata na kuzuia uhalifu wa namna hiyo ambao umetujenga na tutaufanyia kazi ili kuhakikisha nchi inakuwa salama zaidi,”anabainisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles