31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

VIONGOZI CHADEMA ARUSHA WAKAMATWA NA POLISI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo.

Na JANETH MUSHI-ARUSHA

JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu 12, wakiwemo viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Arusha.

Viongozi hao walikamatwa kwa amri ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo wakituhumiwa kuhusika kuchoma moto mashine za kuvuta maji kutoka kwenye chanzo cha Kangdet wilayani Karatu kwa madai kwamba wanatekeleza agizo la Serikali, hatua ambayo imeelezwa kuwa haikufuata utaratibu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, aliwataja waliokamatwa kuwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Karatu, Moshi Darabe ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Barai, anayedaiwa kuhamasisha wananchi kuchoma moto mashine hizo zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 16.

Wengine waliokamatwa ni Diwani wa Kata ya Mang’ola, Lazaro Emanuel, viongozi wa vijiji vya kata hizo pamoja na baadhi ya wananchi.

Kamanda Mkumbo alisema kuwa msako wa kuwakamata watuhumiwa wengine waliohusika na tukio hilo bado unaendelea na uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

Desemba 27, mwaka huu, kundi la wananchi wa vijiji vinne vya  kata hizo waliandamana, wakang’oa na  kuchoma moto mashine za kuvuta maji katika chanzo cha  maji cha Kangdet, kinachotegemewa na  vijiji vingine vya Kata ya Barai.

Kutokana na tukio hilo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ikiongozwa na mwenyekiti wake ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Gambo, walitembelea eneo la tukio na baada ya viongozi kueleza kilichotokea, aliagiza kukamatwa kwa watu wote waliohusika na uharibifu huo.

“Sheria lazima ichukue mkondo wake kwani agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa lilikuwa wazi na halikusema wananchi wachukue sheria mkononi, jambo hili ni kinyume cha sheria,” alisema Gambo katika mkutano huo.

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Jubilate Mnyenye (Chadema), alisema kuwa yeye, mbunge wa jimbo hilo, Willy Qambalo na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mang’ola, Jacob Pius, wametakiwa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi jijini Arusha leo asubuhi kwa mahojiano kuhusu tukio hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles