24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

VIGOGO WATUMBULIWA WIZARA YA ELIMU

 

NA TIGANYA VINCENT- TABORA


WAZIRI Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako,  amemwagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuwaondoa   Mratibu wa Miradi na Kaimu Mkurugenzi  wa Mafunzo ya Ualimu kwa kushindwa kusimamia majukumu yao na kusababisha baadhi ya miradi kushindwa kukamilika kwa wakati.

Amewataja viongozi hao kuwa  ni Mratibu wa Miradi, Fredrick Shuma na Kaimu Mkurugenzi wa Mafunzo ya Ualimu, Basiliana Mrimi.

Profesa Ndalichako alitoa agizo hilo wilayani Nzega jana wakati akikagua mradi wa upanuzi wa Chuo cha Ualimu Ndala  ambako alikuta miradi hiyo iko katika hali isiyoridhisha.

Alisema utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa Chuo cha Ualimu cha Ndala hauridhishi na kusababisha  wanachuo wengi washindwe kuanza masomo   mwaka huu.

Profesa Ndalichako alisema watendaji hao ni miongoni mwa waliosababisha vifaa kwa ajili ya vyuo vya ualimu vya sayansi kupelekwa katika vyuo ambavyo havifundishi sayansi na kusababisha  baadhi kupitwa na wakati na kusababisha hasara kwa Serikali.

Profesa Ndalichako pia  alitoa onyo kwa Mhandisi wa wizara hiyo, George Sambali kwa kushindwa kukagua miradi ya ujenzi inayoendelea hadi wasubiri waziri na naibu wake watembelea ndiyo nao waonekana.

Alisema  jambo hilo linasababisha kujengwa   miradi chini ya kiwango  na inachukua muda mrefu.

“Suala la kuhakiki ubora wa miradi ni kazi ya wataalamu na siyo kungoja viongozi waendee ndiyo marekebisho yafanyike.

“Jambo hili ndilo linasababisha baadhi ya miradi kuchelewa,” alisema Profesa Ndalichako.

Waziri  alimuonya Mkuu wa Chuo cha Ualimu Ndala, Abinego Ndikumwe, kutopokea majengo yaliyokarabatiwa na United Builders ambayo yameonyesha kuwa na upungufu.

Alisema kabla ya kuyapokea  ahakikishe wahusika wamefanyia kazi upungufu wote na kufikia Novemba mwaka huu wawe wamekabidhi kazi hiyo ikiwa kamili.

Tumbua ilivyokuwa

Februari 16, 2016, Waziri Profesa  Ndalichako alisimamisha mkataba wa ajira wa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo, George Nyatega na kuwasimamisha kazi wakurugenzi watatu.

Alisema hali hiyo ilisababishwa na matatizo ya utendaji na matumizi mabaya ya fedha za umma yanayofanyika ndani ya Bodi ya Mikopo.

Waliosimamishwa wakati huo ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Yusuph Kisare, Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo Juma Chagonja na Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo,  Onesmo Laizer.

Alizitaja baadhi ya sababu za kufukuzwa na kusimamishwa kazi kwa watumishi hao kuwa ni pamoja na  kufanya malipo yasiyo sahihi kwa baadhi ya wanafunzi wanaosoma ndani na nje ya nchi na udhaifu uliobainika katika mifuko ya fedha.

Siki chache baadaye, Waziri Ndalichako, aliwasimamisha kazi watumishi wengine watatu wa Bodi ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kushindwa kusimamia sheria ya ununuzi na kazi ya uchapaji wa vitabu kupisha uchunguzi.

Kusimamishwa kwa watumishi hao kulitokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kuruhusu vitabu kuchapishwa vikiwa na upungufu.

“Mnamo Januari 22, mwaka 2016 bodi hiyo ilishauriwa kusimamisha uchapaji wa vitabu uliokuwa ukifanywa na kampuni ya Yukos Enterprises Ltd baada ya kubainika kuwa na upungufu lakini haikusimamisha,”  alisema aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Maimu Tarishi  kwa niaba ya Ndalichako

Aliwataka watumishi hao kuwa ni aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Idara ya Vifaa vya Elimu,  Peter Bandio, Mwanasheria wa TET, Pili Magongo na Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi, Jackson Mwaigonela

Upungufu ulioonekana kwenye vitabu hivyo ni    mwingiliano wa rangi, upungufu wa kurasa katika vitabu, ukataji usiozingatia vipimo, vitabu kuchakaa kabla ya matumizi na mpangilo mbaya wa kurasa.

Mei 25, 2016,  Profesa Joyce Ndalichako, aliivunja Bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na kuwasimamisha kazi watendaji wa bodi hiyo kwa kushindwa kusimamia suala la wanafunzi  489 wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph ambao hawakuwa na sifa ya kujiunga na elimu ya juu.

vv Waziri Ndalichako alimteua Profesa Eleuther Mwageni na Dk. Kokubelwa Katunzi kukaimu nafasi ya bodi hiyo.

Agosti 9, mwaka huu, Waziri   Ndalichako, alimuagiza katibu mkuu wa wizara hiyo, kuwasimamisha kazi wakuu wa idara ya fizikia na kemia wa Chuo cha Ualimu Morogoro.

Alitoa uamuzi huo wakati akizungumza na wakufunzi wa chuo hicho   mkoani Morogoro.

Alisema wakuu hao wa idara wanadaiwa kudanganya kuhusu matumizi ya vifaa vya maabara vilivyopelekwa chuoni hapo kutoka wizarani.

Waliohusika na agizo hilo la kusimamishwa kazi ni Mkuu wa Idara ya Fizikia, Noel Mgana na Mkuu wa Idara ya Kemia, Josephat Temba ambao walidaiwa kushindwa kueleza ukweli kuhusu kutokutumika  vifaa vingi vya maabara ambavyo vingine vinaelekea kuisha muda wake wa matumizi.

Katika hatua nyingine, aliagiza Ofisa Ununuzi wa Wizara ya Elimu, Audifasy Myonga, kusimamishwa kazi kwa kununua vifaa hivyo bila kuuliza mahitaji halisi ya chuo na vifaa vingine kununuliwa kwa gharama kubwa zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles