Vigogo vyama vya siasa wakutanishwa kwa siri

0
726

Mwandishi wetu-Dar es Salaam

WAKATI wadau mbalimbali wakisema kuna umuhimu wa kuwapo mjadala wa taifa kuhusu  hali ya nchi, Taasisi ya Mwalimu Nyerere imeamua kukutanisha vyama vyote vya siasa nchini kujadili mustakabali wa taifa.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo gazeti hili limeziona, tangu mapema Agosti mwaka huu, taasisi hiyo imeandaa mikutano kadhaa iliyoshirikisha viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa.

Nyaraka hizo zinasema leo viongozi wakuu wa vyama vyote wanakusanyika  Dar es Salaam kwa majadiliano.

Mwenyekiti wa Wakfu wa Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku, alipoulizwa jana  alithibitisha mkutano huo  upo   lakini hakutaka kuuzungumzia kwa undani.

Alisema baada ya kumalizika mkutano huo ndipo watakapowasiliana na vyombo vya habari  kueleza  mambo yatakayojadiliwa  na makubaliano yatakayofikiwa.

“Kutokana na mambo yanayoendelea na hasa mazingira ya mkutano wenyewe, tunaomba muwe na subira kidogo.

“Tutawaita na kuwaeleza yaliyojiri baada ya kumaliza mkutano, ninaomba sana muwe na subira,” alisema.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo, sababu ya mkutano huo ni kutekeleza mpango wa amani na utatuzi wa migogoro nchini.

Awamu ya kwanza ya mpango huo kwa taasisi hiyo, ulianza mwaka 2017 na kukamilika Februari 2018.

Mpango huo  ulijikita kwenye makundi ya wakula na wafugaji na awamu ya pili inalenga wanasiasa.

Katika awamu hiyo ya pili, tayari taasisi hiyo imezungumza na viongozi mbalimbali wakiwamo Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru All na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu.

Wengine ni  Jaji Mark Bomani, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula na Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo, vyama vya siasa katika awamu hiyo vimelengwa zaidi uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwakani  na Uchaguzi Mkuu 2020.

Mashauriano na viongozi

Nyaraka hizo zinaeleza kuwa  ushauriano na viongozi mbalimbali ambao umekwisha kufanyika umeonyesha   kuna dalili za katiba kutoheshimiwa.

Wengi walionyesha kutoridhishwa na uchaguzi mdogo unavyoendeshwa, matamko ya viongozi ikiwamo kukataza mikutano ya hadhara na wakuu wa wilaya na mikoa kuweka watu ndani bila sababu za msingi.

Pia walieleza  kupungua   uvumilivu wa siasa na demokrasia za vyama vingi, huku wakitoa mifano wa matamko  yanayotolewa na viongozi yakiwamo yaliyodai ifikapo 2020 kutakuwa hakuna vyama vya upinzani, wakidai hali hiyo siyo nzuri.

Walidai pia kuwa kwa sasa viongozi wa vyama vyote nchini wanajadili zaidi vyeo badala ya masuala muhimu ya taifa.

Kuhusu mikutano ya awali ambayo ilikutanisha wadau  wa vyama mbalimbali na taasisi hiyo, wengi walionyesha kuwa hivi sasa kuna woga na hofu ya kudadisi.

Washiriki wa mikutano hiyo walieleza  kuwa hivi sasa wananchi wamekuwa waoga kudadisi na kukosoa   mambo yanapofanywa kinyume na matarajio yao.

Katika kikao kilichofanyika Agosti 16, baadhi ya viongozi hao walizungumzia suala la viongozi mbalimbali kuhama vyama vyao na kujiunga na CCM kwa madai ya kuunga mkono mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano.

Baadhi ya viongozi hao walidai hali hiyo inasababisha kutumika  fedha nyingi ilihali kuna matatizo mengi ya kufanyia kazi katika jamii ikiwamo kutokomeza umasikini, maradhi na ujinga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here