27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

VIFO VYA WAJAWAZITO, WATOTO VYAPAMBA MOTO DODOMA

Na Amina Omari, aliyekuwa Dodoma

LICHA ya Serikali kutangaza mpango wa maendeleo ya afya ya msingi 2007 hadi 2017 ambao umelenga kupunguza vifo vya wajawazito 578 hadi kufikia 175 kwa kila kizazi hai 100,000 lakini hali bado ni mbaya.

Mpango huo pia ulilenga kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka 112 hadi kufikia 45 na kuongeza idadi ya wajawazito  anaohudumia na wahudumu wa afya wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha kutoka asilimia 46 hadi 88.

Utekelezaji wa mpango huo umesaidia kuongeza vituo vya kutolea huduma za afya karibu na makazi ya wananchi hususani maeneo ya vijijini,  tofauti na miaka ya nyumba ambapo ilimlazimu mgonjwa kutembea umbali mrefu kufuata huduma.

Licha ya mikakati na mipango mizuri iliyopo, kumekuwapo changamoto ya vifo vya wajawazito pamoja na watoto chini ya miaka mitano.

Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa mikoa ambayo inakabiliwa na idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na uzazi huku vingi vikisababishwa na uhaba wa miundombinu pamoja na uhaba wa waatalamu wa afya.

Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto mkoani humo, Mary Shadrack anasema takwimu za vifo vya watoto wakati wa kujifungua imeongezeka kutoka  487 mwaka 2015 hadi kufikia 500 mwaka jana.

Anasema kuwa takwimu hizo zimetokana na jumla ya wajawazito 50,000 hadi 75,000 kwa mwaka ambao waliweza kurekodiwa kufika katika vituo vya afya kwa ajili ya kupata huduma.

Sababu nyingine ni wajawazito kwenda kwa wakunga wa jadi badala ya hospitali au vituo vya afya hali inayosababisha kufikishwa kwenye vituo vya kutolea huduma wakiwa katika hali mbaya hatimaye kupoteza maisha huku wengine wakipasuka mifuko ya uzazi na kupata ugumba.

“Licha ya takwimu hizo lakini kuna wastani wa wanawake zaidi ya 60 hadi 65 ambao hujifungulia nyumbani kwa wakunga wa jadi na wengine kwa waganga wa kienyeji,” anasema.

Anataja wilaya zinazoongoza kwa wajawazito kuwatumia wakunga na waganga wa jadi kuongeza uchungu wa kujifungua ni pamoja na Chamwino, Bahi na

Chemba ambapo kwa mwaka jana pekee wanawake wawili walifariki na wengine mifuko ya uzazi ilipasuka hali iliyowalazimu wataalam wa afya kuwaondoa vizazi.

Anasema kukosa maadili kwa baadhi ya watumishi wa afya pia huchangia vifo kwa wajawazito.

Mratibu huyo anasema ili kupunguza vifo hivyo wameamua kusogeza huduma ya upasuaji wa dharura katika baadhi ya maeneo.

Anasema pamoja na mambo mengine wameanza kuelimisha

watu kuhusu madhara ya kujifungulia nyumbani ili kumaliza kabisa tatizo hili.

Anasema elimu hiyo kwa kiasi fulani imesaidia kuleta hamasa kwa jamii hasa wajawazito kuhudhuria kliniki mapema wakiambatana na wenza wao.

“Wilaya za Kongwa na Mpwapwa ndio zimeonekana kuwa na mwitikio mkubwa

wa wajawazito kuhudhuria kliniki wakiwa na wenza wao ikilinganishwa na wilaya za Bahi, Kondoa, Chemba, Dodoma mjini, Dodoma vijijini

na Chamwino,” anabainisha Shadrack.

Anataja mikakati mingine kuwa ni kupeleka wahudumu wa afya katika maeneo ambayo yanakabiliwa na changamoto ya vifo vya wajawazito na watoto.

“Kuna maeneo mengine vituo vya afya vinavifaa vyote lakini changamoto iliyokuwapo ni ukosefu wa wahudumu ambao wataweza kutumia vifaa hivyo,” anasema.

Mmoja wa wananchi wanaoishi katika eneo la Chinangali Marium Ali anakiri kuwapo kwa baadhi ya wajawazito kuhudumiwa na waganga wa jadi sababu ikiwa ni umbali wa vituo vya afya.

Naye Atanasia Mapunda mkazi wa Makuru, anasema licha ya elimu ya afya kufika hadi kwa wananchi, bado wananchi wamekuwa wakiendelea kutumia dawa za kuongeza uchungu kwa kificho.

Anasema wakati mwingine dawa hizo zimekuwa zikiwasaidia kuwahi kujifungua pale zinapotumiwa kulingana na vipimo vinavyoelekezwa na waganga, lakini wakizidisha husababisha madhara makubwa.

“Si kwamba hatutumii dawa za mitishamba kwa ajili ya kuongeza uchungu… wanaopata matatizo ni wale wanaokiuka maagizo waliyopewa kwa kuongeza kwa makusudi au kwa bahati mbaya,” anasema Mapunda.

Anawashauri wananchi hususani wajawazito kuona umuhimu wa kuwahi kuhudhuria kliniki kwa wakati ili kuweza kupata

ushauri wa kitaalamu kwa wakati badala ya kuchelewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles