25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

VIFO VYA WAJAWAZITO BADO VINAITESA TANZANIA

Kina mama wakisubiri huduma ya afya hospitalini

Na Editha Karlo, Kigoma

MWANAMKE kupata ujauzito ni kitendo cha furaha katika familia yake na hata kwa jamii nzima inayomzunguka, lakini furaha hii inaweza kugeuka majonzi pale inapotokea amepoteza maisha kabla au baada ya kujifungua.

Ripoti mpya ya jamii na afya (DHS) ya ofisi ya Taifa ya takwimu kwa mwaka 2015/2016 inaonesha kuwa kuna vifo 556 vya uzazi katika kila vizazi hai 100,000.

Kiwango hicho ni kikubwa kuliko kile cha mwaka 2012 ambapo wanawake 432 walikufa kwa matatizo ya uzazi. Hata hivyo idadi hiyo ni ndogo ukilinganisha na ya mwaka 2004/05 iliyoonesha wanawake 578 hupoteza maisha kwa matatizo ya uzazi.

Mwaka 2010/11 ripoti ilionesha kuna vifo 454. Ripoti hii ni ya sita kufanyika nchini ambapo ya kwanza ilikuwa mwaka 1991/92.

Emiliana Joseph (38) mkazi wa eneo la ujiji katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, anasema hivi sasa wajawazito wengi wanakuwa na shaka kwa kuofia kufariki.

“Siku hizi ukiona umebeba mimba hapo ujue ni kufa na kupona kwa sababu lolote linaweza kutokea kati ya mama au mtoto, wakati mwingine wote japo kuwa si mara zote,”anasema mama huyo.

Anasema maeneo mengi huduma za afya ni duni hasa kwa upande wa wajawazito.

“Naiomba serekaki iboreshe huduma ya afya hasa kwa wajawazito, walipe uzito unaostahili suala hili,” anasema.

Naye Mariam Chuma (72) anasema kila mwanamke ana haki ya kuishi na kupata mtoto, lakini sasa hivi uzazi umekuwa ni jambo la kuogopwa.

“Enzi zetu sisi, mwanamke akiwa mjamzito tulikuwa tunasema si ugonjwa lakini sasa hivi mimba ni ugonjwa usipokuwa makini unaweza kupoteza maisha.

“Ombi langu kwa serekali waweke vifaa muhimu vya kujifungulia katika vituo vya afya, pia elimu kuhusu masuala ya uzazi itolewe kwa wazi hasa kwa mabinti waliopevuka ili kuepuka mimba zisizotarajiwa wakapata matatizo wakati wa kujifungua,”anasema.

Rais wa Shirika la Afya la Pathfinder, Louis Quiam anasema ni vyema wanawake wakapewa nafasi ya kupanga uzazi ili kujihakikishia usalama na kuepuka vifo wakati wa kujifungua.

Anasema shirika la Pathfinder linatoa huduma za afya na vifaa tiba ili kupunguza hatari ya wajawazito kufariki wakati wa kujifungua.

“Sisi tunatoa elimu ya uzazi kwa vijana kwa mfano tumeanzisha klabu  mkoani  Kigoma zinazojumuisha vijana waliojifungua katika umri mdogo kurudi shuleni na wengine kujizuia na kupata ujauzito usiotarajiwa,”anasema.

Anasema njia za uzazi wa mpango ni muhimu zaidi katika kupunguza vifo hivyo, kwamba kitendo cha wanawake 9000 kufariki kila mwaka wakati wa kujifungua hilo ni zaidi ya janga.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa mimba za utotoni ni chanzo kingine cha vifo vya wajawazito.

WHO inaeleza ongezeko la vifo linaweza kuirudisha nyuma Tanzania katika jitihada za kupunguza vifo kwa wajawazito.

Mganga wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Anna Kalinda anasema hivi sasa asilimia 90 ya wanawake wanaopata ujauzito nchini wamekuwa wakihudhuria kliniki katika vituo, zahanati au hospitali kwa ajili ya kupima maendeleo ya mimba zao, lakini cha ajabu wanaorudi kujifungulia katika vituo hivyo ni asilimia 45 tu.

Anasema bado kuna wajawazito wanaojifungulia nyumbani, hali hii inaweza kusababisha vifo kwa wazazi au vichanga vyao, pindi linapotokea tatizo linalohitaji tiba maalumu na ya haraka sababu wanaowapatia huduma majumbani wengi wao si wataalamu wa afya.

“Akina mama wanaojifungulia nyumbani na kufariki mara nyingi taarifa zao hazifiki katika vituo vya afya, hivyo nawaomba wajawazito wote wajifungulie katika vituo vya afya na hospitalini,”anasema.

Kuhusu dhana na fikra potofu ya madhara ya njia za uzazi wa mpango, anasema faida ni nyingi kuliko wengi wanavyofikiria.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dk. Paul Chawote anasema ongezeko la vifo vya wajawazito kwa Mkoa wa Kigoma ni changamoto inayohitaji ufumbuzi wa haraka.

Anazitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na upungufu wa watumishi wa afya kwa asilimia 65 na umbali wa vituo vya afya, jambo linalosababisha baadhi ya wajawazito kujifungulia njiani.

Changamoto nyingine ni uhaba wa dawa, vifaa tiba na uwepo wa vituo vichache vya kutolea huduma.

Anasema Serekali imekuwa ikifanya juhudi kubwa kuhakikisha changamoto zote zinakwisha na kuboresha huduma kwa wajawazito, wao wamejiwekea mikakati ya kukabiliana na suala hilo.

Anaitaja mikakati hiyo kuwa ni kuhakikisha watumishi katika sekta ya afya wanaongezeka, uwapo wa uhakika wa damu salama katika banki ya damu, utoaji wa elimu kwa wajawazito kuhudhuria kiliniki mapema na kujifungulia katika vituo vya afya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles