24.3 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Vicoba vyakwamisha muswada bungeni

Mwandishi Wetu -Dodoma


MUSWADA wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha wa mwaka 2018 uliowasilishwa bungeni kwa hati ya dharura Novemba 6, mwaka huu, umeshindwa kusomwa kwa mara ya pili jana, huku kifungu kinachohusu vicoba kikitajwa kuwa moja ya eneo lililosababisha mvutano.

Tangu kusomwa muswada huo bungeni kwa mara ya kwanza Novemba 6, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imekuwa ikikaa kuujadili.

Kamati hiyo ambayo mara nyingine imekuwa ikikaa hadi usiku, imeshakutana pia na wadau mbalimbali kujadili muswada huo.

Novemba 5, Spika wa Bunge, Job Ndugai alizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa 13 wa Bunge la 11, na alisema pamoja na mambo mingine itawasilishwa miswada na mmoja kati yake utawasilishwa kwa hati ya dharura.

Alisema miswada hiyo ni pamoja na Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018, Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 4 wa Mwaka 2018, Muswada wa Hali ya Hewa wa Mwaka 2018 na Muswada wa Mamlaka ya Usimamizi wa Nchi Kavu.

Alisema katika kikao hiki kutakuwa na Muswada wa Sekta Ndogo ya Fedha wa Mwaka 2018 (Micro Finance) ambao utapitishwa kwa hati ya dharura.

“Kama inavyotakiwa na kanuni kuwa kupitisha muswada wa namna hii lazima Kamati ya Uongozi ipitishe, baada ya kupokea hati ya dharura kutoka kwa Rais, leo Kamati ya Uongozi ilikaa na kukubali kuupitisha muswada huu kwa hati ya dharura na utajadiliwa kwa siku mbili na kupita kwenye hatua zote,” alisema Ndugai.

 

KUKWAMA

Muswada huo ulitarajiwa kusomwa kwa mara ya pili jana, lakini baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson alitangaza kuahirisha kikao hicho hadi leo asubuhi.

MTANZANIA iliwatafuta baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bajeti ambao walisema muswada huo haujamalizika kujadiliwa na kamati hiyo.

“Kuna mambo makubwa mawili ambayo yanaleta mvutano, kwanza katika kutungwa kwa muswada huu Zanzibar haijajumuishwa, sasa wajumbe wanasema hakuna Tanzania bila Zanzibar.

“Lakini pia kuna suala la vicoba, watu kukopeshana hili nalo limeleta ukakasi, hivi vicoba watu wanakopesha siyo kwa misingi ya kibiashara, wapo wengine wanafanya hivyo kwa sababu ya ada za shule.

“Ukiacha lipite kama ilivyo utakuja kushangaa hata michango ya harusi inajumuishwa huko,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo.

Alisema muswada huo unabana hata watu binafsi wanaokopeshana jambo alilosema ni hatari zaidi.

“Kwa lugha waliyoiweka ina maana hata wewe ukija ili mimi mtu binafsi nikukopeshe inaleta shida, sasa hii haiwezekani, wao wameona benki hakuna hela sasa wakajua kwamba zitakuwa huku kwenye vicoba,” alisema.

Alisema sheria hiyo ikipita kama ilivyo, hata makundi ya Whatsapp ambayo watu huhamasishana ili kuchangia jambo fulani yatabanwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, George Simbachawene alipotafutwa kuzungumzia mambo yanayobishaniwa katika kamati hiyo na kusababisha muswada huo kutosomwa jana, alisema; “mimi ni mwenyekiti, unataka vipi nikwambie mambo yanayobishaniwa tu? Subiri tumalize nitasema, siwezi kusema vitu nusunusu.”

Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alipoulizwa sababu za muswada huo kutosomwa kwa mara ya pili alisema; “bado hatujamalizana (na kamati), leo (jana) saa saba tutakaa tena, tukimaliza naweza kuwa na cha kuzungumza.”

Mbunge mwingine ambaye si mjumbe wa Kamati  ya Bajeti lakini amekuwa akihudhuria vikao vyake, alisema; “hii wakipitisha hata hiyo asilimia 10 ya vijana na wanawake tunazosema zitengwe na halmashauri itakuwa haina maana.”

 

MUSWADA

Lengo la muswada huo ni kutoa leseni, kudhibiti, kufuatilia na kusimamia biashara ya huduma ndogo za fedha.

“Muswada huu umeweka madaraja ya taasisi za huduma ndogo za fedha na utaratibu wa kuhama kutoka daraja moja hadi jingine.

“Aidha muswada huu unaipa mamlaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kusimamia sekta ndogo ya fedha, kuweka utaratibu wa kisheria wa kumlinda mlaji na utaratibu wa kushiriki katika mfumo wa ubadilishanaji wa taarifa za wakopaji,” inasema sehemu ya taarifa ya muswada huo iliyo kwenye tovuti ya Bunge.

Sehemu ya nne ya muswada huo inahusu masuala ya utoaji leseni na usajili wa watoa huduma ndogo za fedha.

“Sehemu hii pia inaweka katazo kwa mtu au taasisi yoyote kujihusisha na biashara ya huduma ndogo za fedha bila kuwa na leseni au usajili.

Aidha sehemu hii inaainisha utaratibu wa taasisi ya watoa huduma ndogo za fedha zikiwemo taasisi za nje kuomba leseni na kusajiliwa. Sehemu hii pia inaainisha utaratibu wa kusitisha au kufuta leseni na kukata rufaa,” inasema sehemu ya taarifa ya muswada huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles