25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Viboko vyatembezwa makaburini

Jiji la Mwanza
Jiji la Mwanza

NA VICTOR BARIETY, SENGEREMA

WAJUKUU wa marehemu Sabina Ngalu (77) wa jijini Mwanza, wamecharazwa bakora na watoto wa marehemu baada ya kung’ang’ania kaburini wakitaka kupewa fedha.

Tukio hilo la aina yake lilitokea katika Kitongoji cha Nyamwanza, Kata ya Sima, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza juzi muda mfupi baada ya mwili wa marehemu kuwasili eneo la mazishi ukitokea Kanisa la Roman Catholic Parokia ya Yesu Kirsto Mfalme la mjini Sengerema.

Chanzo cha wajukuu hao zaidi ya 10 kuchacharazwa bakora, ni kung’ang’ania ndani ya kaburi lililokuwa limeandaliwa kwa ajili ya kuuhifadhi mwili wa marehemu.

Wajukuu hao walitaka wapewe ng’ombe mmoja au Sh 100,000 kama zinavyotaka mila za kabila la Kisukuma.

Jambo hilo lilipingwa na baadhi ya wanandugu waliodai mila hizo zilikwishapitwa na wakati na kuwataka wajukuu hao kutoka kaburini ili taratibu za mazishi ziendelee.

Hata hivyo, wajukuu hao waligoma kutoka ndani ya kaburi hilo huku wakisema wapo tayari kufa, lakini si kutoka bila kupatiwa ng’ombe mmoja au kiasi hicho cha fedha.

Kitendo cha wajukuu hao kugoma kutoka ndani ya kaburi hilo, kilimchefua Padre Nicodemus Mayala ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Yesu Kristo Mfalme Sengerema, na kuondoka eneo hilo huku akitaarifu polisi kuhusu vurugu hizo.

Kufuatia hali hiyo, kaka wa marehemu, Enosi Ngalu, aliyeonekana kukerwa na kitendo hicho, alitafuta fimbo ndefu kisha kutinga eneo hilo na kuanza kutembeza mkong’oto kwa wajukuu hao waliokuwa ndani ya kaburi.

Kitendo hicho kilizidisha hasira kwa wajukuu hao ambao wakiwa ndani ya kaburi walianza kujibu mapigo kwa kumrushia mchanga.

WAOMBOLEZAJI WAKUBALI YAISHE

Kufuatia hali hiyo, mmoja wa waombolezaji aliamua kuwapa wajukuu hao kiasi hicho cha fedha ndipo walipotoka ndani ya kaburi hilo.

PADRE AGOMA KUONGOZA IBAADA YA MAZISHI

Baada ya wajukuu hao kutoka ndani ya kaburi, Padre Mayala ambaye wakati huo alikuwa akizungumza na baadhi ya ndugu wa marehemu, aligoma kurejea eneo la makaburi kuongoza ibada ya mazishi.

“Hata kama wameshatoka, siwezi kurudi tena huko kuongoza ibada ya mazishi maana hili jambo limefanywa kinyume na taratibu za sisi Wakristo, haya ni mambo ya kipagani, yalipaswa yafanywe kipagani,” alisema Padre Mayala.

Baada ya mazungumzo ya muda mrefu, Padre Mayala aliwataka wajukuu hao kurudisha pesa waliyochukua na kuwataka radhi wanamtaa huo na ndipo anaweza kurudi eneo la kaburi kuongoza ibada ya mazishi na kwamba kinyume na hapo asingeendesha ibada hiyo.

Baada ya msimamo huo, wajukuu hao waliitwa mbele ya Padre na wanamtaa kisha wakaomba msamaha na kurudisha fedha walizokuwa wamepewa.

POLISI
Askari polisi wanne kutoka kituo cha Sengerema wakiwa na bunduki na mabomu ya machozi, walifika eneo hilo kufuatia wito wa Padre Mayala, lakini hawakuchukua hatuab yoyote baada ya kukuta hali ni shwari.

VURUGU ZAHAMIA NYUMBANI

Baadaa ya kutoka makaburini, wajukuu waliwahi nyumbani kwa marehemu na kuficha chakula na vyombo vya kupakulia wakidai warudishiwe fedha walizokuwa wamezirudisha.

“Mmetucharaza bakora na fedha zetu mkatunyang’anya, sasa tuko tayari kupigwa hadi mtuue, lakini chakula hakitoki hapa au la sivyo mturudishie pesa yetu,” alisema mmoja wa wajukuu hao, Enos Ntilaga.

Baada ya hali hiyo, mmoja wa wafiwa alitoa fedha na kuwapa wajukuu hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles