Imechapishwa: Tue, Oct 10th, 2017

VANESSA MDEE, ASLAY WAITIKISA IRINGA FIESTA

Na MWANDISHI WETU

MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Vanessa Mdee, ameacha gumzo kwa wakazi wa mkoani Iringa waliofurika katika Uwanja wa Samora, kushuhudia tamasha la burudani la Tigo Fiesta 2017 lililofanyika juzi katika Uwanja wa Samora mjini hapa.

Vanessa ambaye ni miongoni mwa wasanii waliopanda katika jukwaa la Tigo Fiesta mkoani hapa, aliimba nyimbo zake mbalimbali ambazo mashabiki wake walikuwa wakiimba huku wakishangilia kwa shangwe.

Katika tamasha hilo, Vanessa Mdee, aliimba nyimbo zake mbalimbali ikiwemo ile ya Kisela, Niroge na Cash Madame, ambazo ziliwapagawisha vilivyo mashabiki waliohudhuria katika uwanja huo.

Msanii mwingine ambaye pia alikonga nyimbo za wakazi wa Iringa alikuwa ni Aslay ambaye aliimba nyimbo zake kama Natamba, Angekuona, Pusha na Mhudumu.

Wasanii wengine waliopanda jukwaani kutoa burudani katika Tigo Fiesta Iringa ni Ben Pol, Maua Sama, Mr. Blue, Chege, Darassa, Joh Makini, Jux, Nandy, Ommy Dimpoz na Rostam.

Mgeni rasmi katika tamasha alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela, ambaye alipanda jukwaani huku akionyesha uwezo wake wa kuimba huku akishangiliwa.

Hadi sasa Tigo Fiesta 2017 imezuru mikoa ya Arusha, Kahama, Musoma, Mwanza, Tabora, Njombe, Dodoma, huku pia ikitarajia kufika Songea, Sumbawanga, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Mtwara na kuhitimishwa Dar es Salaam.

Meneja Masoko wa Kampuni ya Tigo ambao ni wadhamini wa tamasha hilo, William Mpinga, alisema Fiesta ya mwaka huu itahusisha wasanii ambao watapendekezwa na mashabiki wenyewe kutoka katika mikoa husika kama ilivyo kauli mbiu ya ‘Tumekusoma’ ambayo inajali vile wateja wao wanavyohitaji.

Alisema pia kutakuwa na punguzo la bei ya tiketi kwa asilimia 10 kwa mashabiki watakaonunua kupitia Tigopesa na kwamba hata walio kwenye mitandao tofauti wanaweza kununua tiketi hizo kupitia nambari 0678 88 88 88.

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

VANESSA MDEE, ASLAY WAITIKISA IRINGA FIESTA