23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

UZAZI TANZANIA: SAFARI YENYE MILIMA NA MABONDE

Wakunga wakionesha jinsi ya kumuhudumia mama anayetokwa na damu baada ya kujifungua wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani.
Na VERONICA ROMWALD – ALIYEKUWA MOROGORO   |

Mei 5, mwaka huu Tanzania iliungana na mataifa mengine duniani kusherehekea Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani ambayo kwa mwaka huu yalipewa Kauli mbiu isemayo ‘Wakunga ni Chachu katika Utoaji Huduma bora kwa mama na mtoto’.

Tanzania iliadhimisha siku hii ya pekee, maadhimisho hayo yalifanyika huko mkoani Morogoro katika viwanja vya sabasaba.

Upo msemo wa wahenga usemao, usitukane wakunga na uzazi ungalipo, msemo huu unalenga kuhamasisha jamii kumthamini mkunga kulingana na nafasi yake nyeti aliyonayo.

Mkunga ni mtu muhimu mno katika kusaidia kufanikisha kuanza kwa safari ya mwanadamu duniani, huhitajika katika kusaidia na kufuatilia hali ya mama tangu anapogundulika kuwa mjamzito, kipindi cha ujauzito na hadi kujifungua.

Hata baada ya mama kujifungua, mkunga huendelea kufuatilia hali yake na mtoto au watoto waliozaliwa hadi wanapofikisha kipindi cha umri wa miaka mitano.

Zamani mabibi zetu walilazimika kujifungua kwa msaada wa wakunga wa jadi ingawa hadi sasa bado zipo jamii ambazo hujifungua kwa wakunga hao. Hata hivyo, kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia wengi leo hii wanajifungua kwa msaada wa wakunga wataalamu.

Pamoja na umuhimu wao, baadhi ya wakunga kwa miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakilalamikiwa na wananchi wakiwamo wajawazito, kwamba wanatenda kazi bila kuzingatia misingi ya taaluma yao.

Wapo ambao wanatuhumiwa kuwatolea lugha zisizofaa wajawazito wakati wanapokuwa wakiwahudumia huko kliniki au katika vyumba vya kujifungua (labour). 

Simulizi ya Frida

Frida Eliud Mkazi wa Morogoro ni mama wa watoto wawili, anasema mtoto wake wa kwanza alijifungulia katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro mwaka 1998.

Anasema wakati wa ujauzito wake huo wa kwanza alipatwa wasiwasi mwingi wa kuanza kuhudhuria kliniki hasa alipokuwa akikumbuka simulizi alizosimuliwa na wanawake wenzake kuhusu lugha zinazotolewa huko kliniki.

“Walikuwa wakinisimulia jinsi walivyopokelewa katika hospitali walizokwenda, kwamba baadhi ya wakunga na wauguzi wanatoa lugha za kuudhi. Lakini ilifika mahali nikasema wacha niende tu kwa sababu sina jinsi na lazima nifuatilie maendeleo ya hali yangu na mtoto wangu aliye tumboni.

“Nilianza kuhudhuria kliniki, sitasahau siku ile ya kwanza, muuguzi aliyenipokea hakuwa na lugha nzuri, hata siku nilipokwenda kujifungua mkunga aliyenisaidia naye hakuwa na lugha nzuri, kusema ukweli wapo wanaofanya vema lakini kuna wengine wanawaangusha kwa kufanya yasiyofaa.

“Kila nilipomuita aje anisaidie alikuwa akiniambia nisimsumbue, kwamba kuna wengine pia waliokuwa wakihitaji kusaidiwa na yeye hakuwa na uwezo wa kujigawa atusaidie wote.

“Nilihangaika usiku kucha sikufanikiwa kujifungua hadi ilipofika asubuhi, mume wangu alikuja nikamsimulia kilichokuwa kikiendelea.

“Alisikitika mno lakini hakuwa na jinsi, ilibidi wasubiri hadi nilipojifungua majira ya saa nne hivi, tukarudi nyumban,” anasema.

Anasema kuwa ujauzito wake wa pili akaamua kwenda tena hospitali nyingine ya serikali, akapokelewa na mkunga wa kiume, nilichelewa kujifungua lakini aliendelea kunihudumia kwa upendo na kwa kunithamini mno.

Anasema alikuwa akimtia moyo na kumtaka asiogope, kwamba nitajifungua salama. 

Mama mwingine

Mariam James (50) Mkazi wa Morogoro Mjini ni mama wa watoto watatu, anasema awali alikuwa akiishi jijini Dar es Salaam eneo la Sinza kwa Remmy.

Anasema alipojihisi kuwa ni mjamzito, mwaka 1990 aliamua kufanya uchunguzi hospitali ipi itamfaa kwa huduma ya kliniki.

“Wanawake wenzangu walishanisimulia changamoto walizokumbana nazo katika hospitali mbalimbali, lakini nikasema kwa kuwa ninahisi ni mjamzito nifanye uchunguzi kwanza hospitali ipi itanifaa nianze kliniki.

“Basi nilikwenda kwanza Hospitali ya Tandale, nikakaa kwenye benchi nikaangalia namna ambavyo wauguzi na wakunga walivyokuwa wakipokea wagonjwa na kuzungumza nao,” anasema.

Anasema hakuridhishwa na watumishi wa hospitali hiyo, hivyo aliondoka tena hadi Hospitali ya Mwananyamala akakaa kwenye benchi na kufanya tena uchunguzi wake.

“Hapo napo sikuridhika na huduma, nikaondoka hadi Hospitali ya Mnazi Mmoja nikafanya hivyo hivyo, kidogo hapo niliridhishwa na huduma, kulikuwa na wauguzi na wakunga wenye umri wa utu uzima tofauti na kule nilipokwenda awali, walikuwa wakipokea watu kwa kauli nzuri mno.

“Lakini nikasema ngoja niende na Hospitali ya Taifa Muhimbili nikaangalie huduma zilivyo, huko sikuridhishwa, nikaamua kurudi Mnazi Mmoja wale watumishi wakaniambia muda ulikuwa umekwisha, ilikuwa siku ya Ijumaa basi wakanishauri niwahi mapema asubuhi nianze kliniki,” anasema.

Mariam anasema aliondoka akiwa na furaha na kwamba aliwahi mapema Jumatatu hospitalini hapo na kuanza kliniki ya uzazi.

“Wale watumishi walikuwa wakiongea nasi kwa lugha nzuri, walikuwa wanahudumia kwa upendo, wanafariji na wanabembelea mtu unajisikia amani muda wote tofauti na wale watumishi wa hospitali zingine ambazo nilikwenda walikuwa wakizungumza vibaya na wagonjwa.

“Niliendelea kuhudhuria kliniki Mnazi Mmoja lakini nilipofikia kujifungua walinishauri nitafute hospitali nyingine kwa sababu wakati ule pale walikuwa hawana huduma ya kujifungua bali ya kliniki tu.

“Ingawa nilitamani kujifungulia pale lakini sikuwa na jinsi ilibidi nirudi Mwananyamala nikajifungulia hapo, kusema ukweli jinsi wauguzi na wakunga wenye umri wa utu uzima walivyokuwa wanahudumia ilikuwa tofauti kabisa na wale wenye umri wa ujana wakati huo,” anabainisha.

Anasema hadi sasa anaona kuna tofauti kubwa kati ya watumishi wenye umri mkubwa jinsi wanavyohudumia wagonjwa na wale wenye umri mdogo.

“Wenye umri mkubwa wana hudumia kwa upendo zaidi kuliko hawa vijana, kwa msingi huo, ikiwa inawezekana basi naishauri serikali iangalie hii kazi ya uuguzi na ukunga ifanywe na watu wenye umri wa utu uzima kuliko vijana,” anashauri.

 Ukweli wa mambo

Pamoja na umuhimu wa kada hii katika sekta ya afya, kwa muda mrefu sasa yamekuwapo malalamiko kutoka kwa jamii wakidai baadhi yao wamekuwa wakizungumza lugha zisizofaa (kejeli au matusi) kwa wajawazito hasa wanapokwenda kujifungua.

Hivi karibuni, tulishuhudia jinsi ambavyo ‘sekeseke’ hilo lilipamba moto kiasi cha baadhi ya viongozi wa serikali kuonekana waziwazi wakiwachukulia hatua wauguzi na wakunga waliodaiwa kutoa lugha zisizofaa kwa wagonjwa kwa kuwaweka rumande.

Hata hivyo, ililazimu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoa tamko la kuwataka viongozi wa serikali kuziachia mamlaka zinazosimamia maadili ya kitaaluma kuwachukulia hatua watumishi hao kwa kufuata misingi ya sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Pamoja na hayo, inadaiwa watumishi wengi wa kike wa kada hizo ndiyo ‘vinara’ wa kutoa lugha chafu kwa wajawazito tangu wanapohudhuria kliniki na hadi kipindi cha kujifungua kuliko watumishi wa jinsia ya kiume.

Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA). Feddy Mwanga, anakiri kwamba wamekuwa wakipokea malalamiko kutoka kwa jamii dhidi ya baadhi ya wakunga.

“Wapo wanaotuhumiwa kutoa lugha zisizofaa na tunapopokea malalamiko tunafuatilia kwa ukaribu na ambaye anakutwa na hatia tunamchukulia hatua kwa mujibu wa sheria,” anabainisha. 

Utafiti wafichua mambo

Maurice Hiza ni Ofisa katika Idara ya Huduma na Ukunga wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, anasema waliamua kufanya uchunguzi wa kina juu ya malalamiko hayo.

“Tulipokea malalamiko mengi mno na tukaamua kufanya uchunguzi wetu wa kina ili kujua je, ni kweli au watu walikuwa wakieneza tu uvumi, baada ya uchunguzi wetu tulibaini ni kweli wapo baadhi ya wakunga ambao hutamka lugha zisizofaa wanapokuwa wakihudumia wateja,” anasema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubsya anasema wizara ina utaratibu maalum wa kushughulikia kero zinazowapata wafanyakazi wake.

Anasema taratibu hizo zinaendana na sheria za nchi na zimewekwa mahususi kuzishughulikia kero zozote ziwe zimesababishwa na mazingira ya kazi, wafanyakazi wenzao au watu wanaokuja kupata huduma.

“Mara nyingi tunaweza kuwa tunashughulika na watu wanaotoa huduma baada ya wafanyakazi kuja kutoa taarifa kwamba wamefanyiwa jambo fulani au mtu ameona mfanyakazi amefanyiwa jambo akatupa taarifa na sisi tunafuata utaratibu.

“Tunauliza mfanyakazi amefanyiwa jambo gani na lazima tumjue aliyefanya jambo husika, hatua hii imetusaidia mno kutatua kero mbalimbali za wafanyakazi, vile vile mahali pa kazi ni salama kwa sababu ya utaratibu tuliojiwekea wa ndugu, namna ya kuingia katika maeneo ya kazi hata wagonjwa wenyewe.

“Kwa hiyo, hatutegemei wakunga wanaweza kudharauliwa, kutukanwa na ndugu kwa mazingira ya kawaida ya kazi kwa sababu anaposhughulika na wajawazito kuna utaratibu wao ambao wanausimamia,” anasema.

Dk. Ulisubisya anasema hata hivyo, pamekuwa na malalamiko na mengi huyapokea kutoka kwa ndugu wa wagonjwa kulalamikia huduma zinazotolewa hasa kuhusu lugha.

“Hilo tumekuwa tukilishughulikia kwa kuhakikisha tunakuwa na huduma rafiki katika maeneo yote,” anabainisha.

 Wakunga wafunguka

Wakati jamii ikilalamika na kuwatuhumu baadhi ya wakunga kutotimiza wajibu wao kwa mujibu wa misingi ya taaluma yao.

Wakunga nao wamefunguka na kutoa yale yaliyo moyoni mwao ambapo hapa wanaeleza changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Akizungumza na MTANZANIA Mariam Japhet, Mkunga wa Hospitali ya Ulanga mkoani Morogoro, anasema amefanya kazi hiyo tangu mwaka 1990 na kwamba amekutana na mikasa mingi.

“Nakumbuka kuna siku nilipokea mjamzito ambaye mapigo yake ya moyo na ya mtoto yalionekana kushuka mno, nilimjulisha daktari aliyekuwa akimfanyia vipimo zaidi, yule mama alibaini mtoto alikuwa tayari amefariki dunia.

“Alipofanyiwa upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni, alikutwa na tatizo la kichwa kikubwa, basi ndugu aliyekuwa amekuja na mgonjwa alijulishwa lakini alipokuja mumewe hakuwasilisha vizuri maelezo yale aliyopatiwa,” anasema.

Anasema hali hiyo ilisababisha baba wa mtoto husika na baadhi ya ndugu kuanza kulalamika kuwa mtoto wao alikuwa amefariki kutokana na uzembe.

“Ikabidi tutumie ujasiri kumuita baba husika na kumuonesha ule mwili wa mtoto wake alipoangalia na kuona alikuwa na tatizo la kichwa kikubwa aliamini hakukuwa na uzembe uliokuwa umefanyika,” anasema.

Muuguzi mkunga mwandamizi, Agnes Mtawa ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa Msajili wa Baraza la Wakunga Tanzania anasema katika miaka zaidi ya 20 aliyohudumu katika fani hiyo amepitia mambo mengi.

“Katika hospitali niliyokuwa nasimamia, kuna siku aliletwa mjamzito ambaye alifikishwa akiwa amechoka mno na bahati mbaya mtoto alifariki tukiwa zamu ya usiku tutachukua kitenge chake tukamstiri mtoto.

“Ndugu walipokuja asubuhi wakabaini kitenge hakikuwepo wakadai kwamba kilikuwa kimeibiwa na wakunga tuliokuwa usiku ule, kwa haraka haraka tulikubaliana tulipe.

“Lakini tulifanya jitihada kuangalia kilienda wapi, tukakagua na kubaini kwamba tulimfungia mtoto baada ya kufariki dunia, ndugu walikuwa tayari wamekasirika hawakuwa na uchungu tena na kifo cha mtoto wao walikuwa na uchungu na kile kitenge.

“Kwa kawaida tulikubaliana kwamba mama akiletwa pale hospitalini (Muhimbili) kila kitu chake alichokuja nacho lazima kiandikwe anapoingia na anapotoka, na hatua hiyo ndiyo ilitusaidia kujua ukweli kwamba kitenge hakikupotea bali alifungiwa mtoto kumsitiri,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles