24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

UWEKEZAJI WA MUDA MREFU SAWA NA MBIO ZA MARATHON

Na ARODIA PETER-DAR ES SALAAM


UWEKEZAJI wa muda mrefu ni sawa na mbio za marathon. Hivi ndivyo tunavyoweza kusema kutokana na utekelezaji wake hufanyika kwa miaka kadhaa na katika mpango au mtiririko maalumu.

Kampuni ya Uwekezaji Tanzania ya UTT AMIS inaunga mkono dhana hii ambayo kwa zaidi ya miaka 10 imekuwa ikihamasisha umma kujikita katika uwekezaji kupitia mifuko yake mbalimbali.

Hadi kufikia mwaka 2015, UTT AMIS ilikuwa na jumla ya mifuko ya uwekezaji wa pamoja mitano

ijulikanayo kama; Umoja, Wekeza Maisha, Watoto, Kujikimu na Ukwasi huku ikisimamia mali zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 249 na wawekezaji zaidi ya 120,000.

Katika mahojiano maalumu na MTANZANIA, Mkurugenzi wa Masoko wa UTT AMIS, Daud Mbaga, anasema kampuni hiyo ni taasisi ya Serikali yenye uzoefu wa zaidi ya miaka 10 katika usimamizi wa mali kupitia mifuko ya uwekezaji wa pamoja, lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi kuwa na utamaduni na tabia ya kujiwekea akiba.

Shughuli zote za taasisi hiyo zinaratibiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Tanzania.

Mbaga anasema wataalamu wa mambo ya ushauri wa fedha na uwekezaji wanalinganisha kukimbia mbio ndefu za marathon na kupanga mipango ya muda mrefu ya kipato.

Wanatoa mfano kwamba lengo la mkimbiaji wa mbio za marathon au nusu marathon ni kukimbia kilomita 42 kwa mara moja.

“Kanuni na maandalizi ya mbio ndefu za marathon, mkimbiaji huanza taratibu, atakimbia kilomita 3 hadi 5 kila siku katika siku za mwanzo na kuendelea kuongeza umbali kwa asilimia 10 kila mwili unapozoea umbali husika.

“Katika mbio ndefu kuna msemo unasema hali inapokuwa ngumu, ugumu hutoweka. Katika nyakati fulani hii huweza kuwa kweli pia kwa wawekezaji wa muda mrefu.

“Tuangalie kwa kina kufanana huku kunavyoweza kuamsha ari na hamasa ya kuwekeza kwa muda mrefu iwe kwenye mifuko ya pamoja au sehemu nyinginezo,” anasema Mbaga.

Anasema kitu muhimu zaidi cha kwanza kwa mwekezaji ni kuweka malengo ya muda mrefu ya kifedha.

Kwamba mwekezaji anatakiwa kuanza kuwekeza kiasi kidogo kila mwezi na kuongeza uwekezaji wake kila kipato chake kinavyoongezeka.

Mkurugenzi huyo wa Masoko anasema ni makosa makubwa kufanya uwekezaji bila malengo.

Malengo hayo yanaweza kuwa ya kustaafu, elimu ya watoto, kununua nyumba, kuanzisha mradi, kuoa/kuolewa.

Mbaga anasema mfumo wa kuwekeza kwa awamu kwenye mifuko ya pamoja kama vile Wekeza Maisha unaoendeshwa na UTT AMIS, ni mfano mzuri ambapo mwekezaji anaweza kuanza kuwekeza kwa kima cha chini cha Sh 8,340 kwa mwezi na kuongeza kadiri kipato kinavyoongezeka.
 

Akijikita zaidi katika mifano ya mbio za marathon, anasema pale mkimbiaji anapozoea mazingira anayofanyia mazoezi, mkufunzi wake hulazimika kumbadilishia mazingira. Kwamba anaweza kutoka katika mazingira ya tambarale na kupelekwa kwenye vilima na miteremko au kwenye mchanga.

Anasema hali kadhalika, washauri wa kifedha na uwekezaji humshauri mwekezaji kuanza kuwekeza kwenye bidhaa rahisi, mfano mifuko ya uwekezaji wa pamoja ambayo ni rahisi kuielewa.

Mwekezaji akianza kuzoea mfuko unavyofanya kazi na kupata imani, mshauri humuelekeza kuwekeza kwenye sehemu nyinginge au mifuko ambayo ni mikubwa na yenye hatari kidogo kwenye uwekezaji.
 

Hata hivyo, kutokana na  vikwazo mbalimbali mwekezaji mwenye lengo la kukuza fedha zake kwa muda mrefu anatakiwa asiyumbishwe na kupanda na kushuka kutokana na mabadiliko ya soko.

Kwa mfano mwekezaji anatakiwa kuendelea kubaki kwenye lengo lake hata katika kipindi ambacho hali ya  soko si  imara sana.

 

Uwekezaji sahihi

Kuhusu uwekezaji sahihi, Mbaga anasema kama ilivyo kwenye mbio ndefu, hali kadhalika katika uwekezaji wa muda mrefu, mwekezaji asianze kuwekeza kiwango kikubwa cha fedha, hata kama mwekezaji anakiwango kikubwa cha mtaji kwa ajili hiyo. Kitaalam inashauriwa kuziwekeza kwenye mfuko salama kama Liquid Fund na kuhamisha fedha hizo kwenda kwenye sehemu nyingine za uwekezaji taratibu sawa na mahitaji.

Hii itamsaidia mwekezaji kutawanya uwekezaji na kupunguza athari za uwekezaji.

Tuhitimishe makala yetu kwa mfano wa mbio za marathon kwamba: “Wakati wa kumaliza mbio mkimbiaji hatakiwi kusimama hapo hapo bali kukimbia taratibu kwa umbali kidogo kabla ya kupumzika.

Vivyo hivyo inashauriwa kuwa baada ya kuwekeza kwa miaka kadhaa na kutimiza lengo lake, haitakiwi kuwa mwisho wa kuwekeza isipokuwa labda awe amefikia umri wa kustaafu au amepata matatizo ya kifedha labda kama amefanya tathmini na kuona anapoteza muda na hakuna faida anayopata.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles