23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

UWEKEZAJI UMEME WATAKA MTAJI DOLA BILIONI 46.2

Na Joseph Lino,

TANZANIA itahitaji uwekezaji wa Sh trilion 103.3, sawa na Dola za Marekani  bilioni 46.2  katika kipindi cha miaka 20 ijayo kwenye kuzalisha nishati ya umeme.

Ripoti ya Power System Master Plan (PSMP 2016 – 2040) iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini hivi karibuni, inaonesha Tanzania inatarajia kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawati 1,583  ya sasa kufikia  zaidi ya MW10,000 katika kipindi cha miaka 10 ijayo.

Kwa mujibu wa PSM, Serikali itagharamia asilimia 70 ya miradi na miundombinu ya nishati ya umeme kupitia mikopo na vyanzo vyake vingine.

Asilimia 80 ya gharama zitakazotumika zitawekezwa katika uzalishaji wa umeme na gharama nyingine zitatumika katika usambazaji na katika kujenga vituo vya kusambazia umeme.

PSMP inasema sasa asilimia 40 ya Watanzania  milioni 50  wanafikiwa na huduma ya nishati ya umeme na Serikali inataka kufikisha huduma ya umeme kwa asilimia 90 ifikapo mwaka 2035.  

Pia inaelezea kwamba mahitaji ya umeme yataongezeka kwa asilimia 71 kutoka GWh 7,860 mwaka jana kufikia GWh 13,430 mwaka 2020.

Sababu zinazochangia ongezeko la nishati ya umeme ni ukuaji wa pato la taifa ambayo ni wastani wa asilimia 7 kila mwaka, ikichangiwa na ukuaji wa maendeleo ya matumizi ya gesi, miundombinu ya usafiri na ongezeko la uwekezaji kutoka nje (FDI).

Pia miuondombinu ya gesi itahamasisha biashara ya uhakika ya gesi kama kemikali na gesi asilia na viwanda vya usafirishaji. Viwanda hivyo hutumia nishati ya umeme katika shughuli zake.

Matumizi ya viwanda ya nishati ya umeme yanatarajia kukua kwa asilimia 18 kufikia mwaka 2020, ikiwa ukuaji wake utakuwa kwa wastani wa asilimia 11 katika viwanda na asilimia 13 kwa upande wa matumizi ya biashara za kawaida.

Kwa upande wa matumizi ya  majumbani ya umeme, yataongezeka kwa wastani wa asilimia 11 kila mwaka hadi kufikia 2040.

Viwango vya gharama ya umeme tangu mwaka 2015 vilikuwa asilimia 41, bado kuna nafasi ya kuongezeka kufikia asilimia 50 ifikapo 2020 na asilimia 90 mwaka 2035.

Matumizi ya nishati ya umeme kwa kila mtu (per capita) nchini ni kwh 137  kwa mwaka jana, kiasi kidogo ikilinganishwa na Kenya.

Lakini kwa siku za usoni itakuwa kWh 240 kwa kila mtu kufikia 2020 na kWh 1,050 mwaka  2040.

Kwa umeme unaozalishwa, bado haukidhi mahitaji kwa sasa lakini ripoti hiyo inasema kuwa upungufu wa umeme utapungua kwa kiasi kikubwa kuelekea mwaka 2020.

Kwa hali ya sasa, Tanzania huzalisha umeme wa gridi ya taifa wa MW 1,356.59 ambayo ni pamoja na umeme wa MW 566, sawa na asilimia 42, gesi asilia MW 607 ambayo ni asilimia 45 na mafuta mazito MW 173 sawa na asilima 13.

Serikali inatarajia kuongeza uzalishaji na kufikia MW 10,000 ifikapo 2025.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles