33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Uwekezaji ulivyowapa utajiri mkubwa Jay Z, Rihanna 

NA CHRISTOPHER MSEKENA

HAKUNA msanii duniani anayemfikia kwa utajiri rapa Shawn Carter ‘Jay Z’. Hakuna mwanamuziki wakike mwenye utajiri mkubwa kama alionao Robyn Fenty ‘Rihanna’ kwa mujibu wa Forbes.

Jarida la Forbes linaloaminika duniani kwa kutoa orodha mbalimbali za watu maarufu na utajiri wanaoumiliki, limebainisha vyanzo vya mapato vinavyofanya wawili hao wawe na utajiri mkubwa zaidi tofauti na wasanii wenzao.

Wameweka wazi kuwa Jay Z kwasasa ni rasmi amekuwa bilionea baada ya kufikisha utajiri wa dola za Marekani Bilioni 1 ambazo ni zaidi ya shilingi Trilioni 2 za Tanzania huku Rihanna akimiliki utajiri wa dola za Marekani milioni 600 sawa na shilingi Trilioni 1.3.

Swaggaz, tunakupa mchanganuo rahisi wa vyanzo vya mapato vya Jigga na Rihanna kama ambavyo Forbes wamebainisha kwenye orodha zao, karibu ujifunze zaidi.

JAY Z

Mara kadhaa orodha ya utajiri imekuwa ikiongozwa na P Diddy, Jay Z na Dr Dre lakini safari hii ‘bae’ wa Beyonce ameshikilia namba moja na kuweka rekodi ya kuwa msanii wa kwanza kufikisha utajiri wa dola bilioni 1.

Vyanzo vyake vya mapato vimewekwa wazi. Jay Z ni mwanamuziki, mfanyabiashara na mwekezaji kwenye miradi mbalimbali katika tasnia ya muziki na ujasiliamali.

Ikumbukwe kuwa Forbes hawatoi hesabu za fedha taslimu wanazomiliki wasanii bali wanahesabu thamani ya uwezekezaji aliofanya msanii husika, mapato ya kazi zake na vitega uchumi vingine.

Kwa muktadha huo, Jay Z anapiga sana pesa kwenye uwekezaji wa shampeni yake inayoitwa Armand de Brignac inayouzwa shilingi 29,850 kwa chupa moja na kinywaji hicho humwiingizia dola za Marekani milioni 310 kwa mwaka.

Rapa Jay Z, benki ana akiba inayokadiliwa kuwa ni dola za Marekani milioni 210 huku pombe yake kali inayoitwa D’Usse unayouzwa shilingi 91,800 na kuendelea kulingana na ukubwa wa chupa hivyo jumla imemwingizia dola milioni 100.

Jay Z pia anatengeneza kiasi cha dola za Marekani milioni 100 kupitia mtandao wake wa kusikiliza nyimbo (music streaming service) unaoitwa Tidal ambao ndani yake zinapatikana kazi za wasanii wakubwa duniani Kanye West, Coldplay, Beyonce, Nicki Minaj, Madonna, Usher na wengine huku ukichuana vikali na mtandao wa Spotify.

Pia rapa huyu anamiliki lebo ya muziki ya Roc Nation iliyowahi na inayoendelea kufanya kazi na wasanii kama Dj Khaled, marehemu Nipsey Hussle, Shakira, Alicia Keys, Rihanna, Beyonce, Big Sean na wengine wengi.

Lebo hiyo aliyoianzisha mwaka 2008, ina thamani ya dola za Marekani milioni 75 sawa na mapato yanayotokana na mauzo ya muziki hasa albamu zake ikiwamo ile ya 4:44.

Hali kadharika sanaa ambazo amekuwa akizifanya sehemu mbalimbali ikiwamo mavazi ya Roca Wear ambazo thamani yake ni dola milioni 70.

Hali kadharika, Jigga amefanya uwekezaji katika usafiri maarufu duniani wa Uber sambamba na kuwekeza kwenye ardhi kwa kujenga majumba ya kifahari kama vile Bel-Air Estate na East Hampton Mansion ambazo zina thamani  ya Dola milioni 70.

JAY Z, BEYONCE WAJIPONGEZA

Kwa mara ya kwanza baada ya kutangazwa kuwa Jay Z ndiye msanii wa kwanza kuwa bilionea, rapa huyo na mke wake Beyonce walikwenda kuburudika kwa mchezo wa mpira wa kikapu, usiku wa kuamkia juzi kwenye uwanja wa Courtside Oracle Arena katika fainali za ‘game’ 3 ya NBA kati ya Golden States Warriors na Torinto Raptors.

Inadaiwa wawili hao walikaa viti vya mbele ambavyo kawaida huwa vinalipiwa shilingi milioni 190 lakini kwao viti hivyo vikauzwa kwa dola elfu 92 ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 200.

RIHANNA 

Unaweza ukashangaa kwanini Rihanna ametajwa kama mwanamuziki wakike mwenye utajiri mkubwa zaidi licha ya kutotoa  wimbo wowote toka alipoachia albamu yake ANTI mwaka 2016.

Nje ya muziki Rihanna ni mjasiliamali na mwekezaji katika tasnia ya mitindo na urembo, amekuwa akiingia ubia na kampuni mbalimbali kubwa ambazo zimechangia kipato chake kuongezeka.

Mrembo huyo kutoka visiwa vya Barbados, ameowaburuza wanamuziki wengine kama Madonna mwenye utajiri wa dola 570, Céline Dion mwenye dola 450 na Beyoncé mwenye utajiri wa dola 400.

Vyanzo vikuu vya mapato kwa Rihanna ukiacha muziki ni bidhaa zake za urembo kama vile rangi za kucha na midomo zenye chapa Fenty Beauty, bidhaa iliyozinduliwa kwa kishindo mwezi Septemba, 2017 na kwa wastani mwaka jana ndani ya miezi 15 toka izinduliwe zikaingiza mapato ya dola za Marekani milioni 570.

Pia Rihanna ni mbia wa kampuni ya Kifaransa, LVMH (Louis Vuitton Moet Hennessy), inayozalisha bidhaa za kifahari kama vile mvinyo, mavazi ya ngozi, saa za mkononi na manukato yenye chapa Fendi.

RIHANNA AKODI KISIWA KUANDAA ALBAMU

Mtandao wa Mirror umeripoti kuwa Rihanna, ambaye amekuwa akiishi nchini Uingereza tangu mwaka jana, amekodi kisiwa na studio za ‘State of the Art’ zilizopo visiwa vya Oseate,  ambacho kinagharibu Paundi 20,000 ambazo ni sawa na shilingi milioni 58 kwa siku moja lengo likiwa ni kupata utulivu wa kuandaa albamu yake ya tisa inayotajwa itaitwa R9.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles