25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

UWAJIBIKAJI, MBINU ZA AMUNIKE SILAHA YA KUVUNA MATOKEO NELSON MANDELA

Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike

NA MAREGES NYAMAKA              |              


ZIMEBAKI siku sita kabla timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kushuka dimbani kuumana na timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’, mchezo wa kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon).

Taifa Stars na Uganda ziko kundi L pamoja na timu nyingine mbili zinazotarajia pia kuzivaa Cape Verde dhidi ya Lesotho, huku The Cranes ikiwa vinara baada ya kuvuna pointi tatu.

Cranes ilivuna pointi hizo dhidi ya Cape Verde, ilipokubali kichapo cha bao 1-0, mchezo uliopigwa Uwanja wa Estádio da Várzea. Bao la Cranes lilifungwa na Geofrey Sserunkuma dakika ya 83.

Stars itakuwa ugenini katika mchezo huo unaotarajiwa kupigwa Uwanja wa Mandela, zamani ukijulikana kama Namboole, kila timu ikisaka tiketi kufuzu michuano hiyo mikubwa itakayofanyika mwakani nchini Cameroon.

Kikosi hicho chini ya kocha mpya, Emmanuel Amunike, raia wa Nigeria,  kinashuka dimbani kikiwa na kumbukumbu kuanza kampeni zake kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Lesotho, mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.

Kutokana na rekodi bora ilizonazo Cranes, hasa katika uwanja wao huo wa nyumbani dhidi ya timu kubwa, baadhi ya Watanzania wameingiwa na woga.

Hatua hiyo inachagizwa na miongoni mwa timu bora barani Afrika kuwahi kupoteza michezo yao, ambazo ni Misri iliyopoteza kwa bao 1-0 Agosti 31 mwaka jana, lililofungwa na mshambuliaji Emmanuel Okwi.

Cranes ilipata ushindi dhidi ya Mafarao hao katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia, kabla ya kugeuziwa kibao  ugenini nchini Misri.

Mbali na Misri, timu nyingine zilizowahi kukumbana na hali ngumu Nelson Mandela ni Ivory Coast, iliyolazimishwa suluhu, kama ilivyokuwa kwa Malawi katika mchezo wa kirafiki.

Oktaba 7, 2017, Ghana iliyokuwa na mastaa kama Asamoah Gyan, Andrew Ayew, iliambulia kuvuna pointi moja pekee baada ya pambano kumalizika kwa suluhu, huku Congo (DRC) ikiambulia sare ya bao 1-1, mechi zote mbili zikiwa za kuwania kufuzu Kombe la Dunia.

Tangu kuanza kwa mwaka huu, ni timu ya Taifa ya Namibia pekee iliyofanikiwa kuvuna pointi tatu, baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0, hiyo ilikuwa  Januari 18, ukiwa mchezo wa  michuano ya wachezaji wanaocheza Ligi ya Ndani (CHAN).

Lakini pamoja na rekodi hizo nzuri za  Cranes, ikionyesha ugumu ilionao inapocheza katika uwanja wake wa nyumbani, shaka nyingine inayoonekana ni hatua ya Kocha wa     Taifa Stars, Emmanuel Amunike, kuwaondoa nyota sita wa Simba na mmoja wa Yanga katika orodha yake.

Hawa ni pamoja na beki mzoefu, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, John Bocco, Mzamiru Yassin na Jonas Mkude, kwa upande wa Simba pamoja na Feisal Salum wa Yanga.

Nafasi za wachezaji hao zilizibwa na wachezaji wasiokuwa na uzoefu  mkubwa kutoka timu za Mtibwa Sugar, Tanzania Prisons na Lipuli.

Ni sawa uzoefu una asimilia kubwa  kwa mchezaji kuisaidia timu, Amunike alisimamia nidhamu katika uamuzi wake, lakini pia aliamini katika uwajibikaji.

Lakini pia bado kikosi kina wachezaji wengi wazoefu kama kina Aishi Manula, Agrey Morris, Kelvin Yondani, Abdi Banda, Himid Mao, Simon Msuva na nahodha Mbwana Samatta.

Hakuna kingine zaidi kinachoweza kuipa matokeo bora Stars zaidi ya mbinu na uwajibikaji.

Hiyo inatokana na The Cranes kuwa na idadi kubwa ya wachezaji wengi wanaocheza soka nje ya nchi katika ligi  ambao kiufundi wako vizuri zaidi sambamba na uwajibakaji wa mchezaji mmoja mmoja.

Kwa mujibu wa viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), vilivyotoka Agosti, Uganda inashika nafasi ya 82, huku Taifa Stars ikishika nafasi ya 140.

Ikumbukwe kuwa, timu hizo mbili zimekutana mara 53 katika mashindano mbalimbali, Stars ikifanikiwa kushinda mechi 10, sare 14, huku ikichapwa mara 29.

Taifa Stars

Makipa: Aishi Manula wa Simba SC, Mohammed Abdulrahman Wawesha (JKU), Benno Kakolanya (Yanga).

Mabeki ni Salum Kimenya (Tanzania Prisons), Hassan Kessy (Nkana FC, Zambia), Paul Ngalema(Lipuli) Gardiel Michael (Yanga SC), Ally Sonso (Liupuli), David Mawntika (Azam), Abdi Banda (Baroka FC, Afrika Kusini), Kelvin Yondan (Yanga SC), Aggrey Morris (Azam FC) na Andrew Vincent ‘Dante’ (Yanga SC).

Viungo ni Himid Mao (Petrojet FC, Misri), Mudathir Yahya (Azam FC), Frank Domayo (Azam ), Salum Kihimbwa (Mtibwa Sugar), Simon Msuva (Difaa Hassan El-Jadida, Morocco), Shiza Farid Mussa (CD Tenerife, Hispania).

Washambuliaji ni Rashid Mandawa (BDF XI, Botswana), Yahya Zayed (Azam FC), Shaaban Iddi Chilunda (CD Tenerife, Hispania), Kelvin Sabato, (Mtibwa Sugar), Emmanuel Ulimwengu (El HIlal, Sudan) na Nahodha Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji).

Kikosi cha Cranes

Kipa: Denis Onyango (Mamelodi Sundowns), Jamal Salim (El Meriekh), Charles Lukwago (KCCA FC) na Nicholas Sebwato (Onduparaka FC),

Mabeki: Isaac Isinde (Kirinya Jinja SS), Murushid Juuko (Simba SC), Timothy Awanyi (KCCA FC), Denis Iguma (Kazma FC), Nicholas Wadada (Azam FC), Musitafa Mujuzi (Proline FC), Godfrey Walusimbi (Gor Mahia) FC, Isaac Muleme (Haras El Hodood),  Joseph Ochaya (Lusaka Dynamo),

Viungo: Hassan Wasswa (El Geish), Khalid Aucho (Un attached), Ibrahim Saddam Juma (KCCA FC), Tadeo Lwanga (Vipers SC), Opondo Moses (Vendsyssel), Allan Kateregga (Cape Town City), Faruku Miya (Gorica), Moses Waisswa (Vipers Sc), William Luwagga Kizito (FC Bate Borisov), Yasser Mugerwa (Fasil Kenema).

Washambuliaji: Yunus Sentamu (FK Tirana),  Martin Kizza (Sc Villa Jogoo), Allan Kyambadde (KCCA FC), Emma Okwi (Simba SC), Edrisa Lubega (SV Ried), Derrick Nsibambi (Smouha), Patrick Kaddu (KCCA FC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles