27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

UVUNJIFU WA AMANI WAMSHTUA MAALIM SEIF

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesena anashtushwa na vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyoendelea kutokea nchini.

Kutokana na hali hiyo, ameitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuandaa mjadala maalumu wa kitaifa kujadili juu suala la uvunjifu wa amani unaoendelea.

Maalim Seif aliyasema hayo jana wakati  wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Vijana ya CUF, Wilaya ya Kaskazini A Unguja.

Alisema kuwa kutokana na vitendo vinavyoendelea kwa sasa nchini, kuna haja ya kuitisha mjadala wa kitaifa utakaotoa taswira na mwongozo mwema katika taifa.

“Ni vyema mjadala huo pia ukashirikisha watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa dini,” alisema Maalim Seif.

Alisema ni jambo la kushangaza kwa sasa kuona maisha ya Watanzania kuwa hatarini, hivyo ni vyema Serikali ikakubali kuweka mjadala wa kitaifa uweze kueleza ni nsehemu gani ambayo imejikwaa hadi kufikia hapa.

Alieleza kuwa Tanzania ilikuwa ikitambuliwa kama kisiwa cha amani na kudai kuwa kitendo cha kuvamiwa ofisi za mawakili na kupigwa risasi mbunge ni kuonyesha sifa ya Tanzania imepotea.

Aliongeza kuwa haiwezekani mbunge akitokea kwenye majukumu yake anapigwa risasi hovyo, tena mchana kweupe  na wahusika kutopatikana hadi leo jambo ambalo likilelewa ni hatari kwa taifa hili.

Alisema Watanzania wamekuwa waoga ndani ya nchi yao jambo ambalo ni baya katika taifa ambalo lilikuwa likisifika kwa amani na upendo.

“Kufumbiwa macho na kuendelea kwa vitendo hivyo bila kuchukuliwa hatua, ni sawa na kutoa baraka vitendo  viendelee jambo ambalo linatia hofu na kutishia uchumi wa nchi kama taifa litakaa kimya.

“Kunahitajika kuwepo kwa juhudi za makusudi na tuzingatie maoni ya Watanzania katika kuleta amani, ni lazima sote tushiriki katika kupata njia ya kuinusuru nchi yetu,” alisema Maalim Seif.

Sambamba na hilo, amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuipokea amri ya Rais Dk. John Magufuli katika kulifanyia kazi tukio la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) kama wanavyozifanyia kazi amri nyingine kutoka juu.

“Ukiligusa jeshi letu linakuambia linafanya kazi kisayansi, basi tunataka kuiona sayansi yao kwenye tukio hili ikitumika kwa kuwa ni kitendo cha kinyama na hakivumiliki. Tunaomba uchunguzi huu kisayansi ufanywe kwa haraka kwani taifa limo katika hofu kubwa,” alisema.

Alisema kitendo alichofanyiwa Tundu Lisu ni cha kinyama, na kikatili ambacho alidai hakivumiliki katika ulimwengu huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles