UVCCM YAAZIMIA KUWALINDA JPM, SHEIN

0
407

Na SARAH MOSES -DODOMA          |               


BARAZA Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) limeazimia kwa kauli moja kuwalinda Rais Dk. John Magufuli na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Ali Mohamed Shein, dhidi ya uharamia wowote kutoka ndani au nje ya nchi.

Pia limeahidi kuifanyia kazi hotuba ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, kwa sababu wameipokea kama maelekezo na kuahidi kuyafanyia utekelezaji kuanzia ngazi ya tawi.

Akizungumza jijini hapa jana, Katibu Mkuu wa UVCCM, Raymond Mwangwala, alisema waliazimia mambo saba katika kikao chao cha kuwapata wajumbe wa kamati ya utekelezaji.

Alisema wapo tayari kukabiliana na changamoto yoyote na wanaamini kuwa vijana kwa sasa lazima waungane wawe na umoja.

Akitaja maazimio mengine, alisema ni pamoja na kuitaka Serikali kuweka mazingira rafiki kwa vijana waliohitimu vyuo vikuu kupata nafasi za kujitolea katika taasisi, idara, mashirika na mamlaka ya Serikali na sekta binafsi ili kupata uzoefu.

“Pia tunaitaka Serikali kutazama masharti ya taasisi za kifedha ya upatikanaji wa mikopo ili waweze kujiajiri,” alisema.

Pia alisema baraza hilo liliazimia kupitisha mpango mkakati unaokusudia kujitegemea kiuchumi na kuimarisha jumuiya nchi nzima ili kwenda sambamba na dhana ya siasa na uchumi.

Katika hatua nyingine, aliwataja wajumbe walioteuliwa wa kamati ya utekelezaji ya baraza hilo kuwa ni Saitoti Steven na Joanfaith Kataraiya kutoka Bara na Abdulghafar Juma na Mariam Juma kutoka Zanzibar.

Pia alisema kikao hicho kilipokea na kuwathibitisha wakuu wa idara tano za UVCCM Taifa ambao ni Peter Kasera kuwa Katibu wa Idara ya Organaizesheni, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Lusekelo Nelson kuwa Katibu wa Idara ya Uchumi, Uwezeshaji na Fedha, Kamana Simba kuwa Katibu wa Idara ya Vyuo Vikuu, Hassan Bomboko kuwa Katibu wa Idara ya Uhamiaji na Chipukizi na Mohamed Abdallah kuwa Katibu wa Idara ya Usalama na Maadili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here