24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Utata waibuka aliyechunwa ngozi Mkuranga

IGP Mangu
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Mangu

Na Aziza Masoud, Dar es Salaam

SIKU moja baada ya gazeti hili kuripoti juu ya tukio la mkazi wa Kijiji cha Dondo, wilayani Mkuranga mkoani Pwani, Hamisi Maimbwa (20) kufariki dunia baada ya kudaiwa kuchunwa ngozi mwili mzima na watu wasiojulikana, utata mkubwa umeibuka kuhusu tukio hilo.

Wakati ndugu na mmoja wa viongozi wa zahanati iliyomtibu Maimbwa kabla mauti hayajamkuta wakidai kuwa kijana huyo alichunwa ngozi, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Athumani Mbambalaswa na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Dk. Francis Mwanisi, wamedai kuwa taarifa za awali zinaonyesha kuwa marehemu alijichoma moto.

Tukio hilo la kinyama lililotokea Jumatano wiki hii, saa mbili usiku, baada ya wakazi  wa eneo hilo kumkuta Maimbwa akiugulia kichakani, kabla ya kumpeleka katika zahanati ya Kisiju kwa matibabu.

Hata hivyo, wakati Kaimu Kamanda wa Polisi Mbambalaswa na Mganga Mkuu wa Wilaya wakitoa kauli hiyo, mmoja wa viongozi wa zahanati ya Kisiju ambaye aliomba ahifadhiwe jina lake, aliliambia gazeti hili  walimpokea kijana huyo katika zahanati hiyo saa tano usiku baada ya kupelekwa na ndugu zake na baada ya kumuangalia vizuri, waligundua kuwa hajaungua na moto.

“Tulimpokea akiwa hai huku akiwa anaugulia maumivu makali, alikuwa na majeraha ambayo tulishindwa kuyatambua, awali tulipomuona tulidhani ameungua na moto, lakini tulipomsogelea karibu alikuwa anaonyesha kama amemwagiwa kitu jamii ya tindikali. Tulimpokea akiwa  hana ngozi ya juu mwili mzima ilikuwa imebaki ngozi nyeupe ya ndani tu,” alisema kiongozi huyo.

Alisema marehemu baada ya kupokelewa usiku alianza matibabu ya awali pamoja na kuchukuliwa sampuli za ngozi kwa ajili ya vipimo.

Kwa mujibu wa tabibu huyo,  baada ya vipimo vya awali usiku wa Jumatano Maimbwa alilazimika kulazwa hospitalini hapo na alikaa kwa muda wa saa saba kabla mauti hayajamfika  juzi saa 11 asubuhi.

Kwa upande wa dada wa marehemu, Rehema Athumani, alidai kuwa  mdogo wake alichunwa ngozi akiwa hai, hivyo kutokana na hali hiyo familia imeamua kufanya uchunguzi kuhusu tukio hilo na taarifa za awali kutoka kwa wanakijiji zinaeleza siku moja kabla ya tukio kuna wanaume wawili wasiofahamika walionekana kijijini hapo.

“Familia tumekubaliana kufanya uchunguzi wetu binafsi ili kupata chanzo cha tukio na wahusika jana (juzi) tulipokuwa makaburini kuna watu walisikika wakiongea kuwa kuna watu wawili wageni walionekana kijijini kwetu siku moja kabla ya tukio.

“Tumefanikiwa kujua walikofikia kwa nani, tunajipanga kwenda kuwauliza watuambie wale watu ni wakina nani na walifuata nini,” alisema Rehema.

Alisema wao kama familia wamekwishajiridhisha kuwa ndugu yao hajaungua kwa kuwa kuna baadhi ya viungo ambavyo vilikuwa  havijatolewa  ngozi.

“Ule siyo moto, polisi wameweka tu baadhi ya vitu kupoteza ushahidi, moto gani unamuunguza mtu nusu, tulipompeleka hospitali alikuwa anaangalia kabisa macho yalikuwa mazima na viganja vya mkono, miguu na kichwa vyote vilikuwa havijatoka ngozi,” alisema Rehema.

Alisema kabla ya kuuchukua mwili huo katika kituo cha afya na kwenda kuuzika hospitali walichukua vipande vya  vyama kiganjani na miguuni na kuomba kwenda kuvitumia  kwa ajili ya vipimo.

Hata hivyo kwa upande wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Mwambalaswa, alisema kuwa taarifa za kuungua kwa moto kwa kijana huyo ziliripotiwa Agosti sita saa mbili usiku katika kituo cha polisi Mkuranga na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Saidi Matitu, ambaye alidai kuwa wananchi walimkuta kijana huyo anaungua kichakani katika eneo la Dondo.

Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa baada kupata taarifa, maofisa wa polisi walitoka na kwenda katika eneo la tukio ambalo lipo kilomita 45 kutoka kituoni hapo.

“Eneo lipo mbali na kituo, lakini askari walifika japokuwa walichelewa, walipofika walimkuta kijana huyo akiwa ameungua na pembeni kulikuwa na kiberiti, chupa ya soda yenye mabaki ya petroli, nguo zilizoungua na mabaki ya ngozi, inasemekana alikuwa na maradhi ya muda mrefu,” alisema Kamanda Mwambalaswa.

Alifafanua kuwa baada ya taratibu zote mwili ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya kuzikwa na vielelezo hivyo vimechukuliwa na kuhifadhiwa katika kituo cha polisi cha Mkuranga.

Alipotafutwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Dk. Francis Mwanisi, alisema sampuli za ngozi zilizotolewa katika mwili wa Maimbwa zimekwishapalekwa katika ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kujiridhisha, japokuwa picha ya awali inaonyesha mwili huo uliungua na moto.

Dk. Mwanisi alitoa kauli hiyo jana, baada ya kikao cha muda mrefu  kati yake na Mkurugenzi wa Wilaya hiyo.

Awali Dk. Mwanisi alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa alikuwa katika kikao hicho.

Hata hivyo alikuja kuzungumza baadaye baada ya gazeti hili kumweleza juu ya umuhimu wa yeye kuzitolea ufafanuzi taarifa hizo.

“Sample (sampuli) tumechukua, lakini picha inayoonekana ni kama mtu aliyejimwagia petroli akajichoma moto na  alipopokelewa kwenye zahanati alikuwa anaongea, lakini ukimuuliza nini kimemtokea alikuwa hajibu,” alisema Dk. Mwanisi.

Alisema majibu ya vipimo ambayo yataondoa utata wa tukio hilo yanatarajiwa kutoka muda wowote  kuanzia sasa.

HOFU YAZUKA

Wakati huo huo, taarifa za kudaiwa kuchunwa ngozi Maimbwa zimeibua hofu kubwa wilayani humo, ambapo jana wananchi wa kijiji cha Kitomondo, Wilaya ya Mzaya, walidai kupata taarifa juu ya kuwako kwa watu waliotaka kumkamata mtoto ambaye alikuwa akienda kisimani kuchota maji.

Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa wanakijiji wa eneo hilo alisema wakati watu hao wakimkimbiza mtoto huyo walitokea wanakijiji wachache ambao walikuwa wakitokea kisimani, ndipo vijana hao walipokimbia na kumuacha mtoto huyo ambaye aliamua kurudi nyumbani kwa hofu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles