UTALII WA UVUVI SELOUS WAINGIZA MILIONI 198/-

0
347
Mtalii akiwa amemvua samaki aina ya "Tiger Fish" Mto Kilombero.
Mtalii akiwa amemvua samaki aina ya “Tiger Fish” Mto Kilombero.

Na MWANDISHI WETU – MOROGORO


SEKTA ya utalii wa Uvuvi ndani ya Mto Ruaha, eneo la Wilaya ya Kilombero na Msolwa inayopatikana Pori la Akiba Selous Kanda Kaskazini Magharibi – Msolwa imefanikiwa kukusanya mapato ya Dola za Marekani 87,000 sawa na Sh milioni 198. 1 kwa mwaka jana pekee.

Hayo yameelezwa leo kwenye ziara ya wanahabari wanaotembelea pori hilo kwa lengo la kujionea shughuli za uhifadhi na mchango wa kiuchumi kutoka kwenye uwindaji wa kitalii unaosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA).

Akizungumza na MTANZANIA Digital, Mkuu wa Kanda, Augustine Ngimilanga, amesema utalii huo umekuwa ukiwavutia watalii kila mwaka tofauti na zamani.

“Watalii wengi Kanda yetu wanapendelea kuja kuvua samaki aina ya “Tiger Fish” mwaka jana tulipokea watalii kati ya 32 mpaka 38 na kufanikiwa kukusanya mapato ya Dola za Marekani 87,000,” amesema Ngimilanga.

Kutokana na kuongezeka kwa watalii hapa amesema juhudi za kuboresha maeneo ya uvuvi zinaendelea kufanywa ili kuvutia wageni wengi zaidi kufika maeneo husika.

“Tukiboresha zaidi maeneo ya uvuvi tutapata mapato zaidi ya haya na kazi hii tunaendelea nayo, wageni wanavutiwa zaidi kuvua ‘Tiger Fish.’

“Aina hii ya Samaki ni wakubwa wana meno wanapatikana Mto Kilombero, watalii hupenda kuwavua na wakivuliwa hupimwa urefu na uzito kisha wanawarudisha kwenye maji. Sheria za uhifadhi ndani ya Pori la Akiba haziruhusu kuwachukua kwa ajili ya kitoweo hivyo burudani yake huwa ni kuwavua kisha kuwarudisha,” amesema

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here