27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

UTAJIRI KUTOKA MAWASILIANO WAJA

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Ian Ferrao
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Ian Ferrao

Na Justin Damian,

Baada ya mvutano wa muda mrefu kati ya Serikali na makampuni ya simu, hatimaye Vodacom Tanzania imekuwa kampuni ya kwanza ya simu kupiga hatua moja katika utaratibu wa kujiunga na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), kwa kutangaza nia ya kuuza hisa zake za kwanza (IPO).

Katika hatua hiyo ya kwanza, Vodacom Tanzania imepeleka maombi ya muundo na muda wa kujiorodhesha DSE kwa Mamlaka ya Dhamana  na Soko la Mitaji (CMSA). Mamlaka hiyo itapitia maombi hayo kuona kama inakidhi vigezo vya kisheria kabla ya kuiruhusu kuendelea mbele.

Baada ya kujiunga na DSE, Vodacom itajulikana kama Vodacom Tanzania Public Limited Company (Plc). Kujiorodhesha kwa Vodocom katika soko la hisa, kuna maana kwamba sasa wananchi wa kawaida wataweza kumiliki kampuni hii ambayo imekuwa ikitengeneza faida ‘nono’ kila mwaka.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Vodocom Tanzania ndiyo kampuni kubwa zaidi katika soko la huduma za mawasiliano kwa simu za kiganjani kati ya kampuni saba, ikichukua asilimia 31 ya soko na laini milioni 12.06 hadi kufikia Juni  mwaka huu.

Kampuni za Tigo na Airtel zinashikilia nafasi ya pili na ya tatu kwa kuwa na asilimia 29 na 26 ya soko. Kampuni ya Tigo ina laini milioni 11.6, huku kampuni ya Airtel ikiwa na laini milioni 10.3.

Vodacom imekuwa kampuni ya kwanza ya simu kujiorodhesha DSE wakati ukiwa umebaki mwezi mmoja tu kwa makampuni mengine kujiorodhesha, ikiwa ni agizo la Serikali kutaka makampuni yote kujisajili DSE kufikia 1/01/2017.

Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Watanzania wananufaika na biashara hii yenye faida kubwa na kuhakikisha nchi inanufaika zaidi na sekta hii inayokuwa kwa kasi kubwa. Hatua ya kampuni za simu kujisajili DSE itaongeza uwazi wa namna makampuni hayo yanavyoendeshwa na pia itakuwa rahisi kulipa kodi zote zinazostahili kwa Serikali.

Itakumbukwa kuwa kwa miaka kadhaa, Kampuni ya simu ya Vodacom imekuwa kinara katika ulipaji kodi na hatua hii ya kujisajili DSE, kunaweza kusaidia kuongezeka kwa kiasi ilicholipa serikalini kama kodi.

Hatua ya makampuni ya simu kujiorodhesha DSE si geni ila limecheleweshwa kwa njia moja au nyingine kwani ni utekelezaji wa sheria ya Elektroniki na Mawasiliano ya Posta (EPOCA) na Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 inayoelekeza makampuni ya simu kumilikishwa asilimia 25 ya hisa zake kwa wananchi kwa kujiunga na DSE.

Mafanikio haya yanakuja baada ya msuguano mkali na wa miaka mingi kati ya Serikali na makampuni haya ambayo mengi ni makubwa na ya kigeni kwa kuwa wakati mwingine sheria zao hukinzana na za kwetu na hivyo kuhitaji utangamano wa kisheria.

Chama cha Wenye Makampuni ya Simu Tanzania (MOAT) kilikuwa kikipinga vikali hatua hii kwa madai kuwa ni kinyume na sheria mbalimbali ikiwamo Sheria ya Makampuni, Sheria ya Soko la Mitaji na hata Katiba ya nchi kwenye kipengele cha umiliki wa mali binafsi.

Mengi yalitokea wakati wa mchakato wa muswada wa kuyataka makampuni ya simu kujiunga na DSE kama sharti la leseni. Mwenyekiti wa Bodi ya DSE, Peter Mchunde, alijiuzulu nafasi yake kwa kile kilichodaiwa kupinga Muswada huo ambao hata hivyo Rais Jakaya Kikwete aliusaini kuwa Sheria.

Mchunde alimwandikia Rais Kikwete na kumweleza kuwa, kuyalazimisha makampuni ya simu kujiunga na DSE kungeyafanya makampuni yenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya mawasiliano ya simu kukata tamaa na kuachana na mpango wa kuwekeza kwenye sekta hii.

Wachunguzi wa mambo wanasema kama sababu ndiyo hiyo, Mchunde alionesha udhaifu mkubwa wa uzalendo na uongozi kwani ni wazi wenye kampuni wao hufuata faida popote ilipo na si mapenzi au kuburuza nchi. Kwao kila kitu ni fursa.

Hata hivyo, hofu ya makampuni ya simu kujiunga na DSE inatokana na hofu ya kupungua kwa kiwango cha faida wanachokipata kutokana kuwa mara tu watakapojisajili na watu kununua hisa, watatakiwa kuweka wazi hesabu zao za fedha na gharama zao nyingine za uendeshaji kwani wanawajibika na sheria ya mitaji kufanya hivyo.

Itakumbukwa kuwa hatua ya Muswada ilipokelewa vizuri na Chama cha Madalali ambao walisema makampuni ya simu yalikuwa yakihofia kujisajili DSE kwa kuogopa kuweka wazi taarifa zao za kifedha.

Pamoja na kwamba Vodacom imekuwa kinara wa kulipa kodi miongoni mwa makampuni ya simu, haijawahi kuweka wazi hesabu zake na kuonyesha kwa mfano mapato yake kwa mwaka ni shilingi ngapi pamoja na matumizi yake. Ukitaka kupata itabidi uulize Uingereza au Afrika Kusini ambako imesajiliwa.

Makampuni mengi yamekuwa yakijificha nyuma ya sheria ya kodi ya Tanzania ambayo inasema kiasi anacholipa mtu au kampuni ni siri yake ambayo haiwezi kutolewa kwa umma, labda kama taarifa hizo zitahitajika na vyombo vya sheria.

Hatua hii ya kuyalazimisha makampuni ya simu ambayo yanatengeneza faida kubwa itasaidia sana katika kuweka uwazi katika uendeshaji wa makampuni haya ambapo pia Watanzania wataweza kuyamiliki kwa dhana nzima ya kuwa na hisa na kuvuna faida. Serikali kwa upande wake pia itaweza kupata mapato zaidi kwa kuwa kila kitu kitakuwa wazi.

Kimsingi faida ya kampuni hizo zinalingana  na modeli ya uchumi wa mafuta na gesi na hivyo huwa ni fedha nyingi sana, ingawa bei ya mauzo kiwango chake ni kidogo. Kadiri kampuni ikiwa na wateja wengi ndivyo inavyotengeneza faida.

Mamlaka ya Hisa na Mitaji (CMSA) itayapitia maombi hayo ya Vodacom, ikitazama kwa undani namna inavyoweza kutekeleza utoaji taarifa na hatari za utendaji kabla ya kuorodheshwa kwenye soko la DSE na aina ya ushiriki wake sokoni.

“Tunafurahi kuutangazia umma kuwa tumeleta maombi yetu rasmi ya Kujiunga na nia ya kutekeleza mahitaji ya Sheria na muundo na ratiba kamili ya  kujiunga kama muhtasari wa nia ya Kampuni yetu unavyosema,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Ian Ferrao.

Hii ni kampuni ya kwanza, nyingine ni Airtel, Tigo, Halotel, TTCL, Smart na Zantel.

Serikali ilishatangaza TTCL ambayo inaimiliki kwa asilimia 100 itaingia soko la hisa mwakani na Airtel ambayo ina asilimia 40 ya umiliki inajipanga, wakati Halotel ndio kwanza imeingia sokoni na huenda ikasubiri hadi miaka mitatu ipite kama sheria inavyoruhusu na hakuna kauli kutoka Smart. Kuhusu Zantel, asilimia 15 ya hisa ni mali ya Serikali ya Zanzibar na ilisajiliwa kule.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles